Uraia wa Joseph Kabila wazidisha kizaazaa Kongo


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
Wakongomani walia na majeshi ya UN

ADRIEN Christofer Kanambe, yule baba mzazi wa  rais wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Joseph Kabila, anatoka kabila la Watutsi nchini Rwanda.

Taarifa zilizopatikana zinasema baba huyo ni Mnyarwanda wa tumbo la wazazi wawili Wanyarwanda. Alizaliwa na kukulia Rwanda. Alikimbia nchi yake mwaka 1958.

Adrien alikimbia baada ya Gregoire Kayibanda wa kabila la Wahutu, kupindua utawala wa kifalme wa Omwami Kigeri wa V aliyekuwa mtusi.

Christofer, ambaye katika maandishi mbalimbali jina lake linaandikwa pia kama Christopher, alikimbilia Kongo. Aliishi eneo la Salamabela, mpakani mwa Manyema na Kivu ya Kusini, Mashariki mwa Kongo.

Alipotoka Rwanda mwaka 1958 alikuwa akijulikana kwa jina la Adrien Christofer. Jina la “Kanambe” alijipachika ili aweze kujichanganya na wakazi wa Salamabela. Hakutaka kujulikana kuwa ni Mnyarwanda.

Mmoja wa wapiganaji nchini Kongo aliyeongea na mwandishi wa habari hizi mjini Lubumbashi na kuthibitishwa na mwenzake jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, alikiri kumfahamu Kanambe, baba mzazi wa Hypolite Christofer Kanambe (Joseph Kabila).

Anasimulia pia alivyokuwa na Kanambe katika Bandari ya Wimbi, tarafa ya Fizi, Kivu Kusini; hata kabla Kanambe hajamuoa Marcelina, mama yake Joseph.

Anasema, “Tulipoingia bandari ya Wimbi, tulimkuta Adrien Christofer Kanambe pamoja na wanajeshi wake wa kabila la Kitusi.”

Adrien na watutsi wenzake, baada ya kukimbilia Kongo, waliunda jeshi. Waliahidi kusaidia wapinzani wa utawala wa Joseph Kassavubu na Jenerali Joseph Mobutu (Sese Seko).

Ulikuwa mkataba wa aina yake; kwamba wasaidie wenzao kumwondoa Mobutu na baada ya ushindi, majeshi ya Kongo yawasaidie kuondoa “utawala wa kihutu” nchini Rwanda.

Wakati mwanamapinduzi wa kimataifa kutoka Latini Amerika, Che Guevara anaweka mguu wake Wimbi, kulikuwa na majeshi mawili.

Che Guevara aliingia Kongo kupitia Tanzania. Askari wa Kabila walimfuata Kigoma na kumpeleka moja kwa moja hadi bandari ya Wimbi. Hapa ndipo alitambulishwa kwa majeshi mawili.

Jeshi la kwanza lilikuwa la Wakongomani chini ya Laurent Kabila. Lilikuwa likiongozwa na Jenerali Kaliste Majaliwa wa kabila la Wabembe. Jeshi la pili lilikuwa la askari wa Kitusi wakiongozwa na Adrien Christopher Kanambe.

Mtoa taarifa anaeleza kuwa walishirikiana vizuri na Adrien Christopher Kanambe, wakati huo Hypolite Kanambe (Joseph Kabila) hajazaliwa.

Marcelina, mama yake Hypolite (Joseph), aliolewa na Adrien Christopher Kanambe mwaka 1968. Joseph alizaliwa mwaka 1972.

Baada ya shambulio lililolenga kuteka mji wa Moba kutoka mikononi mwa Mobutu kushindwa, Laurent Desire Kabila aligombana sana na wenzake.

Ugomvi ulikolezwa na chupa ya dhahabu ambayo wapiganaji walikuwa wameteka katika mashambulizi yao na kuwasilisha kwa mkubwa wao, Laurent Kabila.

Wakati wapiganaji walitaka wampe mwenzao aende kuuza ili wapate fedha za kununulia silaha, Kabila alichukua chupa na kumkabidhi ndugu yake aliyetajwa kwa jina moja la Yave, ili aende kuziuza Lusaka, Zambia.

