TFF imeiabisha kamati ya uchaguzi Yanga SC

MTU anayefuatilia mfululizo wa matukio katika klabu ya Yanga kuanzia ulipofanyika mkutano mkuu wa wanachama Juni 6, 2010 atagundua kujiingiza kupita kiasi kwa kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo.
Ilipoteuliwa kamati hiyo kusimamia uchaguzi, ambao awali ulipangwa kufanyika Julai 4, 2010, ilidhani ya kuwa imepewa ‘rungu’ la kuongoza. Mjumbe mmoja akashinikiza baada ya mkutano kufungwa, uongozi wa mwenyekiti Imani Madega ukae kando, halafu kamati ikatangaza uchaguzi mkuu kufanyika Juni 27 kabla ya kusogeza mbele hadi Julai 18.
Mtu angegundua walakini mwingine wakati wa usaili wa wagombea. Bila sababu za msingi na hata kupuuza ombi la ruhusa kwa baadhi ya wagombea, kamati ikakata majina wasigombee.
Leo hii, baada ya wagombea hao kukata rufaa kwenye kamati ya uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Francis Mponjoli Kifukwe na Ahmed Falcon wameiumbua Kamati ya Uchaguzi ya Yanga.
Kamati ya uchaguzi ya TFF chini ya Deogratius Lyatuu, imetengua uamuzi wa kamati ya uchaguzi wa Yanga chini ya Jaji John Mkwawa na kuwarejesha Kifukwe na Falcon katika kinyang’anyiro cha uenyekiti katika uchaguzi huo.
Pamoja na sababu nyingine, Kifukwe ambaye aliwahi kuongoza klabu hiyo ya Jangwani, jina lake liliondolewa kwenye orodha ya kuwania uongozi kwa sababu ya kutohudhuria kikao cha usaili kilichoketi mwishoni mwa mwezi uliopita.
Sababu nyingine ya kuenguliwa Kifukwe iliyotajwa katika barua ya kamati hiyo, inasema kwamba ameshindwa kutoa taarifa za kina juu ya uuzwaji wa gari aina ya Double Coaster lililokuwa na namba za usajili TZR 6200.
Ingawa Jamali Malinzi aliyekuwa katibu mkuu wakati Kifukwe ni rais wa klabu, aliwasilisha maelezo kujibu madai hayo, kamati ilipuuza. Kifukwe, katika utetezi wake mbele ya kamati ya TFF amesema kwamba aliaga kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Yanga, Jaji Mkwawa kwamba angekuwa na safari ya Afrika Kusini.
Taarifa zinasema kwamba jaji huyo ambaye ni Kamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), alikubaliana naye akamruhusu, lakini katika mazingira ya kutatanisha kamati ilitumia kigezo hicho hicho cha kutokuwepo kwenye usaili kumuengua kushiriki kwenye uchaguzi.
Kuhusu gari, Kifukwe alijitetea kwamba uamuzi wa kuuza haukuwa wake binafsi bali ni uongozi mzima, ulioridhia kufanya biashara hiyo kwa sababu mbili ambazo ziko kwenye rufaa yake.
Kwanza basi hilo lilikuwa limetumika kwa muda mrefu hivyo kuchoka kabla ya kuliuza huko Moshi mkoani Kilimanjaro kwa Sh milioni 6.5, fedha ambazo zililipwa kwa Ahmad Kiluvia, mwanachama wa Yanga aliyetoa fedha za kununua hisa katika kampuni wakati ule.
Licha ya Kiluvia kulipwa fedha hizo, pia Kifukwe alitoa mfukoni mwake Sh 3,000,000 ili kuongeza kwenye fedha hizo na kumlipa Kiluvia ambaye alikuwa anadai Sh 9.8 milioni. Kifukwe aliiambia kamati hiyo ya TFF kuwa kuonyesha kwamba hakuwa na nia mbaya kuuza basi hilo, uongozi wake ulinunua basi jingine lenye thamani ya Sh milioni 22.
Lakini Kifukwe alikwenda mbali zaidi katika utetezi wake, akisema kwamba, katika mchakato huo mzima haoni kama ni busara, Kamati ya Uchaguzi Yanga kuwa na mjumbe anayetuhumiwa kuhusishwa na mmoja wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti. Kamati ilifanyia kazi pingamizi la Suleiman Katto.
Mjumbe ambaye Kifukwe alimlalamikia ni Ridhiwani Kikwete, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM). Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, anadaiwa kumbeba wakili mwenzake, Lloyd Nchunga anayewania nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi huo.
Aidha Ridhiwani alilalamikiwa na mwanachama Juma Issa Matandika aliyewasilisha pingamizi juu ya Nchunga akidai mgombea huyo anabebwa na Ridhiwani. Matandika ambaye ni mwanachama kadi Na. 000277, alisema: “Kuna ushahidi kuwa amechukuliwa fomu na ndugu Ridhiwani Kikwete. Hali hii haikubaliki kimaadili na inamnyima Ndugu Lloyd Nchunga moja kwa moja haki ya kuchaguliwa.”
Mbali ya Kifukwe na Falcon ambao waliondolewa kabla ya kurudi waliong’oka moja kwa moja ni Kanali Mstaafu wa JWTZ, Ally Hassan Mwanakatwe kwa nafasi ya uenyekiti wakati kwa upande wa makamu, aliyeondolewa ni Hashim Lundenga.
Wao walipingwa kwa sababu wanadaiwa kushindwa kumshawishi mwenyekiti anayemaliza muda wake, Imani Madega kuipeleka timu uwanjani kucheza na Simba mwaka juzi katika mashindano ya Kombe la Kagame.
Falcon aliondolewa kwa kutowasilisha cheti halisi kwenye usaili, lakini kwenye rufaa yake juzi alikwenda na cheti halisi. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imekubaliana na hoja za Kifukwe na Falcon, ikatengua uamuzi wa kuwaengua na kuwarejesha kwenye kinyang’anyiro hicho.
Ikiwa kamati ya uchaguzi wa Yanga haikujua inafanya kosa kuingia hadi jikoni kumtaka Madega akae kando wakati kanuni haziruhusu, ikiwa kamati ilidirika kutaka kuongoza klabu kinyume cha taratibu ni dhahiri kamati inajiweka katika mazingira magumu ya kuaminika.
Kwa mantiki hiyo, wanaowania nafasi ya mwenyekiti watakuwa Kifukwe, Falcon, Mbaraka Igangula, Lloyd Nchunga na Edgar Chibula.