Tumejifunza nini kutoka kwa Selebi?

JACOB (Jackie) Sello Selebi (60), aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Afrika Kusini kwa muda wa miaka nane, amekutwa na hatia ya rushwa wiki iliyopita na sasa anasubiri hukumu.
Kabla ya kuwa Mkuu wa Polisi, Selebi aliwahi kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Afrika Kusini kwenye Umoja wa Mataifa (UN) na pia Rais wa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol).
Selebi aliwahi kuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama tawala nchini humo cha ANC na nyadhifa nyingine mbalimbali za kisiasa.
Jambo la msingi kufahamu katika historia ya Selebi ni kwamba hakuwahi kuwa askari. Lakini bado akateuliwa kuwa Mkuu wa Polisi !
Na nafikiri hapa ndipo Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla linapokosea katika miongoni mwa mambo mengi yanayolifanya lidumu katika mkwamo wake wa kimaendeleo.
Selebi ni mwanasiasa. Na sote tunafahamu kwamba ili mtu awe mwanasiasa aliyefanikiwa, ni lazima awe na uhusiano na watu wa aina mbalimbali; wabaya na wazuri.
Na ndiyo maana, kama mtu utaangalia kwa makini, karibu wanasiasa wote duniani walikuwa na uhusiano au wanaendelea na uhusiano na walau mtu mmoja au wawili wenye kutia mashaka.
Anguko la Selebi lilikuwa mahusiano yake na mfanyabiashara Glenn Agliotti. Huyu alikuwa akimnunulia bosi huyu wa polisi nguo za bei mbaya yeye na mkewe. Na si nguo pekee, bali kila aina ya msaada wa mali ambao Jackie aliuhitaji.
Lakini naomba tujiulize swali moja la msingi, hivi ni kwa ni viongozi wetuhawapati somo la nani ateuliwe wapi na kwa nafasi ipi. Ngoja nikupe mifano miwili mitatu ya hapahapa nchini. Na nafikiri itakuwa vema zaidi iwapo nitaanzia na ule wa karibuni zaidi.
Wakati mkataba wa kuendesha lililokuwa shirika la ndege la ATCL baina ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) ulipovunjika (na niliunga mkono uvunjwaji huo), serikali ilifanya uamuzi wa ajabu kidogo.
Ilimteua David Mataka, ambaye hakuwa na uzoefu wowote katika sekta ya usafiri wa anga, kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa ATC, liliporudishwa serikalini.
Inawezekana Mataka ni mtendaji mzuri. Lakini yeye ni mjuzi zaidi wa masuala ya bima na kipindi hicho hata Shirika la Bima la Taifa lilikuwa likiyumba.
Sasa badala ya serikali kumpeleka Bima ambako pengine angefanya vizuri zaidi, akapelekwa ATC ambako alikuwa anakwenda kuanza moja.
Ndani ya ATC na katika sekta ya usafiri wa anga kwa ujumla, walikuwapo watu ambao wangeweza kufanya vizuri zaidi kuliko Mataka lakini wakaachwa kwa sababu ambazo ni serikali pekee ndiyo inayojua.
Matokeo yake ni kwamba sasa serikali imetangaza kuwa ATC imefilisika. Kwa hali ilivyokuwa, haingewezekana kwa mtu kama Mataka kufanya chochote kuliokoa shirika hilo.
Ipo mifano ya viongozi kutoka katika jamii za wafugaji ambao waliteuliwa kuwa wakuu wa wilaya au mikoa ya wakulima. Matokeo yake mikoa hiyo ikarudi nyuma.
Wale watu waliokuwa katika mikoa yenye ushirika, waliosomeshwa na kukulia kwenye ushirika, wakapelekwa kwenye mikoa ya mjini ambako ushirika hakuna kabisa.
Ndivyo tulivyofanya. Ninafahamu madaktari wa binadamu waliopelekwa kuwa mawaziri katika wizara za ujenzi huku wale waliosomea na kuielewa vizuri sekta hiyo wakipelekwa kwenye wizara ambazo naogopa kuzitaja kwa vile naweza kuonekana ninazidharau.
Kama nitaamua kuorodhesha hapa maeneo ambako uteuzi mbovu wa viongozi uliharibu kila kitu, nadhani ukurasa huu hautatosha. Iko mifano mingi mno.
Lakini hili ni jambo ambalo linaweza kabisa kuepukika. Na wenzetu, kwa mfano Marekani, ambako wanajua athari za uteuzi mbaya, wameamua kwamba kuna nafasi ni lazima zithibitishwe na Bunge.
Kuna nafasi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Fedha, Jaji Mkuu, Mkuu wa Majeshi, Gavana wa Benki Kuu na wakuu wa vyombo vingine nyeti kama CIA na FBI.
Hii ni kwa sababu, baadhi ya nafasi zina umuhimu mkubwa kwa taifa na kufanya uteuzi kuwa suala la uamuzi wa mtu mmoja si sahihi. Kama mtakuwa na gavana mbaya wa benki kuu, uchumi wa nchi nzima utaathirika.
Ajira zitapungua na watu wataendelea kuwa mafukara. Kama nchi itakuwa na Mwanasheria Mkuu mbaya, uwezekano wa kuwapo kwa sheria kandamizi utakuwa mkubwa na kwa mfano wa nchi yetu, ufisadi unaweza kushamiri (kama tulivyoona katika miaka ya nyuma).
Kama tutakuwa na wakuu wasiofaa wa vyombo vya usalama, nchi yetu itakuwa hatarini kwa mashambulizi ya kigaidi na hata amani yetu hii tunayojivunia kama wimbo kila siku, haitaweza kudumu.
Kwa kuanzia, ningependa kuona serikali yetu ikikubali kubadilisha sheria zake na kuamua Bunge ndilo liwe likithibitisha uteuzi unaofanywa na serikali.
Uzuri wa kuthibitishwa huku ni kwamba wananchi watapata fursa ya kumjua kiongozi huyo kabla hajakabidhiwa madaraka. Watajua watarajie nini kutoka kwake.
Mtu ambaye ni mwanasiasa, tutajua ni nafasi ipi inaweza kumfaa na ipi haimfai. Tutajua pia kiongozi wa dola anatakiwa kuwa na sifa zipi. Hii ni nchi yetu sote na hatuwezi kuachia mtu mmoja (kama ilivyokuwa kwa uteuzi wa Selebi uliofanywa na Thabo Mbeki) uamue hatma ya nchi yetu.
Tukubaliane pia kwamba ingawa uongozi ni taaluma inayojitegema, lakini yapo mazingira yanayomfanya mtu mmoja awe bora zaidi kwenye nafasi fulani kuliko mwingine.
Kwamba kama kuna wasomi wawili wa ngazi ya shahada ya uongozi; mmoja akiwa mwanajeshi na mwingine daktari, ikitokea nafasi ya Mkuu wa Majeshi, yule mwanajeshi atafaa zaidi kuliko daktari. Huu ndiyo ukweli.
Hilo ndilo funzo ambalo nataka Watanzania tujifunze kupitia kesi ya Jackie Selebi.