Tanzania: Aibu tupu Marekani


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Rais Obama na Balozi wa Tanzania Marekani, Bi Majaar

KOSA la jinai la ofisa mmoja wa ubalozi wa Tanzania mjini Washington, linatishia kuvuruga uhusiano kati ya nchi hii na Marekani, MwanaHALISI limeelezwa.

Kwa mujibu wa balozi wa Tanzania mjini Washington, Mwanaidi Maajar,  iwapo serikali haitachukua hatua za haraka kushughulikia suala hilo, kuna uwezekano mkubwa wa uhusiano kati ya Tanzania na Marekani kuvurugika.

Kosa lenyewe linahusu mwambata wa ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Dk. Allan Mzengi ambaye mahakama ya mjini Washington, D.C, imehukumu kulipa fidia ya dola za Marekani 1.05 milioni (karibu Sh. 1.6 bilioni), kwa mwanamke aliyempeleka nchini humo kuwa mtumishi wake wa nyumbani.

Taarifa kutoka ubalozi wa Tanzania mjini Washington, D.C na ikulu jijini Dar es Salaam zinasema, Dk. Mzengi alihukumiwa mwaka jana jijini Washington. Tarehe ya hukumu haikuweza kupatikana haraka.

“Hili ni jambo kubwa sana. Katika hukumu ile ya mahakama, Dk. Mzengi na mkewe wameamriwa kumlipa Bi. Zipora Mazengo kiasi cha dola za Marekani 1.05 milioni,” anaeleza mtoa taarifa.

Katika shauri hilo, Dk. Mzengi alituhumiwa kumsafirisha, kinyume cha sheria hadi nchini Marekani, Bi. Zipora na “kumfanyisha kazi kwa saa 15 kila siku na kushindwa kumrejesha nchini kwa miaka minne hata pale alipofiwa na ndugu yake.”

Chini ya sheria za Marekani, upelekaji mtu yeyote – mwanamke au mwanaume – kutoka eneo moja hadi jingine kwa shabaha ya kumtumikisha, linakuwa chini ya kosa baya sana nchini humo la “usafirishaji haramu wa binadamu.”

Mwanaidi Maajar ananukuliwa akieleza wasiwasi wa kuharibika uhusiano kati ya nchi hizi mbili wakati akiwasiliana na Sanze Salula, katibu mkuu wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.

Barua ya Balozi Maajar kwa Salula, yenye Kumb. Na. WEPC.179/53 ya tarehe 4 Februari 2011 ilinakiliwa pia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo na katibu wa rais, Prosper Mbena.

Anasema, “…narudia ushauri wangu wa awali kwa serikali kuangalia namna ya kumkopesha Dk. Mzengi fedha zote anazodaiwa ili aweze kulipa deni lake kwa mkupuo mmoja kuepuka dhahama ya kuharibu uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Marekani,” inasema barua ya Balozi Maajar.

Inasema, “Ingawa kwa sasa serikali ya Marekani imeonyesha kuridhika kutokana na mawakili wa Bi. Zipora kupunguza deni na Dk. Mzengi kukubali kuanza kulipa kwa awamu, suala hili litabaki kuwa tete kutokana na hatua ya mawakili wa Bi. Zipora kupinga utaratibu wa kulipa.”

Balozi Maajar anasema, “Mawakili hao wameanza tena kampeni za kuichafua Tanzania katika Congress, pamoja na kuishinikiza tena serikali ya Marekani ili nayo iishinikize serikali yetu kulipwa deni hilo…”

Anasema, “Kuchelewa kulipa kutapelekea mawakili wa Bi. Zipora Mazengo kurejea tena kampeni yao ya kuichafua Tanzania. Kampeni zao zinavuruga juhudi zetu kujaribu kujenga mahusiano ya karibu na Congress.”

Akiandika kwa njia ya tahadhari, Balozi Maajar anaeleza, “Sheria ya kupambana na usafirishaji haramu wa watu ya hapa Marekani ina kipengele kinachoipa mamlaka Congress kuiamuru serikali kusimamisha misaada kwa nchi ambayo imethibitika kuvunja sheria hiyo.”

Andishi la Balozi Maajar linafika mbali zaidi. Linasema, “…sheria hiyo huichukulia serikali kuwa mkosaji pale ofisa wa serikali anapopatikana na hatia, kwa maana kwamba haitofautishi kosa la mtu binafsi na kosa la serikali…”

Kuhusu umuhimu wa kulipa fedha hizo sasa, Balozi Maajar anashauri, “…kwa maoni yangu, baada ya mawakili wa Bi. Zipora kukubali malipo kidogo sana licha ya hukumu ya mahakama kumpa zaidi ya dola milioni moja, halitakuwa jambo la busara kuacha kiasi hiki kidogo kiathiri uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Marekani na zaidi kuweza kuathiri misaada mikubwa kama ile ya MCC Compact,” anaeleza.

Gazeti hili lilipowasiliana na Dk. Mzengi, saa 11.35 jioni, Jumapili iliyopita, kutaka kufahamu iwapo ameweza kumaliza tatizo linalomkabili ambalo laweza kuingiza nchi katika mgogoro wa kidiplomasia, alijibu haraka, “Hilo liko kwenye process” – mchakato.  

Alipotakiwa kueleza kwa undani hicho anachoita “mchakato” kimefikia hatua gani, Dk. Mzengi alikata simu. Alipopigiwa dakika tatu baadaye, simu yake iliita bila kupokewa. Gazeti liliendelea kumtafuta tena na tena, lakini halikufanikiwa kumpata.

Naye waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alipoulizwa juu ya jambo hilo alisema, “Jambo hili tunalifahamu. Linashughulikiwa na serikali. Ni jambo la mtu binafsi.”

Alisema, “Tayari tumejadiliana na Dk. Mzengi na ameanza kulipa deni lake.” Kuhusu tishio la kukatiwa misaada na serikali ya Marekani, Membe alisema, “Hilo haliwezekani. Serikali ya Marekani inajua kuwa hili ni jambo la mtu binafsi…”

MwanaHALISI halikuweza kumpata Balozi Maajar kuzungumzia suala hili.

Awali Balozi Maajar akiandika kwa Salula, alieleza kwa urefu hatua lilizopitia sakata hilo ikiwa ni pamoja na kikao kati ya wanasheria wa Bi. Zipora na Balozi Maajar kilichofanyika tarehe 1 Novemba 2010 katika ofisi za ubalozi wa Tanzania, Washington D.C.

Katika kikao hicho, wanasheria wa Bi. Zipora walichukizwa na hatua ya serikali ya Tanzania ya kumbeba Dk. Mzengi na kuahidi kufanya kazi usiku na mchana kuichafua Tanzania nchini Marekani.

Walisema mteja wao aliathirika kutokana na hatua ya Dk. Mzengi na mkewe kumfanyisha kazi kama mtumwa na bila malipo, ikiwamo kupika chakula cha biashara (mamantilie), kazi ambayo ilikuwa inafanywa na mke wa Dk. Mzengi.

Mawakili wa Bi. Zipora waliohudhuria mkutano huo, ni Martina E. Vandenberg, Lorelie S. Masters na Daniel I. Weiner. Martina na Master ni washirika katika kampuni yao ya Jenner & Block, wakati Daniel ni wakili wa kawaida wa kampuni hiyo.

Katika nyaraka za awali ambazo Balozi Maajar aliwasilisha serikalini, inaonyeshwa alishauri serikali kutolipa fedha hizo kwa maelezo ni kinyume cha taratibu za matumizi ya fedha za umma; badala yake akataka fedha hizo zilipwe na Dk. Mzengi mwenyewe.

Msimamo huo wa serikali aliuweka wazi katika mazungumzo yake na mawakili wa Bi. Zipora, tarehe 1 Novemba 2010. Imefahamika sheria za Tanzania haziwezi kuitambua hukumu hiyo bila kwanza kusajiliwa mahakama kuu.

“Kufanya hivyo kutapelekea kuwepo hoja za wakaguzi wa hesabu za serikali kutoka kwa mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG) na pia hoja za Kamati ya Bunge inayosimamia hesabu za serikali ambayo mwenyekiti wake huwa ni mbunge toka chama cha upinzani,” ananukuliwa Balozi Maajar akieleza mawakili wa Bi. Zipora.

Katika maelezo yao kwa Balozi Maajar, wanasheria wa Bi. Zipora walisema hawako tayari kuja nchini au kuajiri wanasheria ili kuwezesha hukumu iliyopo kutekelezwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Walisema kuwa gharama za kufanya hivyo ni kubwa na hawako tayari kuingia katika gharama nyingine, kwani tayari wametumia zaidi ya dola za Marekani 330,000 kwa ajili ya kugharamia kesi hiyo.

Lakini si hivyo tu, “Wanasheria walisema pia kuwa hawana imani na mahakama za Tanzania kwa vile zimejaa rushwa,” inaeleza barua ya Balozi Maajar aliyotuma nchini.

Anasema wanasheria hao waliomba serikali kumwadhibu Dk. Mzengi kwa kumfukuza kazi na wanataka serikali iwe na sheria ambayo kwao Dk. Mzengi anaweza kushitakiwa. Wanasheria hao walilalamika kuwa badala ya serikali kumwadhibu, ilimpandisha cheo na kupangiwa kazi katika ofisi ya rais ikulu.

Akijibu hoja hizo, Balozi Maajar alieleza kuwa serikali inaheshimu hukumu iliyopo dhidi ya Dk. Mzengi. Hata hivyo, ili hukumu hiyo iweze kutekelezwa nchini; na ili serikali iweze kusaidia utekelezaji wake, ni lazima utaratibu wa kisheria uliopo kuhusu hukumu za nje ufuatwe kikamilifu. 

Kuhusu Dk. Mzengi kupandishwa cheo, Balozi Maajar alikanusha madai hayo. Alisema kwa anavyojua yeye, Dk. Mzengi hafanyi kazi katika ofisi binafsi ya rais kama wanasheria hao wanavyodai.

MwanaHALISI limeelezwa kwa sasa, Dk. Mzengi anafanya kazi idara ya usalama wa taifa akiwa miongoni mwa wasaidizi wa karibu wa mkuu wa idara hiyo, Rashid Othmani.

Mkutano wa 1 Novemba 2010 kati ya wanasheria hao na balozi ulihitimisha hoja zao kwa kueleza yafuatayo:

Kwanza, Dk. Mzengi aendelee kuwekewa shinikizo ili atoe utaratibu wa jinsi atakavyolipa pesa hizo anazodaiwa hususan mishahara ambayo haikulipwa.

Pili, waliahidi kuacha kampeni chafu dhidi ya serikali kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo ili kutoa nafasi kwa serikali kulishughulikia suala hili. Walitaka kupata ahadi kutoka kwa Balozi ni lini suala hili litamalizika.

Tatu, walitaka kupata majibu ya hatua zilizochukuliwa kidiplomasia kutoka serikali ya Tanzania. Walisisitiza kuwa hawataacha kufuatilia suala hili hadi ufumbuzi wake upatikane.

Mawakili wa Bi. Zipora waliahidi kuendelea kuwasiliana na Bunge la Marekani na Wizara ya Mambo ya Nje hadi hapo suala hilo litakapomalizika.

Nne, walitaka kujua hatua za kuchukuliwa iwapo Dk. Mzengi atakubali kuanza kulipa na baadaye kuacha kulipa.

Tano, walitaka kujua mchakato wa maombi ya pasi ya kusafiria ya Bi. Zipora yaliyowasilishwa ubalozini uko hatua gani.

Sita, walisema kuwa wizara ya usalama wa ndani ya Marekani imemtambua na kumthibitisha Bi. Zipora Mazengo kuwa mwathirika wa “biashara haramu ya usafirishaji binadamu” na imempa visa ambayo inamwezesha kuishi na kufanya kazi Marekani wakati wote wa uhai wake.

0
Your rating: None Average: 3 (3 votes)