Laurent Kabila alifadhaika sana baada ya jeshi lake na lile la kitusi lililoongozwa na Adrien Christopher Kanambe kushindwa kuteka Moba Moba katika shambulio lake la kwanza mwaka 1984.

Kutokana na kushindwa huko, Laurent Kabila “alimuhukumu kifo” Jenerali Kaliste Majaliwa, (Mbembe) aliyekuwa akiongoza majeshi ya Wakongomani.

Lakini Jenerali Majaliwa alikimbilia Tanzania, katika mji wa Ujiji, Kigoma ili kunusuru maisha yake.

Baada ya Jenerali Majaliwa kukimbia, Kabila akampa Adrien Christopher Kanambe uongozi wa majeshi yote mawili – la Watutsi na lile la Wakongomani.

Kuona hivyo, Wabembe wakakataa kushiriki katika shambulio la pili lililoitwa Moba II mwaka huohuo wa 1984. Walitamka wazi kwamba hawawezi kushiriki kwa kuwa Laurent Desire Kabila “amemhukumu kifo” ndugu yao – Jenerali Kaliste Majaliwa.

Kuona hivyo, Kabila akaamuru Adrien Christofer Kanambe kuogoza jeshi lake la kitusi peke yake kuivamia Moba. Adrien alikubali. Alienda vitani.

Vita vilikuwa viguvu sana. Inasadikiwa askari wapatao 180 wa kitutsi, kati ya 200 aliokuwa nao Adrien, waliangamizwa na majeshi ya Mobutu. Adrien alipigwa risasi na kuvunjika mguu.

Wakongomani wa kabila la Wabembe walimwonea huruma Adrien; walimvusha kwa mtumbwi kutoka bandari ya Moba hadi bandari ya Wimbi ambako kulikuwa na makao makuu ya chama cha Laurent Kabila – Parti de la Revolution du People (PRP).

Wale waliompeleka Adrien Christofer Kanambe kule Wimbi akiwa majeruhi, walisemezana kuhusu hatima yake. Hapa kuna maelezo ya aina mbili.

Maelezo ya kwanza ni kwamba waliompeleka walipewa amri na Laurent Kabila ya kumtosa majini kwa madai kuwa alikuwa “msaliti” kutokana na kushindwa vitani.

Maelezo pili yanasema waliogopa kumpeleka kwa Kabila kwa hofu kwamba wote wangeuawa; hivyo wakaamua kumtupa majini.

Mtoa taarifa amesema, “…bali ni kweli kwamba Adrien Christofer Kanambe alitupwa Ziwa Tanganyika ili kutekeleza ‘hukumu’ ya Kabila aliyopitisha baada ya kumtuhumu usaliti katika vita vya pili vya kuwania Moba.

Kifo cha Adrien, mwaka 1984 kiliongeza mtafaruku katika makao makuu ya PRP; na kwa kuwa Kabila alitaka kumuua Jenerali Kaliste Majaliwa, basi Wabembe walimchukia sana na kujikuta hana ulinzi tena.

Baada ya kifo cha Adrien, Laurent Kabila alimchukua Marcelina, mke wa Kanambe. Akawa mke wake.

“Wabembe walitishia kummaliza kabisa Laurent Desire Kabila; ndipo alipoamua kukimbilia Tanzania, akimchukua Marcelina, Hypolite (Joseph) na dada yake Jeanette na kuwabwaga Dar es Salaam.

Jijini Dar es salaam walifikia mtaa wa Sinza ambako waliishi kwa muda kwa Bw. Didier Kazad Nyembo.

Hata hivyo, kufuatia Laurent Kabila kuingia ikulu, Nyembo alifanywa mkuu wa usalama wa taifa, cheo ambacho ameshakitema. Hivi sasa ni mfanyabiashara ya madini nchini Kongo.

