Tume ya Uchaguzi kitanzini Igunga


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 12 October 2011

Printer-friendly version

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) yaweza “kutiwa kitanzini” iwapo itathibitika kuwa ilichakachua daftari la wapigakura katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Igunga, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya serikali, NEC na mashirika huru ya uangalizi wa uchaguzi nchini, zinaonyesha kwamba idadi ya wapigakura waliomo ndani ya daftari la wapigakura la mwaka 2010 na wale waliotajwa katika uchaguzi mdogo wa Igunga, inapishana tena kwa mbali.

Gazeti hili lilimtafuta mkurugenzi wa uchaguzi, Rajavu Kiravu kuzungumzia suala hili, lakini alielekeza mwandishi kuwasiliana na Rajabu Kiboko. Jitihada za kumpata Kiboko hazikufanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.

Kwa mujibu wa taarifa na takwimu zilizopo, mdau yeyote wa uchaguzi katika jimbo la Igunga, aweza kuiburuza NEC mahakamani; na mwanasheshia mmoja aliyeongea kwa sharti la kutotaka kutajwa jina gazeti ameongeza, “...kuiburuza mahakamani na kuishinda.”

Kuna taarifa za kuondoa majina ya wapigakura; kuongeza majina ya wengine na kuonekana, angalau kwa namba moja ya shahada isiyokuwa na jina mbele yake.

Hata hivyo, idadi ya wapigakura wa Igunga na wale wanaotajwa na NEC kwenye uchaguzi mkuu uliopita, inapingana na idadi ya watu waliomo ndani ya daftari lenyewe, idadi ya takwimu za idadi ya watu nchini na hata mazingira halisi ya nchi.

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja takribani miezi 10 baada ya vyombo vya habari kuanika kile vilichoita, “Mkakati wa wizi wa kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.” NEC ilituhumiwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa usalama wa taifa kupika matokeo.

Kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu iliopita, awali NEC ilitangaza kuwapo wapigakura 20,137,303 kabla ya kuipunguza idadi hiyo hadi wapigakura 19.6 milioni, ambayo bado ilipingwa na baadhi ya wanaharakati na vyama vya siasa.

Wakati idadi hiyo ikistukiwa na vyama, NEC ilidai waliojitokeza siku ya uchaguzi walikuwa ni 8,626,283 (42.8%); wapigakura zaidi 11,511,020 (57.2) hawakujitokeza kupigakura.

MwanaHALISI limetaarifiwa kuwa kazi ya kuingiza wapigakura hewa na kuondoa baadhi ya majina imefanyika kwa ustadi mkubwa, kwa kuhusisha NEC na wataalam wenye ujuzi katika mawasiliano ya kompyuta (IT).

Taarifa zinaonyesha kwenye kata ya Mbutu peke yake, wapigakura zaidi 2500 waliongezwa kwenye dafari hilo kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga. Jimbo la Igunga lina jumla ya kata 26.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa MwanaHALISI, daftari la wapigakura lililotumika kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana, linaonyesha wapigakura waliopo kwenye kituo cha Shule ya Msingi Mwabakima C, kata ya Mbutu, ni 382, lakini daftari lililotolewa na NEC kwa vyama vyote vya siasa katika uchaguzi mdogo wa Igunga, limetaja wapigakura 393.

Daftari hilo lenye wapigakura 382 lilitolewa na NEC, 18 Oktoba 2010.

Kwenye kituo hiki peke yake, daftari linaonyesha ongezeko la wapigakura 11, wakati ambapo NEC haikuwahi kufanya marekebisho yeyote kwenye daftari la wapigakura kati ya 23 Septemba 2010 na 18 Oktoba 2010, wala wakati wa kuelekea uchaguzi mdogo wa Igunga.

NEC inasema katika maelezo yake yaliyo mbele ya daftari hilo, “Daftari hili litatumika kuanzia 15 Oktoba 2010 hadi itakapotangazwa vinginevyo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”

Kati ya wakati huo na sasa NEC haijatangaza kusitishwa kwa matumizi ya daftari hilo.

Kwenye kituo cha Mwambakima shule ya Msingi -3, chenye Na. 00015059, idadi ya wapigakura imeongezeka kutoka 393 waliotajwa na NEC, 18 Oktoba 2010 hadi wapigakura 419 waliotajwa kwenye uchaguzi mdogo.

Katika orodha hiyo yupo mpigakura mmoja ambaye hana jina, wapigakura 10 wameondolewa, wapigakura watatu fomu zao zimefutwa, huku wapigakura saba wakiondolewa bila kuelezwa sababu.

Matokeo ya uchaguzi mdogo katika kituo hicho yalikuwa kama ifuatavyo: Chama cha AFP  kilipata kura 1, CCM 72, CHADEMA 71, CUF  2 na wengine wote waliosalia walipata 0.

“Unajua ukiliangalia kwa makini daftari hili la wapigakura, utaweza kugundua madudu mengi. Kwanza, kuna wapigakura waliondolewa kinyume cha taratibu, lakini pili kuna wapigakura wameondolewa hapa na kupelekwa kwingine, huku wengine wengi wakiondolewa moja kwa moja,” anaeleza mtaalamu mmoja wa IT anayefahamu kinachotendeka ndani ya NEC.

 Anasema, “Katika baadhi ya maeneo baadhi ya wapigakura wameondolewa huku majina yao yakiwa tayari yapo kwenye orodha ya wapigakura. Kwa mfano, wapo wapigakura ambao walikuwa wakiandikishwa na mabalozi wa CCM na huku shahada zao zikionekana, lakini ilipofika uchaguzi majina yao hayakuweza kuonekana. Hii yote inaonyesha jinsi taifa hili linavyoweza kuingia kwenye machafuko...”

MwanaHALISI limegundua wapigakura waliongezeka katika kituo cha Mwambakima shule ya Msingi -3 na namba zao za shahada zikiwa kwkenye mabano.

Hao ni Ngasa Mipawa (29611765), Ngolo Seni (29611909), Nhandi Hungilu (29611919), Nhwani Mlega (47371897), Nkinda Magembe (47371805), Peter John (29611911), Rahel Lunili (05148812) na Rahel Nhabi Buluba(24150227).

Wengine walioongezwa kwenye daftari hilo, ni Samwel Kingi (29611760), Say  Mwitagula (29611768), Sesilia Ntugwa (47371813), Shija  Masanilo Tungu (24150219), Shija Chenge (29611905), Shija Itaalamu (29611770), Silvanus Mangwesi Buluba (47371821), Therezia Charles (47371814) na Tui Peter(29611915).

Wapigakura wengine walioongezwa, ni Wande Kashinje (47371885), Zainabu Ramadhani (47371822), Zengo Buganda Saganda(7371893) na mtu ambaye hakutajwa jina wala picha yake haimo kwenye daftari mwenye kadi ya kupigia kura Na. 29611769.

Wapigakura walioondolewa kwenye daftari bila kutolewa sababu ni pamoja na Nchambi Joseph Ntugwa (24150228), Ng'ombeyapi Machiya (05148590), Nhabi John (05148492), Njile Samwel (05148633), Nkwaya Malelemba (05148394), Nsiya Gusu (    05148927), Poya Magoma (05148462) na  Rahel Maduka (05148858).

Vyanzo vya taarifa vinasema kuingizwa kwa wapigakura wapya kwenye uchaguzi wa Igunga, kulikwenda sambamba na maandalizi yaliyofanywa na CCM ya kupeleka wapigakura hewa zaidi ya 500 waliodaiwa kuingia ndani ya vyumba vya kupigia kura wakiwa tayari na kura zilizopigwa.

Uchaguzi wa Igunga ulikuwa na ushindani mkubwa kati ya vyama vya CHADEMA na CCM. Hadi sasa wapo wanaoamini kwamba iwapo uchaguzi huo ungeendeshwa katika mazingira huru na haki, upinzani ungeibuka na ushindi.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, NEC ilitaja wapigakura wa Igunga pekee kuwa 177, 077 huku kwenye uchaguzi mdogo wakitajwa wapigakura171,019.

Idadi hiyo ina tofauti ya karibu kura 6000, kutoka wapigakura wa mwaka jana (2010).

Aidha, wakati msimamizi wa uchaguzi mdogo wa Igunga, Protace Magayane akitangaza idadi ya wapigakura wa uchaguzi mdogo kuwa ni 171,019, dafatri la wapigakura lililotolewa kwa vyama vya siasa 23 Septemba 2010, linaonyesha wapigakura wa Igunga ni 170,586 tu.

Kuna mikanganyiko inayozaa shaka na ambayo yaweza kuigharimu NEC au viongozi wake na hata CCM.

0
Your rating: None Average: 3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: