Umarisheni utekelezaji wa Mpango


editor's picture

Na editor - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MPANGO wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaofungua fursa mbalimbali kwa wananchi kujiletea maendeleo kwa kutumia raslimali zilizopo nchini umewasilishwa bungeni juzi.

Serikali iliyoandaa mpango huo imeeleza kuwa hali ya uchumi wa taifa inaruhusu kuwa na mpango huo. Katika michango yao, baadhi ya wabunge waliunga mkono moja kwa moja lakini wengine walionyesha wasiwasi katika utekelezaji.

Uzoefu unaonyesha kwamba wataalam wa mipango ni wengi, na kumekuwa na mipango mingi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo na uchumi, lakini mafanikio yaliyopatikana ama ni kidogo au hakuna, tatizo kubwa likiwa ni usimamizi katika utekelezaji.

Tunaungana na wabunge walioonyesha wasiwasi juu ya utekelezaji wake tunashauri serikali ijipange barabara kuhakikisha ufanisi unakuwepo ambao ni kupunguza au kuondoa umaskini wa kipato kwa wananchi.

Kasoro ziko wazi. Kila mwaka serikali hutoa ripoti na mwenendo wa kiuchumi kuonyesha uchumi unakua kwa asilimia 7.0, lakini umaskini nao unaongezeka na kufanya hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu.

Katika kipindi ambacho serikali inasema kuwa uchumi unakua, jamii imekuwa ikishuhudia pia shilingi ikishuka thamani. Moja ya sababu za msingi za kushuka kwa thamani ya shilingi ni uchumi wa nchi kuyumba.

Kwa hiyo, kama uchumi unakua kwa kasi, mfumko wa bei umedhibitiwa lakini umaskini unaongezeka, basi kuna kasoro katika ripoti au tafiti. Maadamu umaskini unaongezeka, basi kukua kwa pato la taifa hakuna tija kwa mwananchi.

Serikali inapaswa kufanyia kazi dosari hii na kufanyia kazi maeneo kadhaa kama vile utawala bora na wa sheria.

Katika baadhi ya maeneo serikali imeacha wanajeshi au matajiri au wawekezaji kuchukua au kupora mashamba na maeneo ya kiuchumi ya wakulima na wachimbaji wadogo.

Hatua hii inasababisha watu wazima wenye nguvu ya kufanya kazi kukosa maeneo ya kilimo katika kipindi hiki cha utekelezaji wa Kilimo Kwanza.

Baba wa Taifa alitufundisha kwamba ili nchi iendelee inahitaji mambo manne—watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Watu ambao ni nguvu kazi wapo, ardhi ipo ya kutosha kinachohitajika hapa ni siasa safi na uongozi bora unaojali misingi ya utawala bora, sheria, demokrasia na haki za binadamu ili wananchi watumie raslimali kukuza uchumi na kuondoa umaskini.

0
No votes yet