UCHAGUZI MKUU: Waandishi wa habari wasimame wapi?

KIPENGA kimepulizwa. Andika! Hivi ndivyo waandishi wa habari nchi nzima wanavyoambiwa sasa.
Wakati wa mavuno kwa wanasiasa ndio wakati wa mavuno pia kwa waandishi wa habari. Tusisahau, ndio wakati wa mavuno kwa wananchi.
Katika mbio za kuvuna, wanaotafuta utukufu wa kisiasa wanaweza kuvuna maua, ngwela au mazao yaliyokomaa; kwani kuna joto kali na kimbunga kinachobadili mwelekeo bila taarifa na bila huruma.
Wenye vyombo vya habari vinavyotangaza wanasiasa, waweza kuvuna fedha katika huduma na biashara ya kuuza habari.
Waandishi wa habari waweza kuambulia masazo ya “vijisenti” na kashfa; lakini waweza pia kuvuna sifa kwa umahiri wao katika kusaidia jamii kuelewa na kufanya maamuzi.
Kwani nyakati kama hizi za kwenda kwenye uchaguzi mkuu, baadhi ya waandishi hukaa kama kunguru – midomo wazi – wakijisemea kimoyomoyo kuwa lolote likija likute mdomo wazi.
Baadhi huvaa nyuso za mgegemo, huku ndani wakijenga maghorofa ya kupaa na washindi: kama siyo sasa kwa kiganja kutekenya, basi uteule katika nafasi kitulizo.
Wananchi nao wanaweza kuvuna magugu, mbigiri na hata upupu; kwani hawajui nani ni nani. Kila mwanasiasa anakuja meno juu; mashavu tanu; wakipepeta ahadi tamu zisizofanana na nyuso wala mitima yao.
Lakini Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kimewaonya waandishi wote na kuwataka kukataa kununuliwa. Kimewaonya wananchi pia, “…anayekuhonga hafai!”
Maadili ya uandishi wa habari yamesisitizwa na Baraza la Vyombo vya Habari (MCT) na vyama vya waandishi wa habari ambavyo bado vina uongozi thabiti.
Asasi za kijamii, za ndani na nje ya nchi, zimetaka waandishi wawe thabiti katika kuandika ukweli; kutoonea upande mmoja au kupendelea na kusifia upande mwingine; kutokashifu na kutoelemea, vizuri au vibaya, chama chochote kinachoshindana.
Yote yamesikika. Nami, hapo zamani za kale, nilikuwa mtafutaji wa habari. Mkusanyaji wa habari. Mwandishi wa habari. Msanifu wa habari. Mhariri wa habari na mchapishaji.
Kwa muda wote huo, nilijifunza jambo moja kubwa; nalo ni kwamba maneno husema. Maneno huwa na maana ya kile ambacho yanasimamia.
Neno moja, kama lilivyo kundi la maneno – sentensi au aya – husema. Neno ni fungamani. Hakuna neno popo litokalo kinywani mwa mtu au kwenye wino wa kalamu yake au ncha za vidole vyake kwenye kompyuta mbele yake.
Maneno yamezidi binadamu anayeyatumia. Wakati binadamu anaweza kuwa mnafiki, maneno aliyoyasema kulinda unafiki wake huweza kumuumbua; kwani hayafanani na sura yake. Hayafanani na matendo yake. Hayafanani na ahadi zake. Ni mbingu na dunia.
Huu ndio wakati basi wa kutumia maneno sahihi kuelezea: Huyu anayetaka udiwani, ubunge, urais ni nani, wa wapi, analenga nini, ameibuka tu, kachomekwa au ni mrithi wa baba au babu yake?
Je, kuna anachojua juu ya siasa anazotaka kutumikia? Ana elimu kweli – siyo vidato na digrii tu – ana uelewa; ana maarifa?
Mgombea ana malengo gani? Anataka awe kiongozi ili iweje? Anataka mabadiliko? Mabadiliko yapi iwapo yuko katika chama kilichopanga ikulu? Mabadiliko gani kama anatafuta kuingia ikulu?
Wagombea watasema. Waandishi wa habari watasikia. Wataandika. Lakini wataandika nini ili wasionekane wamependelea chama chochote, mtu yeyote anayetafuta ofisi ya kisiasa au upande wowote?
Hapa, bahati mbaya, kuna njia moja tu ya kutofungamana na mtu yeyote. Lakini hakuna njia ya kutofungama na upande wowote.
Katika siasa kuna watu na vyama vyao. Vyama vina kauli. Wagombea wana kauli pia. Lakini kitu muhimu ni kwamba vyama, kama wagombea, vina upande vinaosimamia. Hata vikiwa katika itikadi moja, bado vinaweza kuwa na mirengo tofauti.
Ni pande hizi ambazo, tutake tusitake, ndizo zitasumbua waandishi, wanasiasa na wananchi katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
Bali ni waandishi wanaopaswa kuelewa vizuri zaidi ili kusaidia – kwa njia ya kutoa habari – wananchi kupata taarifa za kutumia kuchambua na kupembua kabla ya kuchagua.
Ili waandishi waweze kufanya kazi yao vizuri wanahitaji kukiri nguvu ya kila neno. Mara hii siyo kuanza na neno la mwanasiasa. Ni kuanza na neno la mwananchi mpigakura. Anasema nini? Anataka nini?
Mbona kila siku tunakariri kuwa mwandishi wa habari awe jicho la nyongeza, sikio la nyongeza na mdomo wa nyongeza wa jamii?
Tumekuwa tukikariri na wengine kutenda kwa msingi kuwa mwandishi aone zaidi, asikie zaidi na apaze zaidi sauti – kutumikia wasioona, wasiosikia na wasio na sauti katika jamii zao.
Hili ndilo linafanya kazi ya uandishi isianzie kwenye kuandika; bali ianzie kwenye kufikiri, kuona, kutafiti, kukusanya, kuchambua na hatimaye kuandika.
Mwandishi ameishi katikati ya wengi ambao kila kukicha wanalia, “Twafa!” Kama kilio ni kwamba wanakufa – siku zote na sasa – miaka 50 baada ya uhuru wa kisiasa, yuko wapi mwandishi ambaye hawezi kuelewa kuwa kilio cha wengi leo ni mabadiliko?
Na kila neno lina maana na linajisemea. Twafa, linavyosimama katika herufi tano, linatikisa na kuacha mwangwi usioisha masikioni na akilini mwa wanasiasa, waandishi na wananchi wote.
Katika hali hii, mafunzo yote, maelekezo, vitabu vyote juu ya maadili ya uandishi wa habari, hukiri kilio cha wengi cha miaka mingi na matakwa ya sasa ya kujiondoa katika msiba na matanga yaliyopitiliza.
Bali kazi ya mwandishi, licha ya kujielekeza kwenye matakwa ya wengi – uhuru na haki – haiwi kuhubiri. Huwa kuchimba, kuibua, kuweka wazi kwa kila mmoja kuona na kufurahia au kuchukia na kuchukua hatua.
Hii ndiyo huduma sahihi ambayo waandishi wanaweza kutoa kwa jamii yao wakati huu. Ni huduma ambayo inakana kutofungamana na upande wowote.
Ni huduma inayokiri kufungamana na ukweli, uhuru na haki; inayosaidia wananchi kuvunja ukimya wa kauli na vitendo; na kutupilia mbali minyororo iliyonyong’onyeza utashi wao.
Ni huduma inayotoa nafasi kwa mwanasiasa kufahamika zaidi kwa anaowaomba kura – mwelekeo wake, uwezo wake, upungufu na tabia yake.
Kwamba anayeomba kura aliwahi kubaka, kuiba, kutoroka shule au kuwa kiranja, siyo kashfa. Hizi ni “sifa” zisizostahili kufunikwa na chama chochote, kwani vyama ni wanachama na viongozi wake.
Uoza wa wanachama ndio uoza wa chama; ndio chimbuko la kuogopa au kushindwa kutenda hata kama wameingia ikulu.
Uandishi ibuzi, ndani ya sera, programu, malengo, kauli za wanasiasa, marafiki zao katika biashara kubwa, watendaji wakuu katika utawala na wananchi kwa jumla, waweza kusaidia wananchi kupata taarifa sahihi za kufanyia maamuzi.
Kwa kutumia taarifa hizo na nyingine, wapigakura waweza kujiuliza, kabla ya kuchagua: Huyu na chama chake, ndiye atatuwezesha kutoka kwenye tope? Kwa taarifa sahihi wanaweza kufanya chaguo sahihi.