Didier Kazad Nyembo, ambaye jijini Dar es Salaam alijulikana kama “Didi,” naye hakuwa Mkongomani. Taarifa zinasema ni Mrundi na majina yake halisi ni Didier Nyambere.

Kutoka Sinza kwa Nyembo, Marcelina na watoto wake walitafutiwa nyumba ya vyumba viwili eneo la Msasani ambako waliishi kama mume na mke kabla Marcelina kwenda Uganda kutafuta msaada kwa ndugu zake waliokuwa katika jeshi la Museven.

Huko Uganda Marcelina alikutana na Fred Rwigema, mwanzilishi wa chama cha Paul Kagame cha RPF – Rwanda Patriotic Front.

Rwigema alikuwa miongoni mwa vijana Wanyarwanda waliokuwa wamekubaliana na Museven kuwa wamsaidie katika kuchukua madaraka Uganda na kwamba baada ya hapo naye awasaidie kuchukua madaraka Rwanda.

Rwigema ametajwa kuwa binamu wa Marcelina na ombi la mwanamke huyo kwake lilikuwa kumsaidia kusomesha watoto wake. Taarifa zinasema Rwigema alikubali.

Ndipo Marcelina akatuma habari kwa Laurent Kabila, Dar es Salaam kwamba apeleke watoto Uganda, yaani Hypolite Kanambe (Joseph) na dada yake Jeanette. Laurent Kabila aliwapeleka.

Akiwa Uganda, Hypolite Kanambe aliishi nyumba moja na mjomba wake, James Kabarebe ambaye hivi sasa ni mkuu wa majeshi wa Rwanda. Kabarebe ni kaka wa Marcelina, mama yake Hypolite.

Taarifa za mpashaji zinasema Museven alishinda vita nchini Uganda na Fred Rwigema akawa mmoja wa viongozi wakuu katika jeshi la Uganda.

Ndipo Rwigema aliunda kampuni ya uvuvi iliyoitwa Uganda Fishing Company ikifanya kazi zake katika Ziwa Kitwe wilaya ya Kasese. Kampuni hii alikabidhiwa Hypolite Kanambe kuiendesha.

Baadaye Hypolite Kanambe (Joseph) alikuja Dar es Salaam kuonana na Laurent Kabila. Alitumwa na mama yake aje kumshawishi ili aende Uganda kufungua medani ya mapambano dhidi ya Mobutu.

Laurent Kabila alikubali. Alienda Uganda. Akiwa na wenzao ambao mtoa taarifa anakumbuka kwa  mashaka, akina Benade, Filippe Mbanta, Edward na Sikatende, akaanzisha harakati za kijeshi kwenye mlima wa Ruwenzori mwaka 1987.

Mbumba Nathanael, kiongozi wa chama cha FLNC, akitokea Libya, alitua Dar es Salaam mwaka 1987.

Mtoa taarifa anakumbuka jinsi Mbumba alivyomtuma rafiki yake wa karibu kwenda Uganda kufungua medani ya kijeshi ya FLNC.

Anasema huko alikutana na Hypolite (Joseph) pamoja na akina Laurent Desire Kabila.

Uhusiano wa Adrien Christofer Kanambe, Museven, Paul Kagame na Kabarebe ni wa muda mrefu. “Nakumbuka kuna wakati Museven alipokuwa porini, alikuja Wimbi na akina Rwigema kuomba msaada ya risasi na bunduki kwa Kabila,” anasimulia.

Taarifa zinasema akina Museven waliwahi pia kuomba msaada huo wa silaha kwa chama cha Mbumba na kwamba hakuwanyima.

Hata hivyo, mtoa taarifa anasema wakati huo, hakuna vita vyovyote ambavyo unaweza kusema walipata ushindi wa kukumbukwa.

Katika kipindi hicho, akisaidiwa na Adrien, inadaiwa kazi yake kubwa Laurent Kabila ilikuwa “kufukuzana na madini. Tulikuwa hatuna oganaizesheni nzuri. Hakuna vita tulivyoshinda. Mnakamata eneo asubuhi, jioni mnavurumishwa; na ndio sababu Che Guevara aliondoka haraka,” anaeleza mtoa taarifa hizi.

Sasa kwa nini Kongo haitulii na mapigano ya sasa ndani ya nchi hii kubwa ni ya nini?

“Tunapambana kwa sababu Kongo iko mikononi mwa Wanyarwanda. Inaongozwa na Mnyarwanda. Hypolite Kanambe (Joseph Kabila) ni Mnyarwanda; Mtusi asilimia 100. Hili halina ubishi,” anaeleza kwa sauti ya kusononeka.

“Tunapigana kwa kuwa wananchi hawanufaiki na utajiri wa nchi yao. Wavamizi wanachukua kupitia huku; makampuni ya nje yananyonya kupitia kule; mwananchi anabaki masikini mwimba muziki,” analalamika.

Yuko wapi Marcelina, mama yake Hypolite? “Bado yuko Kinshasa; anafichwafichwa, haonekani hadharani. Mara utasikia yuko Kigali, mara yuko Kinshasa. Mimi nimeishi nao wote Wimbi makao makuu ya PRP,” anaeleza.

Hivi karibuni yameibuka madai kutoka kwa wakazi wengi wa Kinshasa kwamba, Mama Sifa Mahanya, ambaye amekuwa akidaiwa kuwa mama wa Hypolite Kanambe (Joseph), sasa afanyiwe vipimo vya vinasaba (DNA) kabla ya uchaguzi mkuu.

Wapinzani wa kabila wanadai kuwa Sifa Mahanya “ametafuta mgogoro mkubwa na Wakongomani” na kwamba unaweza kungharimu.

Hebu angalia hili, anasema mtoa taarifa, “Uganda imehamishia vita Kongo; Rwanda imehamishia vita Kongo; kila mmoja na sababu zake ambazo hazina mashiko.

“Uganda, tangu 1996 inamtafuta Joseph Konyi; imeshindwa kumkamata. Sasa inapeleka majeshi yake kulinda amani Darfour na Somalia. Rwanda vivyo hivyo; interhamwe wake hawaishi hadi lini? Huu ni uongo,” anaeleza mtoa taarifa.

Mkongomani huyu analaani nchi jirani kwa kuua Wakongoni. Anasema viongozi wa kijeshi (anawataja majina), “…wameua Wakongomani zaidi ya milioni sita (6,000,000)”

“Hekima iko wapi? Uko wapi ukweli? Wanyarwanda 800,000 ndio genocide (mauaji ya kimbari); lakini Wakongomani milioni sita ni wanyama? Sio binadamu?” anauliza.

Hata Jeshi la Umoja wa Mataifa (UN) nchini Kongo lenye askari wapatao 17,000 linalaumiwa kwa “makengeneza.”

Lawama kuu ni kushindwa kwake kuwakamata Bosco Taganda, Mnyarwanda anayeongoza jeshi la Laurent Nkunda (Nkundabatware) la CNDP.

Anasema Laurent Nkudabatware na wakuu wengine wa majeshi ya nchi jirani, waliingiza majeshi nchini Kongo na kuua raia; lakini jeshi la UN haliwaoni. Lenyewe linamshikilia Jean Pierre Bemba “eti ni muuaji.”

Hofu ya majeshi ya UN, anasema ni kama ile ya majeshi ya nchi za wavamizi. Wanaogopa kwamba Jean Pierre Bemba akishiriki uchaguzi Kongo, atashinda kwa kishindo.

“Wanamshikilia ili kuzima nyota ya Wakongomani kung’ara,” anaeleza huku hatua kwa hatua, macho yake yakigeuka kuwa mekundu.

Wachunguzi wa mambo ya siasa Kongo wanasema mjadala wa uraia wa Hypolite Christofer Kanambe (Joseph Kabila) umeshika kasi katika sehemu kubwa ya Mashariki mwa Kongo na miji mikubwa nchini humo.

Wanasema kwa kadri mjadala unavyopanuka, waweza hata kusababisha kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu. Uchaguzi ukiahirishwa kutatokea nini?

0
Your rating: None Average: 4.7 (3 votes)