Uchaguzi tayari umevurugwa


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 16 June 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
John Tendwa, Msajili wa Vyama vya Siasa

UCHAGUZI mkuu ujao tayari umevurugwa. Na kama hatua za haraka hazitachukuliwa, taifa linaweza kuwa miongoni mwa nchi zinazoendesha uchaguzi mbovu tangu nchi irudi katika mfumo wa vyama vingi miaka 17 iliyopita.

Hata hivyo, iwapo hili likitokea, anayestahili kubebeshwa lawama, ni viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali.

Si kwa sababu tuna “chuki binafsi,” ila ndiyo wenye kuendesha serikali; kutunga sheria na ndiyo walioweka vyombo vyote vinavyoendeshaji uchaguzi.

Kuvurugika kwa uchaguzi wa mwaka huu, hakuwezi kuwaingiza wafadhili, wapiga kura au wapinzani. Iwapo uchaguzi utaenda kombo watu wa kulaumiwa ni CCM na serikali yake.

Uchaguzi si kupiga kura tu. Mojawapo ya mambo ambayo ukiyaangalia kwa karibu utaona yanasumbua ni nadharia kwamba uchaguzi ni siku ya kura. Msisitizo mkubwa utaona wanauweka kwenye siku ya kupiga kura kana kwamba uchaguzi mzima unahusiana na siku hiyo peke yake.

Hilo nimeweza kuliona kwenye hotuba ya rais Jakaya Kikwete aliyoitoa kwa makatibu tawala wa mikoa na viongozi wengine ambapo kwa kiasi kikubwa mawazo yalionekana kuelemea kwenye kuhakikisha “siku ya uchaguzi” wananchi wanapiga kura katika mazingira ya utulivu na amani.

Hivyo, vyombo vya usalama na vyombo vingine vya serikali vitajitahidi sana kuhakikisha siku ya “uchaguzi” hali inakuwa shwari.

Hata hivyo, fikra za kuona kuwa uchaguzi ni kupiga kura tu, ni fikra potofu. Kwa sababu uchaguzi ni zaidi ya kupiga kura na ni zaidi ya kujipanga mstari au kuweka dole gumba kwenye wino.

Uchaguzi ni mchakato mzima wa kuhakikisha mwananchi anapata fursa ya kupima ajenda za vyama vya siasa, kupima wagombea, na hatimaye kuweza kufikia uamuzi wa kuchagua mtu amtakaye pasipo hila au mbinu zozote ambazo zinazotishia uhuru wake wa mpiga kura.

Kuna vitu vitatu ambavyo serikali imevitengeneza katika mfumo huu wa vyama vingi ambavyo vinaweka bayana kuwa uchaguzi kamwe hauwezi kuwa huru na haki.

Kwanza, ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Hiki ndicho chombo chenye wajibu wa kusimamia uchaguzi. Uundwaji wake unafanywa na rais bila kushauriana na mtu mwingine yoyote yule.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri (Ibara ya 74) rais aweza siyo tu kuwateua watu fulani kuwa wajumbe wa tume hiyo ya uchaguzi lakini pia “aweza tu kumwondoa katika madaraka mjumbe wa tume hiyo kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake, ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote, au kwa sababu ya tabia mbaya au kupoteza sifa za kuwa mjumbe.”

Kwa maneno mengine, rais ana nguvu kubwa katika kuisimamia tume ya uchaguzi na hivyo kuinyima uhuru wake.

Hebu fikiria: Kama rais anaweza kumuondoa mjumbe wa tume “kwa sababu nyingine yoyote” au “kwa sababu ya tabia mbaya” vitu ambavyo katiba haisemi ni tabia gani mbaya au sababu gani nyingine ni nini, kitamzuia rais kumuondoa mjumbe endapo ataona kuwa haweki maslahi ya chama cha rais?

Kukosekana kwa uhuru huu kumechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya NEC kuwa chombo kinachokidhi mahitaji ya kisiasa zaidi.

Kwa mfano, licha ya kwamba katiba inakataza kwa “kiongozi wa chama cha siasa” kuwa mjumbe wa tume, lakini haikatazi kwa mwanachama wa chama cha siasa kuendelea na uwanachama wake.

Matokeo yake, tumeona wakati ambapo mtu aliyewahi kuwa mjumbe wa NEC akionesha nia ya kutaka kugombea uongozi kupitia chama kilichopo ikulu!

Pili, Msajili wa Vyama vya Siasa; Huyu hayuko huru. Hili linathibitishwa na yaliyotokea katika sakata zima la usajili wa chama kipya cha sisasa – CCJ, Chama Cha Jamii.

Kwa wale wenye kumbukumbu nzuri wanaweza kukumbuka jinsi msajili wa sasa John Tendwa alivyopigwa mkwara na Ramadhani Mapuri baada ya kujaribu kuikemea CCM kutokana na hatua yake ya kuwatambulisha wagombea wake kabla ya wakati wa kampeni.

Ofisi ya msajili ilivyo sasa haiwezi kutekeleza kazi zake kwa uhuru unaotakiwa ili kuhakikisha vyama vya siasa vinafanya kazi kwa uhuru sawa.

Kutokana na kukosekana kwa uhuru huu, msajili amejikuta akifanya mambo ambayo ukiyaangalia kwa karibu utaona yanahusiana moja kwa moja na maslahi ya chama tawala.

Lakini fikiria vile vile kuwa sheria imempa uwezo kamili – kukipa chama usajili au kukifuta. Hakuna mwenye mamlaka ya kuhoji hatua hiyo.

Tatu, waziri anayesimamia siasa. Huyu ni kada wa CCM. Anatenda kwa maelekezo ya chama chake; CCM ilitengeneza utaratibu huu ili kujihalalishia madaraka.

Mfano mzuri ni mahusiano katika ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Siasa na Bunge), Phillip Marmo na ofisi ya Tendwa. Waziri ni mwanasiasa, kada wa CCM na mjumbe wa vikao vya juu ndani ya chama hicho. Sheria imemuweka waziri kuwa na maamuzi yenye athari kubwa kwenye ofisi ya msajili.

Msajili akitaka kukifuta chama cha siasa ni lazima waziri akubaliane naye. Inakuwaje kama waziri tayari ameshafikia uamuzi kuwa chama fulani hakitakiwi kuwepo?

Je, itakuwaje kama chama fulani kinatishia chama cha waziri kiasi kwamba yeye na msajili wanaamua kutafuta sababu ya kukinyima usajili au kukifuta?

Zaidi ya hayo sheria inampa waziri uwezo wa kupitisha taratibu mbalimbali za utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa na hasa utendaji kazi wa msajili. Sasa kama waziri ambaye ni mbunge, akiamua kutengeneza utaratibu wenye lengo la kunufaisha chama chake? Nani anaweza kumzuia kufanya hivyo?

Leo hii, upo mjadala wa kutengeneza maadili ya uchaguzi ambayo msajili na waziri wana nafasi kubwa ya kuyasimamia. Je, ni nani atahakikisha kuwa maadili hayo hayatatengenezwa ili kuwakomoa wagombea maarufu au ambao wataonekana kuwa wanaungwa mkono na wapiga kura wengi?

Hakuna mfumo wa kumsimamia waziri isipokuwa kutegemea tu kuwa atakuwa na “roho nzuri” ya kutenda haki.

Kwa mambo haya makubwa matatu utaona kuwa kwa jinsi hali ilivyo hivi sasa hakuna uwezekano wa mchakato wa uchaguzi kuwa huru.

Yote tunaweza kuyoana kuanzia kupitishwa kwa sheria yao mbaya ya gharama za uchaguzi ambayo itatuletea matatizo mengi ikiwamo kusababisha kesi nyingi zaidi za kupinga matokeo.

Ni wazi kuwa kwa vile wapinzani wanajua haya yote niliyoyadokeza hapa kwa kukubali kwao kushiriki uchaguzi katika mazingira haya wanajiweka katika nafasi ya kulalamika sana huko mbele. Hata wagombea wengine wa CCM wataandamwa.

Njia pekee ya kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki ni kuhakikisha kuwa vyombo vyote vinavyohusiana na masuala ya demokrasia ya vyama vingi nchini vinakuwa huru kutoka katika ushawishi wa wanasiasa.

Kinyume cha hapo, siku ya uchaguzi yaweza kuwa ya utulivu na amani, lakini mchakato mzima wa uchaguzi kutawaliwa na vurugu, uonevu, ukandamizaji na ubabe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: