TRL sasa basi


editor's picture

Na editor - Imechapwa 08 September 2009

Printer-friendly versionSend to friend
Maoni ya Mhariri

KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL) imeshindwa kazi. Haina tena uwezo wa kutoa huduma wala kulipa mishahara watumishi wake.

Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa anakiri jambo hilo. Anasema, menejementi ya TRL haina uwezo wa kuendesha shirika na kibaya zaidi inatumia vibaya rasilimali za taifa hili.

Kwa karibu mwaka mmoja na nusu sasa, wafanyakazi wa TRL wanapigia kelele serikali, kwamba waendeshaji wa kampuni hiyo hawana uchungu na Reli ya Tanzania.

Kumekuwa na madai kuwa baadhi ya injini za treni zilizokuwa zikitumika nchini miaka ya nyuma, zimepelekwa nje ya nchi kwa kile kilichoitwa matengenezo lakini hazijarudishwa hadi hivi leo.

Wafanyakazi wanasema kuwa kampuni ya RITES kutoka India ambayo ndiyo inayoendesha kampuni inachota kati ya Sh. 30 milioni na 50 milioni kwa mwezi kwa kulipa mshahara wa ofisa mmoja wa kigeni, huku ikikataa kulipa mishahara ya wafanyakazi wazalendo.

Hata pale serikali inapotoa fedha kukwamua shirika, fedha hizo hazitumiki kama ilivyokusudiwa.

Pamoja na serikali kuibeba TRL iliyochukua kazi ya iliyokuwa shirika la Reli la taifa (TRC), viongozi wa shirika wameshindwa kutimiza wajibu wao.

Wafanyakazi wanalalamika, tena mara nyingi, kuwa baadhi ya vyuma kutoka karakana ya reli vimeuzwa au kusafirishwa nje ya nchi.

Hakika, wakati umefika sasa kwa serikali kutafuna jongoo kwa meno kwa kusema, “Sasa mkataba basi!”

Katika hili, wananchi hawatarajii tena serikali yao kushikwa na kigugumizi. Wanatarajia serikali kuangalia maslahi ya taifa sasa, badala ya huyo anayeitwa “mwekezaji.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: