Tusichague ‘wanaojifunza’ kutuongoza

NANI amepata kusikia watu wanaojitokeza kuwania uongozi katika uchaguzi mkuu ujao? Bila shaka, wengi wamepata fursa hiyo.
Ni kwa sababu, kila kukicha bingwa mmoja anajitokeza akiwa anaamini kuwa yeye hatimaye amepata suluhisho la matatizo yetu; kutokana na ujuzi wake huo mpya; naye anataka kugombea.
Ukiwasikiliza kwa muda kidogo tu, haraka utabaini kuwa wote – kuanzia wagombea udiwani hadi urais, wameamua kufuata kitabu cha “Ulaghai wa Kisiasa cha 2010.”
Kijitabu hiki ambacho wagombea karibu wote wanacho, kinatoa maelekezo ya mambo ya kusema wakati wa kugombea ili uweze kuvutia wananchi.
Kwa mfano, kitabu kinaelekeza mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mambo yanayompasa kusema ili kuonyesha kuwa yeye ni mtu wa mabadiliko, na kwamba chini ya uongozi wake na chama chake, jimbo fulani au hata nchi nzima itabadilika.
Ukiwasikiliza bila kupima kile wanachokisema, haraka unaweza kuamini tatizo la taifa hili, ni ukosefu wa maji, shule, umeme, na kadhalika.
Hata ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kuwa serikali imeanza mpango wa kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana ndani ya mita mia nne kwa kila mwananchi ifikapo 2025 inawavutia wasio na uwezo wa kufikiri wala kupima hoja.
Anayefurahia ahadi ya kuwa na maji safi mita mia nne kutoka nyumbani kwake, ni mwehu. Utaweza vipi kushangilia kupata maji safi mita mia nne (usawa wa viwanja vinne vya mpira wa miguu) kutoka nyumbani kwako?
Sababu pekee ya wewe kushangilia ni kule kuamini kwamba uwezekano wa kupata maji safi ndani ya mita 10 ya nyumba yako ifikapo 2025!
Jingine katika kitabu hicho cha “Ulaghai wa Kisiasa,” ni mgombea wa CCM kujitokeza na kusema mambo ambayo umma utamuona kuwa yeye ni “mpya.”
Wagombea wote wanapojitokeza, huanza kwa kueleza sababu ya kwanini wanataka kugombea. Karibu wote wanaahidi vitu vilevile, ambavyo unaweza kufikiri kuwa ni vitu vipya.
Kwanza, wanataka “kushirikiana na wananchi ili kuleta maendeleo.” Kwamba, katika historia ya taifa hili, hakujawahi kuwepo “ushirikishwaji wa wananchi;” kazi hiyo itaanza baada ya wao kuingia madarakani.
Hoja hii haina mashiko. Ni kutokana na kitu kinachoahidiwa kinatakiwa kutekelezwa bila hata ahadi. Je, utawezaje kuongoza wananchi bila ya kushirikiana nao?
Kuongoza bila kushirikiana na wananchi, ni sawa na fundi ambaye anataka ashone nguo bila kuchukua vipimo vya mwenye nguo yake.
Au yule anayeomba ajiriwe katika ujenzi wa nyumba, halafu ana ahidi kutoa “ushirikiano katika kujenga nyumba.” Sasa angetoa ushirikiano wa kuibomoa?
Pili, wagombea wetu wanatuambia kwamba “wanazifahamu changamoto zinazowakabili wananchi.” Hili nalo halina mashiko hata kidogo. Ni mwananchi gani asiyejua changamoto zinazomkabili?
Kwa miaka zaidi ya 40 sasa, changamoto zetu kama taifa zinajulikana na hakuna ambaye anaweza kuja kutuambia amezielewa. Vijijini hakuna umeme, hakuna maji, hakuna zahanati na wala hakuna vituo vya afya.
Maneo mengi ya vijijini, hayana shule zenye hadhi za msingi na sekondari; hakuna walimu wa kufundisha watoto wetu; hakuna watalaamu wa kilimo na mifugo wenye hadhi na ujuzi wa kufanya kazi inayotakiwa.
Hata maeneo ya mijini, changamoto zinazotukabili tunazifahamu na tunazielewa.
Kitu ambacho wagombea wetu hasa wale wanaotaka katika chama kilichopo ikulu hawajakisema, ni utatuzi wa changamoto hizo. Watazitatua vipi, kwa fedha gani, muda gani watakaotumia na kwa namna gani watazikabili.
Badala yake, wanasema jambo la kwanza watakalolifanya, watashirikiana na “wananchi kutafuta suluhisho.”
Tatu, wagombea wengi wanakuja na kauli kuwa “watatumia uwezo wao na elimu” katika kusaidia kutatua matatizo ya wananchi katika majimbo wanayogombea.
Je, kuna kiongozi ambaye hataki kutumia akili na uwezo wake katika kuongoza? Miaka mitano iliyopita hakuna mgombea ambaye aliahidi kutumia uwezo na akili yake?
Kama walikuwapo, kwanini tunafikiria hawa wa sasa wanaotoka katika chama kilekile kilichochoka, wataongoza kwa namna tofauti?
Mbona tumekuwa na viongozi wengi, wasomi na waliobobea katika mambo ya uongozi na utawala, wenye elimu nzuri, lakini baadhi yao ndio wanaotuhumiwa kulifikisha taifa hapa lilipo?
Nne, karibu wagombea wote wanatumia kisingizio kuwa wanataka kugombea kwa sababu “ni haki yao ya kidemokrasia.”
Hili nalo halina mashiko. Nani amesema wanapotangaza kugombea kuna mwananchi anayefikiria kuwa kuna watu wamewashikia bunduki kisogoni kuwalazimisha kugombea?
Kama wanataka kugombea kwa sababu ni demokrasia na ni haki yao, kwanini wanahubiri kana kwamba wana mashaka nao?
Ni vema tusimsikilize kila mgombea – kuanzia yule anayeahidi kukushirikiana na wananchi,” kukabiliana na changamoto, hadi yule anayejitapa kutumia uwezo na akili yake kukabiliana na matatizo yaliyopo jimboni kwake.
Tusimsikilize kwa sababu mgombea huyo ameishiwa. Ana ahidi ambacho hakijawahi kuahidiwa kwa miaka 50 iliyopita!
Kwamba yote anayoahidi hakuna hata moja ambalo limewahi kutekelezwa kwa kiwango cha kusema “miaka mitano ijayo itakuwa tofauti.”
Sikumbiki rais Kikwete aliahidi nini mwaka 2005 wakati anagombea kwa mara ya kwanza. Lakini kimoja ninachokikumbuka, rais amesema miaka miwili ya kwanza alikuwa darasani akijifunza kazi za urais. Sina hakika, kama hili alilisema wakati anaomba kura.
Bila shaka, ingekuwa amelisema, wananchi wasingemchangua. Ni kwa sababu Watanzania hawakutaka kupeleka ikulu, mtu wa kujifunza kazi.
Tanzania ina matatizo makubwa mawili tu. La kwanza, ni kukosekana kwa uongozi na la pili ni la ufisadi. Yote mawili yameshikamana kama pande mbili za shilingi.
Matatizo haya hayawezi kuanza kutatuliwa kwenye majimbo au mitaani kama tunavyojaribu kwa muda mrefu. Matatizo haya yanaweza kutatuliwa bungeni.
Hata hivyo, si watu wote wanaoweza kutatua matatizo haya. Ni wale tu, wenye dhamira ya dhati.
Hivyo basi, tunahitaji wagombea ambao hawatatuahidi vitu vya kipuuzi, bali wale wanaotuahidi kuwa wanataka kufanya nini wakienda bungeni, watasimamia nini, watabadilisha sheria zipi?
Wasipotuambia wanachotaka kukifanya tofauti na kinachofanywa sasa, wagombea hawa tusiwachague. Kuendelea kuchagua mtu ambaye bado hajahitimu, ni kuzidi kujitafutia matatizo.