Tendwa amejitakia mwenyewe aibu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version

JINA la John Tendwa, msajili wa vyama vya siasa nchini, limegonga tena vichwa vya habari. Jina hili huwa linajitokeza kwa nadra. Ila linapojitokeza, huwa ni kwa masuala yenye utata.

Mara ya mwisho Tendwa alisikika akiwakingia kifua wabunge wawili waliofukuzwa uanachama kwenye vyama vyao – David Kafulila wa NCCR-Mageuzi na Hamad Rashid Mohamed wa CUF.

Huku akijua kuwa serikali, chini ya katiba na sheria ya vyama vya siasa anayoisimamia yeye, hairuhusu mgombea binafsi wala mbunge kufukuzwa uanchama na akabaki na ubunge, yeye alibeza maamuzi ya vyama hivyo akisema yanaviza demokrasia na kuitia serikali katika gharama za kuandaa uchaguzi mdogo.

Wiki iliyopita jina hili liliibuka tena akiwa mkoani Arusha ambako moja ya majimbo yake, Arumeru Mashariki, kunafanyika uchaguzi mdogo wa ubunge Aprili mosi kuziba nafasi ya marehemu Jeremiah Sumari.

Wakati wadau wa uchaguzi huo wanaanza maandalizi, Tendwa naye hakubaki nyuma, akaanza harakati. Kiguu na njia hadi jimboni kwa kazi anazozijua mwenyewe, bila shaka na kuhalalisha posho. Baada ya ziara, kama kawaida yake, akahitimisha kwa kauli yenye utata.

Akawaambia waandishi kuwa wazee wa kimila wa Meru, wajulikanao kama Washiri, wamemuuma sikio kuwa hawataki kumwona Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema katika kipindi cha kampeni ya uchaguzi huo.

Lema anatoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

“Lema alileta dharau kubwa na utovu wa nidhamu siku ya maziko ya Sumari hatua ambayo iliwakera Washiri,” Tendwa alikaririwa na waandishi wa habari.

Akashauri kama alivyonukuliwa na gazeti moja, “ni busara tu, Lema kwenda kuwaomba radhi wazee hao kama anataka kufanya kampeni ya mgombea wa chama chake.”

Gazeti jingine likamnukuu akisema wazee hao walikwenda mbali zaidi, watamuua mbunge huyo ikiwa atakwenda kukampeni Arumeru Mashariki.

Hata kabla wazee hao kukanusha madai ya Tendwa, kauli yake ilionekana wazi kuwa tata na ambayo ilikuwa na malengo ya kisiasa – kusaidia chama tawala. Ina kila dalili za kuchochea vurugu na kumwaga damu.

Kauli hiyo inataka kuibua hasira na chuki za wazee wa Meru kwa mambo ya uzushi. Bali Tendwa anajua anachokifanya na anajua matokeo ya kauli yake endapo itachukukuliwa kwa uzito na kufanyiwa kazi na wazee hao au vijana wao.

Anafahamu kuwa wanaweza kutokea watu, wakamsikiliza na kujaribu kumzuia Lema ambaye anaungwa mkono na vijana. “Amri” ya Tendwa inaweza kuzua tafrani kwani wafuasi wake wasingekubali mbunge wao kuzuiwa.

Mungu bariki, ilikuwa ni uzushi. Na Lema amekwenda Arumeru na hakuna kilichotokea. Hata Kamanda wa Polisi Mkoa, Thobias Andengenye amezungumzia kauli hiyo, akisema hakutakuwa na tatizo kwa Lema kwenda kukampeni na ulinzi utaimarishwa kuhakikisha hakuna atakayemdhuru.

Cha ajabu, Tendwa anatoa uzushi wake huo bila kuweka wazi kauli yoyote au kitendo chochote alichofanya Lema, cha kutosha kuchukuliwa kama maudhi kwa wazee wa kimila wa Meru.

Haelezi hatua yoyote waliyochukua wazee wale baada ya “kusikia au kushuhudia” maudhi ya Lema. Badala yake, wazee hao, eti walikaa kimya na kusubiri kipindi cha kampeni ili wamzuie, kana kwamba walishajua kuwa lazima mbunge huyo atakuwa miongoni mwa wanaounda timu ya kampeni ya CHADEMA.

Msajili wa Vyama ambaye makao yake kikazi yapo Dar es Salaam, haelezi alikwenda Arumeru kufanya nini, hasa kipindi hiki ambapo vyama vya siasa anavyodai kuwa yeye ni mlezi wake, havijaanza kampeni rasmi.

Haelezi jambo gani lilimtuma kwenda kuzungumza na Washiri siku chache kabla ya kampeni kuanza. Hajabainisha kwa nini wazee hao waliamua kutoa “kilio dhidi ya Lema” kwake badala ya chama cha mbunge huyo au mbunge mwenyewe. Ndio maana wengi waliosikia kauli yake wamebaini kitu nyuma ya pazia.

Hata wazee wenyewe wa kimila waliolishwa maneno wamempinga Tendwa. Wamejitokeza kweupe kukanusha madai ya kutishia kumuua Lema akienda jimboni Arumeru Mashariki kumkampenia mgombea wa CHADEMA.

Katibu wa Washiri wa Meru, Jacob Kaaya amekaririwa na gazeti moja akisema kuwa madai ya Tendwa hayana ukweli.

Kaaya anasema mpaka sasa hakuna kikao cha kimila cha kabila hilo kilichokaa kujadili suala hilo, na wao kama wazee wa mila hawajawahi kukutana na Tendwa na kutoa kauli ya pamoja kuhusu madai ya kumuua Lema.

Akaongeza kuwa wazee wasingeweza kutoa madai mazito kama hayo na kwamba huenda Tendwa alikutana na mtu mmoja akamweleza hilo, na kauli ya mtu mmoja asiyekuwa kiongozi aliyeagizwa kusemea wazee, haiwezi kuchukuliwa ni kauli rasmi.

Kaaya anasema shughuli za wazee wa mila ni kulinda amani, usalama na maliasili, hasa ardhi. Jukumu jingine ni kuhakikisha wajane na yatima wanapata haki zao. Amesema kamwe hawahusiki na shughuli za kisiasa.

Kauli ya Tendwa imeibua hisia za watu. Jambo hilo limejadiliwa kwenye mitandao ya kijamii. Mohamed Mtoi anaandika kwenye Mtandao wa Mabadiliko, “Tendwa amejitenda mwenyewe… anavuna aibu kwa kushabikia siasa za maji taka. Amedhihirisha kuwa ni miongoni mwa wapiga zumari wa CCM.”

Mtoi anapendekeza Tendwa akamatwe na vyombo vya dola kwa kauli ya uchochezi, ambayo, amesema, inaweza kusababisha umwagaji wa damu.

Aibu aliyovuna Tendwa kwa uzushi wake ameitaka mwenyewe. Mshale alioulenga umjeruhi Lema na CHADEMA yake, umepinda kona na kumfuata mwenyewe. Umemrudi.

Ameamsha munkari wa wazee wa Kimeru, na leo Jumatano wanalazimika kukutana eneo la Poli, chini ya Mrigariga, ili pamoja na mambo mengine, wajadili kwa kina suala hilo.

Kwa upande wao, CHADEMA wamekuja juu kupinga propaganda za Tendwa. Lema amesema: “Tendwa anafanya propaganda chafu. Anaingilia kazi zisizo zake, kwa kutumiwa na CCM.

Katibu wa CHADEMA wa Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, amesema vurugu zinazotajwa kufanywa na Lema hazimhusu, bali zilianzishwa na vijana wa CCM baada ya kumwona Lema akipita kwenye msiba ambapo walilipuka kwa “shangwe na hamaki”.

Golugwa amesema hata wao walisikitika kwa kitendo hicho na walikutana na viongozi wa CCM kuyaweka sawa, lakini walipoona yamejirudia kwa sura ya Washiri, wamesikitishwa sana.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa anamtuhumu Tendwa kwa kujiingiza kwenye kampeni kuisaidia CCM.

Anasema, "anafanya siasa, sasa anazunguka Arumeru Mashariki anatafuta nini. Kwanini asikae ofisini kwake na kutoa mwongozo kwa vyama vya siasa? Analofanya halikubaliki," anasema Dk. Slaa.

Kwa vyovyote vile, kauli hii kwa kuwa imethibitisha haikuwa na usahihi, imemshusha Tendwa, mtendaji anayetarajiwa kutoa kauli zinazoeleweka na zisizochochea chuki katika jamii.

Lakini, kwa sababu alijua wazi alichokuwa akikifanya na kutarajiwa kuwa kwa nafasi yake angejua athari zake, inatosha tu kusema, “amevuna aibu na amejitakia mwenyewe.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: