Tango: TRA wamenihujumu


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

UKITAKA kujua kwa macho madhara ya ufisadi, kutana na Verani Tango, mfanyabiashara anayemiliki kampuni ya Tango Transport Ltd., ya jijini Arusha.

Na ni vizuri ukakutana naye nyumbani kwake. Akikukaribisha muonane nyumbani kwake, itakuwa bora zaidi. Mbele ya nyumba yake, barabara ya Mbezi Beach, nje kidogo ya jijini Dar es Salaam utakuta magari matatu yaliyochakaa.

Magari hayo pamoja na matela yake, anasema Tango hafahamu hasa ni lini yameegeshwa, lakini anakumbuka kwamba “ni kwa miaka mingi yapo hapo maana hayana kazi ya kufanya. Sina kazi ya kufanya.”

Kuzungumza na mzee Tango, mwenye umri wa miaka 67, kunahitaji uvumilivu. Mwandishi wa gazeti hili alipopanga kufanya naye mahojiano mwishoni mwa wiki, hakujua hali yake ya afya ilivyo.

Ni mgonjwa anayesikia maumivu kila wakati na mguu wake wa kushoto una bandeji na kuashiria kwamba ana kijeraha kinachouma sana. Maumivu hayo yanamsumbua ingawa ni juzi tu amerudi kutibiwa nchini India.

Anasema, “Nimetoka India juzi tu nilikokwenda kwa matibabu. Hata watoto wangu tulikuwa pamoja huko wakinisaidia. Lakini bado madaktari hawajanieleza tatizo langu hasa ni nini.”

Lakini nakwambia, anatoa macho, “maradhi haya nimeyapata kwa sababu ya walichonifanyia TRA. Walichonitendea ni hujuma ambayo sitaisahau maishani mwangu maana wameniumiza sana kimaisha.”

“Inasikitisha sana. Sasa wanatoa maelezo ya kubabaisha wakati wao wenyewe waliotenda makosa walikiri makosa na kukubali kunilipa baada ya kutambua walikiuka sheria za kukamata mali,” anasema.

Mzee Tango hajamaliza mgogoro na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Mgogoro wao unahusu ukamataji wa magari yake 71, malori na magari madogo, kutokana na amri ya kuyakamata iliyotolewa na TRA tarehe 15 Julai 1997.

Magari hayo yalikamatwa Mwanza, Arusha na Dar es Salaam, mengi yakiwa yamekutwa yamepakia mizigo na kulazimika kushushwa ili kuyadhibiti kwenye maeneo ya TRA.

Kwa mfano, magari yaliyokamatwa jijini Mwanza, mzee Tango anasema, yalikuwa yamepakia shehena ya bidhaa za kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL) iliyokuwa inatoka Dar kwenda Mwanza kupitia Arusha, na Eldoret nchini Kenya.

Kadhia yote hiyo ilianza mwaka 1997 baada ya ofisa wa TRA aitwaye Placidus J. Luoga, ambaye sasa ni Naibu Kamishna wa TRA, kusaini waranti ya kuidhinisha magari ya Tango Transport yakamatwe.

Ukisoma waranti hiyo ya Idara ya Kodi ya Mapato ya TRA unabaini kutolewa kwa amri ya kukamatwa magari yasiyo idadi wala kutajwa namba za usajili kwa lengo la kupata malipo ya faini ya Sh. 5,376,725 kwa kile kilichoitwa “ushuru wa stempu na faini.”

Waranti hiyo inaonyesha kuwa malipo ya ushuru wa stempu ni Sh. 1,362,548 na Sh. 4,014,177 ni za faini.

Waranti imemtaja N. A. Kulindwa kama ofisa wa TRA aliyepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa amri hiyo popote pale magari ya Tango Transport yatakapokutwa.

Ilielekeza kwamba magari yakamatwe na kama yana bidhaa zifilisiwe kwa ajili ya kupata kiasi hicho cha fedha pamoja na gharama za utekelezaji wa amri hiyo.

Mzee Tango analalamika kwamba mpaka leo hii haelewi hasa alikuwa ametenda kosa gani hata TRA kutoa amri ya kukamatwa kwa magari yake.

Anasema baadhi ya magari yake yalikutwa yamezidisha uzito, lakini hilo, anasema lilihusu Wakala wa Mizani na Vipimo aliyeko chini ya wizara ya ujenzi siyo TRA.

“Hawa walishikilia magari yangu kwa siku 90. Tulipojadiliana tulifikia muafaka kuwa walitenda kosa na wakakiri nastahili kulipwa.

“Jambo la ajabu ni kuona wanaleta ubabaishaji hata baada ya kutaka suala hili lisifike mahakamani,” anasema mzee Tango ambaye ametumia wanasheria mbalimbali katika kufuatilia mgogoro wake na TRA ulioingia hadi serikali kuu.

Aliwahi kukutana na waziri mkuu Mizengo Pinda mjini Dodoma na baada ya majadiliano iliamuliwa kuwa suala lake litatuliwe kwa maelewano badala ya kupelekwa mahakamani.

“Waziri mkuu alisema wazi kuwa si busara kulipeleka suala hili mahakamani, badala yake watendaji walishughulikie kiutaratibu kama makubaliano yalivyokuwa.

“Sasa mbona wananibabaisha kwa kuanza kutaja watu wasiohusika na kukwepa ukweli wanaojua,” anahoji.

Mzee Tango alikuwa akiendesha shughuli zake kwa ufanisi huku akiwa ameajiri wafanyakazi wapatao 60, wakiwemo madereva na watumishi wa ofisini Arusha, Dar es Salaam na Mwanza.

Iko wapi hatima ya shughuli zake na wafanyakazi wake, hili ndilo swali linalomtia simanzi nyingi mzee Tango kila akikumbuka.

Anasema kwa muda mrefu ameshindwa kuendelea na shughuli zake kwa sababu baadhi ya magari yake yaliuzwa na TRA ili kujilipa “kile ambacho hawakustahili kisheria.”

Anasema, “Hayo magari unayoyaona hapo nje yamekufa kwa sababu siwezi kuyaendesha kutokana na maradhi. Unavyoniona maisha yamekuwa magumu maana sina biashara yoyote.”

Nje ya nyumba yake, iliyopo eneo la Mbezi Beach, yapo malori matatu yaliyofungamana na matela yakiwa yamechakaa.

Anasema miaka yake ya kwanza shughuli zake zilikwenda vizuri na kufanikiwa kumudu kununua kiwanja na kujenga nyumba eneo hilo ambayo ndiyo anayoishi na familia yake.

Mzee Tango, mzaliwa wa kijiji cha Giti, Hanang Wilayani Mbulu, mwaka 1945, ana familia ya mke, aitwaye Theresia Cosmas, mwenyeji wa Mbulu, na watoto 11 – wanne wakiwa ni wanawake. Anasema ameshindwa kusomesha watoto wake ukiacha wale walioko nje ya nchi.

Analalamika, “Tukio hili limenifundisha jambo moja kubwa. Ukidhulumiwa basi umesababishiwa maisha magumu. Watoto hawasomi sasa na mambo hayaendi.”

Hapendi kujadili elimu yake. “Sikusoma,” ndiyo jibu lake alipoulizwa alivyosoma. Alikulia kijijini Giti ambako alishirikiana na baba yake katika kilimo cha ngano kwenye ekari 8,000 katika shamba la Singusta, eneo la Dareda, kiasi cha kilomita nne kutoka Babati mjini.

Mashamba yalipotaifishwa na serikali, alihama kijijini mwaka 1975 na kuhamia mjini Arusha. Alianza shughuli za usafirishaji bidhaa kwa kutumia malori kumi ya aina ya Scania na Fiat, aliyoyanunua kwa fedha zake.

Aliendelea na kazi hiyo hadi alipopatwa na mkosi wa magari yake kukamatwa na TRA.

0
Your rating: None Average: 4.3 (3 votes)