Tayari uchaguzi mkuu umevurugwa


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 26 May 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Uchambuzi
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) Jaji Lewis Makame

UCHAGUZI mkuu wa Okoba mwaka huu, tayari umevurugwa. Serikali inahusika. Maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ambao walijiandikisha kupiga kura, watashindwa kufanya hivyo.

Wakati wanafunzi wengi walijiandikisha katika vituo vilivyoko vyuoni na walitarajiwa kupiga kura kwenye vituo hivyo, sasa uchaguzi utafanyika wakati hawajarejea vyuoni.

Hii ni kutokana na serikali kusogeza mbele tarehe za kuanza muhula mpya kwa vyuo vikuu nchini.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe amekaririwa akisema kuwa vyuo vitafunguliwa baada ya uchaguzi mkuu.

Kawaida muhula huanza 25 Oktoba na kwa tarehe hizo, wanafunzi walikuwa wamejiandaa kushiriki uchaguzi pale walipojiandikisha. Uchaguzi mkuu unafanyika 31 Oktoba.

Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, vyuo vitafunguliwa siku nne au tano baada ya uchaguzi mkuu. Hii ni sawa na siku 11 tangu tarehe ya kawaida ya kufungua vyuo.

Sababu ambazo Maghembe anatoa kuhalalisha kusogezwa mbele siku ya kuanza muhula, ni nyepesi mno. Haziwezi kuzima madai ya baadhi ya wanafunzi kuwa serikali imenuia kuwapora haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Kwa mfano, Maghembe amemwambia mwandishi wa gazeti hili kuwa serikali haijakamilisha maandalizi ya malipo ya wanafunzi na hivyo hakuna sababu ya kuwaita vyuoni mapema.

Amehamisha hoja na kuingiza maelezo kwamba kuanzia sasa malipo kwa wanafunzi hayatakuwa yanatoka kwenye bajeti ya serikali, bali kwenye “taasisi za fedha.”

Hapa ndipo tunakumbana na maswali mengi. Kwanza, je, siku tisa zinatosha kwa serikali kukamilisha taratibu za fedha kwa wanavyuo? Je, serikali haina kalenda ya shughuli zake? Haikufahamu kuwa kuna uchaguzi?

Tuulize zaidi. Je, si serikali hiihii inayohubiri haki ya kila mwananchi kujiandikisha na kupigakura? Je, kama haijamaliza taratibu zake, inatekeleza vipi wajibu wake wa kulinda haki ya raia ya kupiga kura?

Labda hapa, John Tendwa, yule msajili wa vyama vya siasa na mzoefu wa udandiaji, anaweza kusema suala la haki ya wananchi kuchagua viongozi “ni utani” na kwamba wananchi wanapaswa kuanza kuzoea utani huo!

Je, inawezekana waziri hajui kuwa idadi ya wanafunzi vyuoni ni maelfu? Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliliambia bunge mwaka jana kuwa vyuo vikuu (wakati huo) nchini vilikuwa na zaidi ya wanafunzi 80,000.

Takwimu hizi, ingawa ni za mwaka jana, zinaonyesha ukubwa wa tatizo. Hali yaweza kuwa vivyo hivyo katika vyuo vingine vipatavyo 26 nchini.

Pili, kuna uhusiano gani kati ya fedha za kulipa wanafunzi kutoka kwenye bajeti au taasisi za fedha na wanafunzi kuporwa haki ya kuchagua viongozi wao?

Je, hakuna mawasiliano kati na baina ya ofisi na wizara za serikali? Iweje Tume ya Uchaguzi (NEC) ipange siku ya uchaguzi ambayo watu wake wengi na wenye kura ya kundi wakiwa hawawezi kupiga kura?

Tuseme labda hili la kubadili tarehe za kuanza muhula halikutarajiwa; hivyo halikuwekwa kwenye mipango. Je, ilipotokea hivyo, wizara ya Maghembe imechukua hatua gani kuhakikisha wanafunzi wapigakura wanabaki na haki yao?

Kana kwamba Maghembe alihisi ataulizwa iwapo tarehe ya kuanza muhula itaingilia haki ya wanafunzi vyuoni kupiga kura, alisema “Sisi tunaendesha elimu. Hatuendeshi siasa.”

