MENEJEMENTI ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) imeshindwa kuelewana na wafanyakazi wake; imeshindwa kuimarisha njia za usafiri na imeshindwa kuboresha hali za wafanyakazi.
Tayari wafanyakazi wanalalamikia kutokuwapo mkataba wa hiari wa kazi kati yao na mwajiri wao na wanalalamikia kupunjwa mishahara; wakidai mapato yao hayalingani na kazi wanazofanya.
Mamlaka ya Reli ya India (RITES) inayoendesha menejimenti ya TRL ilipewa mkataba wa miaka 25. Lakini hata kabla ya robo ya muda wa mkataba haijafikia, mambo yamekuwa kombo.
Leo hii TRL ni chungu cha migogoro, manung'uniko na kero. Wakati wafanyakazi wanalilia upande mmoja, wananchi ambao walipaswa kuhudumiwa na kampuni wanalilia upande mwingine.
Kabla ya menejimenti ya RITES kutoka India, wananchi walikuwa wakipata huduma ya usafiri, hata kama kulikuwapo usumbufu wa hapa na pale. Kuja kwa waendeshaji kutoka nje sasa ndiko kumeongeza kero na mateso kwao.
Tuangalie baadhi ya kero hizo. Kwanza, menejimenti mpya imeshindwa kuwalipa haki zao baadhi ya wafanyakazi waliopunguzwa.
Pili, imeshindwa kutumia vizuri wataalam iliowakuta, kiasi kwamba mafundi wazuri kama waliopo kwenye karakana ya Morogoro wameachwa bila kazi.
Tatu, kumekuwa na malalamiko kwamba madereva mahiri wa treni wamekuwa wakiwekwa benchi huku wasio wazoefu wakiwekwa mbele.
Nne, bado menejimenti inang'ang'ana na wafanyakazi juu ya haki yao ya kuwa na mkataba wa hiari na hivyo kusababisha mgogoro wa kikazi.
Tano, menejimenti imeshindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati na wakati mwingine kushindwa kabisa hadi kulipiwa na serikali.
Sita, menejimenti imesababisha migomo ya mara kwa mara ya wafanyakazi wakidai mishahara au marupurupu mengine kama malipo ya muda wa nyongeza kazini.
Saba, hali ya usafiri wa treni imekuwa mbaya zaidi kwa maana ya safari nyingi kufutwa wakati abiria wakiwa tayari vituoni na kuwasababishia adha kubwa.
Nane, treni imekosa kiberenge cha kuongozea garimoshi kutokana na kampuni kupunguza baadhi ya wafanyakazi.
Matokeo ya hili ni garimoshi kupita katika njia ambayo haikukaguliwa. Kuna madai kwamba hata baadhi ya ajali zinazotokea huenda zinasababishwa na shirika kupunguza wafanyakazi wake na huduma ya kiberenge.
Kwa mfano, ajali iliyotokea 8 Agosti 2009 katika eneo la Mazimbu – Mkata, nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro, iliyotokana na kung'olewa kwa mataruma ya reli, ingeweza kuepukika kama ungekuwepo utaratibu wa kupitisha kiberenge kukagua njia kabla ya treni kupita.
Katika ajali hiyo, watu 67 walijeruhiwa, wengine wakiwa wameumia sana. Treni iliyopata ajali ilikuwa inaelekea Bara. Ilianzia safari yake kituo kikuu cha Dar es Salaam 7 Agosti 2009.
Treni iliyopata ajali ilianza safari baada ya wafanyakazi kuwa na mgomo wa siku tatu uliovuruga usafiri wa reli na menejimenti kulazimika kurejesha nauli kwa wasafiri "hadi itakapotangazwa upya."
Hii ni mara ya pili kwa wafanyakazi wa TRL kugoma wakiishinikiza menejimenti kukubali kusaini mkataba wao wa hiari.
Mbali na mgororo wa kukosekana mkataba wa hiari, wazo la kutaka kupunguza wafanyakazi watakaofikia 800, linawatia hofu wafanyakazi. Zoezi la kuwapunguza linaweza kufanywa wakati wowote kuanzia sasa.
Meneja Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez, anasema kuwa mkataba wa serikali na wawekezaji hao wa TRL unaruhusu kupunguza wafanyakazi baada ya miaka miwili tangu uanze kutekelezwa. Mkataba wa RITES na serikali unatimiza miaka miwili Septemba mwaka huu.
Ukweli ni kwamba RITES wameshindwa. Kila mmoja anaona wanavyobebwa na serikali. Katika hali hii, serikali itaibeba mpaka lini na itabeba makampuni mangapi ya aina hii? Ifike mwisho tusema kubebwa, sasa basi!
