Ubunge Mbeya 'vurugu' tupu

KINYANG’ANYIRO cha ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya kimeibua mgawanyiko wa aina yake.
Baadhi ya wabunge hawapikiki chungu kimoja na viongozi wa serikali. Kila mmoja na lwake.
Kundi moja linabeba karibu wabunge wote wa mkoa huo, akiwamo mbunge wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya na mbunge wa Chunya, Victor Mwambalaswa.
Wengine katika kundi hili ni mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, Profesa Mark Mwandosya (Rungwe Mashariki) na Hilda Ngoye (Viti Maalum).
Hali ni tete. Karibu kila mbunge ana mpinzani – kuanzia mmoja hadi wanne.
Hata hivyo, Profesa Mwandosya na Profesa David Mwakyusa wanaweza kuwa na ushindani dhaifu kutokana na wapinzani waliojitokeza.
Kamanda wa vijana wa mkoa wa Mbeya, Steven Mwakajumilo, ambaye ni mtumishi wa Benki Kuu (BoT) tawi la Mbeya, tayari ametangaza kumvaa Mwandosya.
Naye aliyewahi kuwa mbunge wa Kigamboni kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Frank Magoba ametangaza kupambana na Mwakyusya.
Bahati pekee aliyonayo Mwakyusya ni kwamba Magoba tayari amemaliza msululu wa vyama, hivyo hana mtandao wa kutosha ndani ya CCM.
Dk. Mwakyembe anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mfanyabiashara Elias Mwanjala na George Mwakalinga.
Mara kadhaa Mwakyembe amekuwa akilalamika kuchezewa rafu na mkuu wa mkoa John Mwakipesile kwa madai kuwa anasaidia washindani wake. Mkuu huyo wa mkoa amewahi kukaririwa akisema anataka mbunge anayeweza kutatua matatizo ya wananchi katika jimbo hilo.
Mwambalaswa ana kibarua kigumu kukabiliana na mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Njelu Kasaka. Kasaka aliyehamia CUF kabla ya kurejea CCM amejipanga kuomba ridhaa ya wanachama.
Naye mbunge wa Songwe, Guido Sigonda anakabiliwa na ushindani mzito kutoka kwa wagombea wengine wanne akiwemo mbunge wa zamani Paul Ntwina.
Mbunge wa Mbozi Magharibi, Lucas Siame atakabiliana na wanachama watatu akiwamo mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Eliakimu Simpasa, mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi, Aden Mwakyonde na mweka hazina wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini, Aglipa Senka.
Gideon Cheyo, mbunge wa Ileje, hajaeleza kama atagombea tena.
Lakini tayari wanachama kadhaa wakiwamo Victory Kanama, meneja wa NSSF wilaya ya Rungwe, Aliko Kibona na mwingine aliyetajwa kwa jina moja, Mbwagha, wametajwa kuwania jimbo hilo.
Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Aloyce Mdalavuma, William Kapenjama na mwanachama mmoja wa CCM aliyefahamika kwa jina moja la Dk. Mbwanji.
Hata hivyo, nafasi ya Zambi kushinda bado ni kubwa, hasa kwa kile kinachodaiwa “kutimiza majukumu yake.”
Kivumbi kipo katika jimbo la Mbeya Mjini, ambako mbunge wa sasa, Benson Mpesya anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mbunge wa kuteuliwa Tom Mwang’onda na mfanyabiashara Frank Mwaisumbi.
Mwang’onda, mtoto wa aliyekuwa mkurugenzi wa usalama wa taifa, Colnel Apson Mwang’onda anaonekana anaweza kumtikisa Mpesya.
Mchungaji Lackson Mwanjale anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Alan Mwaigaga ambaye ni wakala wa kampuni ya magari ya Toyota mjini Mbeya.
Mwaigaga aliwahi kuwa mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Mbeya mjini, 2002- 2007. Katika uchaguzi uliomwingiza madarakani Mwanjale kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Richard Nyaulawa, Mwaigaga alishika nafasi ya pili nyuma ya Mwanjale.
Mwanjale anajivunia rekodi yake ya kufanya kazi kimya, upole, lakini asiye na makeke majukwaani. Yeyote atakayepitishwa na CCM atapambana na mgombea wa upinzani, mwanasheria wa kujitegemea, Sambwee Shitambala.
Mbunge wa sasa wa Mbarali Esterina Kilasi ana wakati mgumu wa kushawishi wanachama wampitishe tena.
Picha yake imeanza kufifia na anakabiliwa na ushindani wa nguvu kutoka kwa mkurugenzi mkuu wa mtandao wa makampuni ya kahawa (Kilicafe), Geofrey Mwangulumbi, mwanasheria wa kujitegemea Mchungaji Dk Lonlick Mchami, kamanda wa vijana wa wilaya, Mhandisi Burton Kihaka pamoja na wengine watatu.
Kwa jumla mkoani Mbeya kuna makundi yanayokinzana. Kundi la kwanza linaongozwa na mkuu wa mkoa Mwakipisile ambalo linaitwa “kundi la wateule.” Jingine ni lile linaloundwa na baadhi ya wabunge wakiongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe.
Hata hivyo, hali inaweza kubadilika iwapo mapendekezo ya kugawa majimbo ya Mbozi Mashariki na Mbozi Magharibi yataridhiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Tayari Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) imependekeza kuundwa kwa majimbo mapya ya Igamba ambalo litakuwa na kata tisa na watu 236,557; na Mbozi Mashariki lenye kata sita na watu 210,426.
Imependekezwa jimbo la Mbozi Magharibi ligawanywe na kutoa jimbo jipya la Ndalambo lenye kata sita na watu 75,995.
Aidha, imependekezwa jimbo la Rungwe Magharibi ligawanywe na kuundwa jimbo jipya la Bonde la Ufa lenye wakazi 99,444.
Jingine ni Mbeya Mjini kwa kuundwa majimbo mapya ya Kisima na Iyunga.
Jimbo jingine ni Mbarali ambalo linakadiriwa kuwa na wakazi 282,911. Imependekezwa kugawanywa katika majimbo mawili ya Mbarali Mashariki linalokadiriwa kuwa na watu 161,047 likiwa na kata 10.
Jingine ni Mbarali Magharibi likiwa na kata 10 na idadi ya watu wanaofikia 121,864.
Hata hivyo, tayari mgawanyo huo wa majimbo umezua tafrani baada ya kuwapo tuhuma za sura ya ukabila kwa wakazi wa maeneo hayo kunakoletwa na sababu mbalimbali zikiwemo za kijiografia.