Ushetani huu basi
WAKATI wananchi wanahamu ya elimu kuhusu masuala ya katiba, mawaziri, viongozi waandamizi na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamegeuka shetani.
Katika mikutano yao mingi, wanajitahidi kuwaambia wananchi wasikubali kupotoshwa na wapinzani.
Viongozi hao hukamilisha tungo zao kwa kuwaambia wananchi “Msisikilize wanasiasa uchwara wasioitakia amani nchi yetu.”
Kwetu, hilo si tatizo maana CCM wameona dalili za kuanguka kihistoria.
Tatizo tunaloliona viongozi hawa kukataa kueleza wananchi sababu za serikali kushindwa kutoa elimu ya uraia kwa umma.
Hawajaeleza kwa uwazi kwanini hawajasambaza nakala za katiba; au kwanini wazuie mtu kuwa nayo.
Wala hawajasikika wakieleza kile kinachowapa hofu kukuta asasi za kiraia zikiwagawia wananchi katiba ili kujisomea.
Ni dhahiri wananchi wengi hawana elimu ya katiba. Na hili si jambo la bahati mbaya. Ndivyo watawala waaminivyo. Raia usimpe elimu ya kujitambua, atakung’oa.
Kwa hivyo basi, kwa miaka yote ya taifa hili, wamewajenga raia katika nidhamu ya woga. Wamewaziba wasione umuhimu wa elimu ya uraia kwa hofu ya kuja kupanga kuwaangusha.
Sasa wakati huu serikali imelazimika kutunga sheria ya kuanzisha mchakato wa taifa kupata katiba ya kwanza iliyoridhiwa na wananchi wenyewe, hofu kwa watawala imeongezeka.
Wanaogopa wanapoona wananchi wanaelimishwa kuhusu katiba. Wanaogopa kwamba wananchi watajua haki zao, watazieleza na kuzidai. Wanaogopa kuwa watazitafuta kwa njia yoyote ile.
Kwa sababu hiyo, wanapita kuwatisha wananchi. Wanawapa kasumba ya kuendeleza woga badala ya ujasiri wa kutafuta elimu ya uraia.
Ama hakika huo ni ushetani wanaoueneza kwa Watanzania. Ushetani haukubaliki. Hakuna mtu mwenye hatimiliki ya kuelimisha wananchi kuhusu haki zao.
Tena yafaa watawala wajue kuwa baada ya kushindwa kuitumikia katiba iliyowapa mamlaka kuwaelimisha raia, hakuna mipaka ya kuwapatia elimu hiyo.
Tunahimiza asasi za kiraia zitie nguvu katika wajibu huu. Zifundishe raia haki zao ili wazidai kwa watawala.
Hakuna nafasi ya watawala kuendelea kudhani ni wao tu wenye haki ya kuwaelekeza wananchi, wengine wote wasimame pembeni wakikomaza woga kwa watu.
Watanzania wanahitaji kuelimishwa sasa ili watakapokuja kuulizwa wanataka nini katika katiba, wajue wanachopaswa kujibu.