Inawezekana profesa akatoa majibu tofauti iwapo ataulizwa kesho juu ya suala hilihili. Kwani waziri ni mwanasiasa. Uteuzi wake ni wa kisiasa. Shughuli zake ni za kisiasa; na Mfuko wa kinachoitwa “mikopo” kwa mwanafunzi umefanywa kuwa wa kisiasa.

Si hivyo tu. Mfuko wenyewe umekuwa sehemu ya siasa. Hata wanaousimamia wameshindwa kueleza iwapo fedha zinazotolewa ni kwa ajili ya “uchangiaji” au ni “mikopo” kwa wanafunzi.

Wameshindwa kueleza na labda kuelewa, kuwa kama fedha hizo ni “mkopo,” kwa nini kila mmoja asipewe sawa au kwa mujibu wa mahitaji yaliyofafanuliwa. Ni siasa tupu!

Hapa, bila shaka profesa alipigwa na mghafala. Bila shaka ni mazoea ya kubeza siasa ambazo yeye sasa ni sehemu yake na anaendelea kujichimbia.

Vyovyote iwavyo, uwezekano wa wanafunzi katika vyuo vikuu kupiga kura katika uchaguzi mkuu mwaka huu, ni mdogo.

Hali hii inaweza kubadilishwa iwapo NEC itatoa amri kwa wasimamizi wa uchaguzi kote nchini, kupokea na kukubali wanafunzi wa vyuo vikuu kupiga kura popote walipo.

Hili laweza kufanywa kwa kuamuru wasimamizi kuhakikisha kuwa wanafunzi wana vitambulisho vya uanafunzi na hati za kupigia kura. Hivi viwili vikiwepo mtu apate uhalali wa kupiga kura pale alipo.

Bali hilo litakuwa limerahisisha upigaji kura kwa upande wa rais peke yake. Kwani uchaguzi wa mbunge na diwani ni wa masafa mafupi.

Siyo vigumu kuona hilo. Wakati uchaguzi wa rais unaokota mtu mmoja kwa taifa zima, uchaguzi wa mbunge na diwani unalenga kuleta mabadiliko ya pale ulipo kutegemea uwakilishi unaotaka barazani kwako.

Hivyo kukubaliwa kwa utaratibu wa kupiga kura kwa masafa marefu – kutoka wanafunzi walipo – kwa kutumia vitambulisho vya vyuo na hati za kupigia kura, hakutawezesha mpigakura kuondoa au kusimika anayeona anafaa katika mazingira ya pale anapoishi.

Ndiyo maana yameanza kuibuka madai, na bado hayajathibitika, kuwa wizara ya elimu yawezekana kuwa imeshirikiana na wagombea wa karibu (wa ubunge na udiwani), kuhakikisha kuwa umati wa wapigakura unawekwa kando ili wagombea waweze kupita.

Ni kazi chafu isiyostahili kuhusishwa na mwadilifu na hata kiongozi wa serikali. Lakini ipo na karibu upepo wake utaanza kuvuma kwa nguvu.

Ukweli ni kwamba wanafunzi wa vyuo vikuu hawatapata fedha za kulipa nauli kutoka makwao kwenda wanakosomea ili waweze kupiga kura na kurudi makwao tayari kwa maandalizi ya kuitwa na wizara kwa muhula mpya.

Hawana uwezo pia wa kwenda mijini viliko vyuo vyao na kujigharamia kwa muda wote wakisubiri kupiga kura. Ama upatikane utaratibu mpya wa kuwawezesha kama ilivyofafanuliwa hapo juu au haki yao hiyo itakuwa imeporwa.

Umati wa wanafunzi watakaokosa fursa ya kupiga kura; ukiunganishwa na umati ambao haukuwezekana kuandikishwa kutokana na taratibu mbovu na visingizio lukuki; uchaguzi hautakuwa huru na wa haki.

Kwenye uchafu huu, ukiongeza njama za wizi zinazoendelea – za wawakilishi wa Chana Cha Mapinduzi (CCM), kupita wakiandika majina na hati za wapiga kura na simu zao – kwa madai kuwa rais atawapigia kura (kama inavyofanyika Iringa mjini), tayari uchaguzi mkuu mwaka huu umevurugwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu:

Ninatamani Waziri Jumanne Maghembe awe amesoma makala hii. Utetezi aliotoa unamfaa nani? Na kwa majibu yake mepesi kwa maswali magumu yanayohitaji majibu makini, labda tumwambie Waziri tu kuwa hawezi kuwadanganya watu wote wakati wote.