TEMCO washupalia serikali


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Ndani ya Jamii

“KAMA serikali inatenga kiasi cha Sh. 60 bilioni kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya kuendesha uchaguzi, inatakiwa ifanye hivyo kwa kutenga angalau shilingi bilioni moja kwa ajili ya uangalizi.”

Ni maneno ya Dk. Benson Bana, Mratibu wa Kamati ya Kuangalia Mwenendo wa Uchaguzi Tanzania (TEMCO) inayoundwa na asasi za kiraia (AZAKI) zipatazo 152.

Dk. Bana anaibana serikali ya Tanzania ichukue jukumu muhimu la kuwawezesha wanaharakati wanaosimamia uchaguzi chini ya mwamvuli wa Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET), unaoendeshwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

TEMCO inahitaji fedha kwa ajili ya kufanikisha mipango ya kupeleka watazamaji nchi nzima wa kuangalia hatua mbalimbali za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Wakati Watanzania walioko Bara watapiga kura kuchagua rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani wao katika uchaguzi unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Zanzibar watapiga kura kuchagua rais wa Zanzibar, wajumbe wa baraza la wawakilishi na madiwani wao chini ya usimamizi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Upigaji kura zote utakuwa 31 Oktoba.

Dk. Bana anasema waangalizi ambao hutokana na asasi za kidini, chama cha walimu, waandishi wa habari na wanataaluma wengine, wana mchango mkubwa katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira yanayokubalika chini ya misingi ya demokrasia na utawala bora.

Akizungumza katika mkutano maalum wa wadau wa masuala ya uchaguzi waliokutana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivi karibuni, Dk. Bana alisema serikali lazima itenge fedha kwa ajili ya kuwezesha waangalizi 7,000 kwenda na kuangalia uchaguzi nchi nzima kwa kipindi kifupi. Waangalizi 210 watatumika kwa muda mrefu.

“Kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki ndio nguzo kubwa ya kidemokrasia hivyo zoezi hili litajielekeza kwenye kutathmini uwazi na uadilifu wa zoezi zima kwa ujumla,” anasema.

Makamu Mwenyekiti wa TEMCO, Mariam Abubakari, anasema mwaka huu waangalizi wa TEMCO wataelekeza zaidi jicho katika masuala ya kisheria, ufanisi wa vyombo vinavyosimamia uchaguzi na utekelezaji wa sheria mpya ya gharama ya uchaguzi.

“Kama mnavyofahamu, TEMCO imekuwa ikiangalia mwenendo wa uchaguzi mbalimbali uliofanyika nchini tangu mwaka 1995. Mwaka huu kuna sheria mpya ya gharama za uchaguzi ambayo tutaipa umuhimu inaostahili,” anasema.

Mariam,mwanaharakati kutoka Zanzibar, anasema tayari TEMCO ilishatuma waangalizi wake wakati wa uandikishaji wapiga kura kwa upande wa Zanzibar kuanzia Oktoba 2009 hadi Juni mwaka huu.

“Zaidi ya hapo, mwezi Julai 2010 TEMCO ilipeleka wataalamu wake kuhudhuria mikutano mikuu maalumu ya vyama vya siasa kwa lengo la kuangalia uteuzi wa wagombea urais na wagombea wenza,” anasema.

Kwa mwezi uliopita, TEMCO ilipeleka waangalizi 62 wa ndani katika majimbo yaliyoteuliwa kama mfano, ili kuangalia hatua za uteuzi wa wagombea wa vyama katika nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani.

Mwaka huu, kwa mujibu wa Mariam, TEMCO itakuwa na mwangalizi karibu katika majimbo yote ya uchaguzi Bara na Zanzibar. Kutakuwa na waangalizi katika vituo 6,650 Tanzania Bara na vituo 700 kwa Zanzibar.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa Tanzania Bara pekee ina vituo 55,000 vya kupigia kura inayoonyesha kuwa TEMCO itaweka waangalizi wake kwa asilimia 12 tu ya vituo vyote.

Hiyo ndiyo changamoto kubwa inayoikabili TEMCO kwani wanahitajika kuziba pengo la kutuma waangalizi la asilimia 88 ili kuvifikia vituo vyote.

Dk. Bana anasema kama wataweka msimamizi mmoja katika kila kituo kwa vituo vyote hivyo na kumlipa kila mmoja kiasi cha shilingi 5,000 tu kwa siku, zitahitajika Sh. 275 milioni kwa siku hiyo moja pekee. “Ni gharama kubwa na ndio maana tunasema serikali ina jukumu la kutusaidia kufanikisha mipango hii,” anasema.

Kwa sasa, Dk. Bana anasema wameamua kuangalia zaidi maeneo ya majimbo ambayo yanajulikana kwa kuwa na ushindani mkubwa wa vyama vilivyoweka wagombea. Hapo ndipo wataweka waangalizi wachache wanaoweza kuwahudumia kwa muda wote.

“Katika miaka yetu hii 15 ya uangalizi, tumepata uzoefu wa kutosha kubaini maeneo yenye ushindani wa kisiasa miongoni mwa vyama. Haya ndiyo tumeyapa kipaumbele kwa waangalizi tulionao. Tutajitahidi kuzingatia uwiano mzuri,” anasema.

Baadhi ya majimbo hayo ameyataja kuwa ni Tarime, Karatu, Ubungo, Moshi Mjini na Arusha.

Dk. Bana anasema shughuli za TEMCO kwa uchaguzi huu zimesaidiwa na wafadhili mbalimbali; wakiwemo Tume ya Nchi za Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) pamoja na nchi za Canada, Norway, Sweden, Denmark, Uholanzi na Finland.

Anasema bila ya wafadhili hao, ingekuwa vigumu kwa TEMCO kufanya kazi muhimu ya uangalizi katika uchaguzi kwa kiwango hicho.

“Uchaguzi huru na wa haki ni kitu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Kama tunataka kupiga hatua katika maendeleo ya demokrasia na utawala bora, ni muhimu tuwe na uchaguzi unaokidhi vigezo vya kuitwa ni uchaguzi huru, wa haki na ulioendeshwa katika misingi ya uwazi na uadilifu,” anasema.

Washiriki mbalimbali wa mkutano huo walieleza kusikitishwa kwao na namna serikali katika nchi nyingi za Afrika zinavyokuwa ngumu kutenga fedha kwa ajili ya vikundi vya waangalizi wakati wa uchaguzi.

“Ni lazima serikali zetu, ikiwamo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ziamue sasa kuwekeza kwelikweli katika eneo hili la usimamizi na ufuatiliaji wa uchaguzi kwani si vizuri kuendelea kutegemea wafadhili watufanyie kila kitu,” anasema mmoja wa washiriki wa mkutano wa TEMCO.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: