Timuatimua ya vyama inaua demokrasia


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 25 January 2012

Printer-friendly version

VYAMA vya siasa vilivyopewa dhamana ya kulea demokrasia kwa kudhamini raia kugombea nafasi za uongozi vinazoea kutumia vibaya dhamana hii.

Viongozi wa vyama wameanza kuwa wehu. Wanaonesha dhahiri walivyoanza kulewa madaraka. Wameamua kugeuka walafi na wenye tamaa ya kupindukia mpaka.

Wala hawakumbuki tena wajibu wa kulea vyama vyao, wanachama wao, wananchi wanaovishabikia vyama hivyo. Tuseme, hawataki kulea mageuzi.

Wamejitoa fahamu. Hawajali tena kuwa demokrasia wanayoililia na kuidai kwa serikali iliyopo madarakani kupitia sera za chama kiliochoiunda, inapaswa kuanzia kwenye vyama wanavyoviongoza.

Viongozi wanasahau walikotoka, walikovitoa vyama vyao au vyama hivyo vilikowatoa. Ndio. Wengine wametolewa vumbi la miguu na vyama hivi baada ya mfumo wa siasa za ushindani kurudishwa nchini mwaka 1992.

Wala wao hawakushiriki zile harakati za mageuzi kama walivyofanya kina Kasanga Tumbo, Ndimara Tegambwage na Mashaka Chimoto, kuwataja wachache. Walikuta jamvi limetandikwa na walioanza harakati. Viongozi waasisi wanasahau waasisi wenzao na kuwafyatulia nje.

Visingizio mbalimbali vinatolewa kutimiza matakwa yao. Dalili za matukio ya hivi karibuni zinaonesha wazi matakwa yenyewe taswira yake ni kama mambo ya binafsi tu.

Kama si hivyo, basi ni matokeo ya woga wa viongozi waliopo kwamba wataonekana labda wamechoka na wakati umefika waondoke.

Viongozi wa vyama sasa wanadharau uhuru wa kutoa maoni kuwa unatakiwa ustawi kisawasawa ndani ya vyama. Hawajali hili.

Wakikuta kuna viongozi wenzao wana mawazo tofauti nao wanawakasirika na kuwajengea chuki, siku hizi vijana wanasema ‘bifu.’ Wanaanza kuwasakama. Wanawatungia mashitaka au tuhuma. Wanawaita wasaliti au wanachama wenye nia ya kuvuruga chama. Kumbe ni tofauti tu ya mawazo.

Wakati mwingine, kumbe ni shauri ya kuhojiwa kwa matendo na mienendo yao kiuongozi. Kiongozi mkubwa anapiga yowe kupinga kuchunguzwa kwa tuhuma dhidi yake. Viongozi hawa wnajifananisha na malaika au mitume, ndio waliokuwa hawana makosa maana utendaji wao ulitokana na nguvu na maelekezo ya muumba wao.

Viongozi wakuu wa vyama wanatumia fedha nyingi kufanikisha mkakati wa kufukuza wenzao katika vyama kwa sababu ya tofauti za mawazo au kutuhumu kwa hili au lile.

Miaka ya mapema ya mageuzi haya ya zama za milenia, vitendo vya viongozi kufukuza wenzao katika vyama vilionekana kama rutuba; ndio kukuza demokrasia.

Kumbe sivyo. Sasa ni kukomoana. Haya ni mawazo muflis kidemokrasia. Wapi umesikia inaruhusika mtuhumu kusikiliza kesi ya mtuhumiwa? Au mtuhumiwa akasikiliza kesi ya anayemtuhumu?

Hawa viongozi wa vyama sasa wanasikiliza kesi za waliowatuhumu ukorofi au kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa mujibu wa katiba zao. Wanaongoza vikao vya kesi, wanaita na kuwahoji watuhumiwa, tena mwisho wanaamua kesi. Wanawahukumu wenzao.

Tumeanza kuona hukumu hasi katika ukuzaji wa demokrasia nchini. Kinachoitwa ukorofi wa kiongozi unajibiwa kwa kufukuza kiongozi mwingine. Yamekuwa hayo!

Fikiria hata chama chenye wabunge mkono mmoja tu, kinathubutu kuchukua hatua inayochochea kupunguza idadi ya wabunge ilionao; kinawatimua. Tuseme hakitaki kuwakilishwa bungeni? Haya chama kinao wabunge wengi kiasi fulani, kinatimua wapungue. Hao wabunge wanafukuzwa bila ya viongozi kuhali nguvu za chama zimedhoofishwa. Akili gani hii?

Katika kujadili haya, Mchambuzi mmoja hivi karibuni alisema, “vitendo hivi vya viongozi kufukuza wenzao ni dalili za woga tu. Wanajenga hofu dhidi ya mamlaka yao. Hawataki kusikia wengine wanaona nini kuhusu jambo fulani. Wanazuia mawazo mbadala. Wanataka kusikia kile wanachokipenda tu siyo udhaifu wao.”

Halafu unakuta vyama ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa na viongozi na au wanachama waliowafukuza, lakini ghafla viongozi wake wanabadilika na kuwapachika majina mabaya wanaowatuhumu.

Utasikia “mwache aende zake msaliti mkubwa” au “Hatuna shida naye shushushu huyu aende tu” au “Hajui hatumtaki si amekuwa akitumiwa na wapinzani wetu… akitumiwa na watawala.”

Kwamba kumbe kwa miaka yote hiyo vyama vinafuga mashushushu ndani yake. Vinalea wasaliti. Vinastahamilia wakorofi.

Hivi kweli chama kinaweza kubaki na mkorofi kwa muda mrefu hivyo? Wanamuangalia tu anavyokiangamiza chama na itikadi za chama chao ambacho naye ana mchango wa kukijenga? Ni fikra za kusadikika.

John Tendwa, msajili wa vyama vya siasa nchini, amekuja na rai katika kutafakari mwenendo huu.

Anasema, pale panapotokea mvutano kati ya wanachama na uongozi wa chama chao, inafaa vyama vitafute wasuluhishaji walioko nje ya mfumo wa vyama vyenyewe.

Kwa mfano, Chama cha Wananchi (CUF) kilipokuwa na mvutano kati ya uongozi wa juu na mbunge wa Wawi, Hamad Rashid na viongozi na wanachama wenzake, basi kungetafutwa mtu wa nje ya chama akasimama katikati kupatanisha.

Kwamba kwa kuwa Hamad Rashid na kundi lililoheshimu maoni yake, wametuhumu uongozi wa katibu mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad umedhoofika na kuathiri nguvu za chama, sasa ni busara kuwepo mtu wa nje ya chama akasimama katikati.

Mtu huyu angesikiliza malalamiko ya wanaolalamika na halafu akasikiliza msimamo wa uongozi wanaotuhumiwa. Hapa pangepatikana suluhu. Hata ingekosekana lakini angalau haki ingekuwa imetendeka. Na hii ingekuwa tija kwa demokrasia.

Mfumo kama huo ungetumika kujadili mvutano uliokuwepo kati ya mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, na uongozi wa juu wa chama chake cha NCCR-Mageuzi.

Kafulila, mbunge aliyegombea baada ya kuhama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambako alizusha mtafaruku na viongozi wake, na wenzake walituhumu Mwenyekiti wao, James Mbatia, kwa uongozi uliochoka na kushindwa kukiimarisha chama.

Nani hajui kwamba NCCR-Mageuzi haina nguvu ilizokuwa nazo kisiasa? Chama hiki kilianza ushindani kwa kupata karibu wabunge 30. Leo, kina wabunge watano tu.

Vikao vyote vya kushughulikia tuhuma dhidi ya Hamad Rashid na Kafulila viliandaliwa katika makeke. Labda haki haikutendeka ndio maana wote wamefukuzia mahakamani.

Unapoamini kuwa hukutendewa haki na mfumo uliopo, unajua huenda usiipate kwa kubaki kutarajia mfumo huohuo ukusaidie. Wamekimbilia mahakamani.

Kungekuwa na mtu wa katikati akasikiliza, yawezekana suluhu ingepatikana. Tatizo ni kwamba viongozi waliotuhumiwa hawakutaka suluhu bali kufukuza waliowatuhumu. Huko ni kuitia doa demokrasia.

0
No votes yet