Tunawatakia kampeni njema
KAMPENI za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba mwaka huu zinatarajiwa kuanza keshokutwa Ijumaa ambapo vyama vinavyoshiriki vitaanza kujitangaza.
Vyama vilivyoteua wagombea vitapita kujinadi na kuomba kura kwa wananchi huku vikieleza vimepanga kuwafanyia Watanzania iwapo wagombea wao watapewa ridhaa ya kuongoza serikali.
Kikubwa ambacho wananchi wanatarajia kusikia kutoka kwa wagombea hao wawe wa urais, ubunge au udiwani ni sera za vyama vyao kuhusu elimu, afya, uchumi nk.
Ni suala la kila chama na mgombea kueleza sera ya chama chake tu. Katika hili vyama vitapambanisha sera zao; kwamba chama chao kina mtazamo gani au sera nzuri kiasi gani kuliko chama kingine tena kwa lugha ya kiungwana kabisa.
Ni kwa njia hiyo, wananchi watapata fursa ya kusikia, kupima na kuamua chama kipi kipewe ridhaa na kipi kinyimwe. Kwa kuwa lengo la kila chama ni kushawishi wapigakura, hapahitajiki kampeni za kuvuana nguo; kubaguana kwa namna yoyote ile wala kuchochea watu wafanye fujo.
Watanzania wanataka kusikia maneno matamu na lugha ya kistaarab siyo kashfa, matusi au maudhi mengine. Lugha nzuri siku zote humtoa nyoka pangoni.
Wagombea watapaswa kuzingatia ilani za uchaguzi za vyama vyao na kuzifafanua ili wananchi wazielewe na kuachwa wafanye uamuzi.
Tunaamini kila chama kimefanya utafiti wa kisayansi kubaini shida za wananchi wa kila eneo. Basi watu wanatumaini kuelezwa shida hizo zitatatuliwaje. Matusi si sehemu ya utatuzi wa shida hizo.
Itakuwa ajabu kusikia mgombea amepanda jukwaani na kuvurumisha matusi yanayomlenga mshindani wake.
Kampeni za kuchafuana hazijapata hata mara moja kumsaidia mgombea. Anayetaka kushinda nyoyo za wapiga kura, achague lugha ya kuvutia si maudhi.
Tukiwa miongoni mwa Watanzania watakaofika kwenye mikutano ya hadhara kusikiliza kampeni hizo, tunawasihi wagombea na vyama vyao kukaa na kutafakari namna ya kuzingatia taratibu ambazo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza.
Baadhi ya taratibu hizo ni kwamba ni marufuku kwa vyama au wagombea kutoa lugha chafu, kuzomea chama kingine, kubeba vinyago kwa lengo la kukejeli vyama vingine, kuvalisha mbwa fulana za vyama vingine nk.
Vilevile imetahadharisha vyama au wagombea kupita na kuhonga wapigakura. Ukiukwaji wa taratibu hizo, mbali ya kuwa zinaweza kusababisha vurugu, NEC inaweza kukiadhibu chama husika.
Ndiyo maana tunatoa rai wagombea watumie lugha ya ungwana kwani wananchi wanahitaji kusikia sera si dharau na kejeli.
Vilevile tunapenda kuwakumbusha wagombea kujiweka kando na matumizi ya rushwa kwani huo kisheria ni kosa la jinai na utovu wa maadili usiokubalika.
Tanzania inapokuwa taifa la viongozi watoa rushwa wakati wanatafuta uongozi itakuwa inajipiga msumari mbele ya macho ya dunia. Itakuwa na viongozi jeuri na wasio wasikivu.
Tunawatakia kila la kheri wagombea waliopitishwa na vyama vyao kuwania nafasi mbalimbali, na pia tunavitakia kila la kheri vyama vilivyojitosa kuomba ridhaa ya kuongoza.