TFF wasaka kocha kutoka mbinguni

UTEUZI wa Marcio Maximo kama kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, ulilalamikiwa na wadau wengi wa soka kutokana na mchakato wake kuwa wa siri.
Katikati ya mchakato wa kumpata kocha huyo kutoka miongoni mwa makocha watatu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ‘alimshusha’ Maximo kutoka Brazil.
Ilielezwa kwamba Rais alikuwa akihangaika kumpata kocha anayefaa baada ya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulala usingizi.
Aliwashutumu TFF mara mbili; tukio mojawapo likawa wakati wa mapokezi ya Kombe Halisi la Dunia. Majina ya makocha wa TFF yakasambaratika.
Mchakato wa TFF ulijaa usiri mkubwa na sasa mrithi wa Maximo anatafutwa kwa usiri.
Tofauti na TFF, mchakato wa kumpata kocha mkuu wa kuinoa timu ya soka ya taifa ya Ivory Coast maarufu kama Tembo ulikuwa wazi na wadau walijulishwa kila hatua.
Kwanza, Ivory Coast hawakuweka siri kuhusu hatma ya Vahid Halilhodzic aliyeshindwa kuwawezesha Tembo wa Ivory Coast kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika katika fainali zilizofanyika mapema mwaka huu nchini Angola.
Hatua iliyofuata ilikuwa ni ya kumsaka mrithi wake. Majina makubwa ya makocha yalitajwa na shirikisho la Ivory Coast lilipofikia kumtangaza Mswidi Sven-Goran Eriksson, haikuwa miujiza.
Kadhalika, baada ya Amodu Shaibu wa Nigeria kurudi nyumbani mikono mitupu kutoka Angola, Chama cha Soka Nigeria (NFA) kilitangaza wazi kumfuta kazi. Mchakato uliomwezesha Lars Lagerback kutangazwa kuwa mrithi wake haukufanywa kimiujiza pia.
Sivyo kabisa walivyo TFF. Wamerudia ugonjwa uleule wa mwaka 2006 wa kujifungia na majina ya makocha walioomba.
Baada ya kufuatwa mara kwa mara na waandishi wa habari, kwa taabu sana, walitangaza kwamba nafasi ya Maximo itakuwa wazi kuanzia Julai na kwamba yeyote anayetaka kuiwania, anaweza kutuma maombi.
Wiki mbili zilizopita, TFF walisema makocha 59 wakiwemo wa kigeni, waliomba kazi hiyo na kwamba watano miongoni mwao, wamepita.
Lakini TFF waligoma kutaja majina ya makocha hao 59; wazalendo ni kina nani na nani ni wageni na nchi watokazo. TFF pia wakagoma kutaja siku ya mahojiano na makocha hao watano ila walitaja nchi zao.
Hivi kutaja kocha XXX anatoka Serbia au kocha YYY anatoka Denmark inavuruga mchakato? Hata kama TFF wanaogopa kwamba vyombo vya habari vitafanya uchunguzi na kuanika sifa nzuri na mbaya, kuna tatizo gani?
Je, si itakuwa kwa faida ya nchi kwamba haitaangamia kuajiri kocha asiyekuwa na sifa? Hivi, zingefuatiliwa rekodi za Maximo kabla ya kuajiriwa Tanzania, si tungejua udhaifu wake kabla ya kusaini mkataba naye?
Gia kubwa aliyoitumia Maximo kushawishi viongozi wa serikali kwamba anafaa ni kuwahi kuwa kocha msaidizi wa vikosi vya timu za vijana chini ya umri wa miaka 17 na U-20 za kwao Brazil.
Vikosi hivyo, vilikuwa na baadhi ya wachezaji nyota wanaotamba katika soka duniani leo; Ronaldo de Lima na Ronaldinho Gaucho. Ni nani angeacha kumkubali Maximo?
Lakini angechunguzwa hatua kwa hatua alipoanza kusimama kwa miguu yake, tungegundua kumbe Maximo hakuwa chaguo sahihi.
Historia yake inaonyesha kwamba baada ya kuondoka akateuliwa kuwa mkurugenzi wa ufundi wa visiwa vya Grand Cayman kwa miaka mitatu. Inadaiwa alikataa ofa ya kuendelea na kazi hiyo kwa miaka 10 akaenda nchini Scotland kuwa kocha mkuu wa klabu ya Livingston, kuanzia 5 Juni 2003.
Maximo alitia saini mkataba wa mwaka mmoja kama kocha mkuu akiwa kocha wa kwanza kutoka Brazil kuinoa timu ya Uingereza. Hata hivyo, mambo hayakwenda vizuri kwani baada ya matokeo ya mechi tisa; ushindi mara tatu, vipigo vitatu na sare tatu, akajiuzulu 14 Oktoba 2004.
Tarehe 29 Juni, 2006, Maximo akateuliwa kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars kwa mkataba wa miaka mitatu. Mwaka jana aliongezewa mkataba wa mwaka mmoja.
Kazi kubwa aliyopewa ilikuwa ni kuiwezesha Tanzania kucheza fainali za Kombe la Dunia 2010, lakini baada ya kupokea vipigo, Rais Jakaya Kikwete akasema sasa malengo yawe kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Vipigo vya awali vilimaanisha Taifa Stars ilichelewa ndege ya kwenda Ghana kwenye fainali za mwaka 2008, lakini hata pale aliposema anajipanga, Maximo hakuiwezesha timu yetu kuwahi ndege ya Angola kwenye fainali za 2010.
Ndiyo Maximo ni binadamu tena anayefanya kazi sana. Ikumbukwe wanaofanya kazi sana hufanya makosa sana, na wanaofanya kazi kidogo hufanya makosa kidogo na wasiofanya kazi hawafanyi makosa, na wasiofanya makosa hupewa tuzo. Maximo yuko kundi lipi?
Ni dhahiri TFF, hata wakijifungia hawawezi kupata kocha asiyefanya makosa na ambaye hatachunguzwa kabisa na vyombo vya habari. Labda kama kocha huyo anatoka mbinguni.