TRA yasutwa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version

MMILIKI wa kampuni ya Tango Transport Ltd., ameendelea kuning’iniza Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa kushikilia kuwa anaidai mabilioni ya shilingi kwa “kuhujumu” biashara yake ya usafirishaji.

Verani Tango, mzaliwa wa Hanang, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa TRA ilikamata magari yake 71 – yakiwemo malori na magari madogo kwa kipindi cha miaka 10.

Baadhi ya magari, amesema mzee huyo wa miaka 67, yameharikiba kiasi cha kutoweza kutengenezeka.

Magari yalikamatwa kwa amri ya TRA ya tarehe 15 Julai 1997 “pasina uhalali wowote wa kisheria”, anaeleza mzee Tango.

Kwa makadirio yake, kwa magari hayo kutofanya kazi kwa miaka kumi, amepoteza biashara ya thamani ya zaidi ya shilingi trilioni moja (au shilingi milioni elfu moja – 1,000,000,000,000).

Wiki iliyopita na wiki hii, TRA imekuwa ikikanusha kukamata magari ya Tango, ikidai kuwa yenyewe huweza “kukamata mali kwa vigezo na hatua zilizo kwenye sheria mbalimbali za kodi.”

TRA imekuwa ikijibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa aliyenukuliwa akituhumu mamlaka hiyo kuingiza serikali katika hasara ya Sh. 800 bilioni.

Dk. Slaa, akiwa mjini Tabora wiki tatu zilizopita, alinukuliwa akisema TRA inamlinda ofisa wake, Placidus Luoga anayedaiwa kukamata magari ya Tango Transport Limited kwa kipindi kirefu, bila sababu za msingi na kusababishia serikali hasara kubwa.

Magari ya kampuni hii yalikamatwa jijni Dar es Salaam, Arusha na Mwanza kwa jumla ya siku 90.

Mzee Tango ambaye hivi sasa ni mgonjwa, anayetoa sauti kwa taabu, alimwambia mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake sebuleni, eneo la Mbezi Beach, kuwa shauri lake lilishafikishwa hata kwa waziri mkuu Mizengo Pinda.

Kulingana na vielelezo ambavyo MwanaHALISI limeona, Waziri Mkuu amewahi kutoa ushauri kwa TRA pamoja na Wizara ya Fedha na Uchumi kumaliza suala hilo kwa kumlipa fidia Tango.

Katika moja ya barua alizoandika waziri mkuu kuhusu suala hilo, Pinda amesema haoni kama ni “…busara kupeleka suala hilo mahakamani.”

Alipendekeza kutumia ushauri utakaotolewa na kikundi kazi ili kumaliza malalamiko hayo ya muda mrefu.

Barua iliyosainiwa na Katibu wake, Ole Kuyan, Kumb. Na. PM/P/2/567/13 ya tarehe 21 Machi 2009, inaonyesha kuwa amerejea barua mbili alizopata kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi na ile ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali zilizokuwa zikizungumzia suala hilo.

Anasema, “baada ya kupitia maelezo ya shauri hili na ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu anaelekeza kwamba serikali imlipe Bw. Verani Tango Sh. 554,464,131.60.”

Malipo hayo ni kati ya Sh. 1,687,500,000 ambazo Tango alikuwa amewasilisha kama madai yake ya fidia ya awali kutokana na magari yake kushikiliwa isivyo halali na TRA kwa siku 90.

MwanaHALISI limefuatilia mgogoro huo na kubaini kuwa ni kweli TRA iliishawahi kutoa amri ya kukamatwa baadhi ya magari ya mfanyabiashara huyo (bila kutaja idadi).

Kampuni ya Tango Transport Ltd., ina makao yake makuu mjini Arusha. Ilisajiliwa kwa anuani ya S.L.P. 220, Arusha.

Mzee Tango anasema baadhi kadi za magari yake zilizochukuliwa na TRA zilipotelea hukohuko na kwamba mamlaka hiyo imekiri kupotea huko.

Msimamo wa Mzee Tango unaonekana kusimama na Dk. Slaa. Katika kauli yake mwenyewe, Tangu anasema, “TRA waache kulumbana na watu wengine; waheshimu makubaliano na kumaliza mgogoro huu na mimi.”

Kampuni ya uwakili ya Nyangarika & Company Advocates ya Mtaa wa Mtendeni, Dodoma iliyomtetea Tango, inatoa mfano tu wa baadhi ya madai yake.

Kuna fidia ya Sh. 1,687,500,000 inayotokana na hasara aliyopata baada ya kushindwa kutekeleza mkataba wake na Kampuni ya Bia tanzania (tanzania bweweries Ltd.).

Kampuni inaeleza kuwa Tango alikuwa akisafirika bidhaa kati ya Dar es Salaam, Mwanza, Eldoret, Arusha na hatimaye Dar es Salaam, kwa malipo ya jumla ya Sh. 15,000,000 kila gari.

Mzee Tango anasema, “…kama magari yake hayakushikiliwa kwa na TRA, kwanini wamekiri kushikilia kadi za magari hayo? Kwanini Luoga mwenyewe amekiri kuamuru magari hayo yakamatwe popote yatakapokutwa?”

Hivi sasa Luoga ni Naibu Kamishna Mkuu wa TRA. Ndiye alisaini, mnamo 15 Julai 1997, waranti ya kukamata magari ya Tango kwa madai ya kudaiwa ushuru wa stempu.

Tango anasema kuwa anataka malipo yake yote na kwamba waliosababisha mgogoro huu ndio wanaopaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

TRA ilikamata magari ya Tango kupitia kampuni ya udalali ya Majembe Auction Mart yenye makao makuu mjini Iringa.

0
No votes yet