Usiri hatari migodini


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version

USIRI umeghubika migodi nchini. Katika usiri huu, ukweli hauwezi kupatikana.

Ni kwenye mgodi wa dhahabu wa Tancan, ndani ya msitu wa hifadhi ya taifa ya Kigosi, kata ya Igulwa, kilomita 80 kusini magharibi mwa makao makuu ya wilaya ya Bukombe, mkoani Shinyanga.

Shuhudia mieleka kati ya diwani wa CHADEMA na kaimu meneja mkuu wa Tancan inayochimba dhahabu katika kata ya Igulwa:

Diwani Yusuph: Mimi nimefanya kazi kwenye migodi ya dhahabu kwa miaka saba. Mtambo huu (akiugusa) ndio wa mwisho katika usafishaji dhahabu na kinachotoka hapa ni dhahabu safi. Sasa huwezi kusema hamjaaza uzalishaji.

Meneja Headlam: Ni kweli, huu ndio mtambo wa mwisho katika kuchuja dhahabu; lakini sio kwamba tumeanza uzalishaji. Huu tunautumia tu katika utafiti wetu.

Hiyo ndiyo hali halisi. Wenye mgodi hawakutegemea kufumaniwa na mjuzi. Hii inaonyesha wanafanya watakalo; waweza kuwa tayari wanachimba madini bila serikali kujua.

Lakini kufika kwenye mgodi “ndiyo ngoma.” Wiki mbili zilizopita Prof. Kulikoyela Kahigi, mbunge wa Bukombe, alijaribu kwenda Tancan.

Alifuatana na madiwani watatu wa chama chake: Yusuph Fungameza wa Uyovu, Patrick Kalugusi wa Namonge na Sudi Ntanyagala wa Igulwa ambako ndiko kwenye mgodi.

Kwenye msafara huo pia kulikuwa na polisi wawili wenye silaha na mwandishi mmoja wa habari.  

Kizingiti cha kwanza: Kilomita 25 hivi kutoka barabara kuu, kuingia msitu wa Kigosi, mti umekatwa; umeangukia barabarani na kuziba njia. Inaonekana wazi kuwa mti umekatwa muda mfupi uliopita.

Dereva anatafuta njia mbadala. Anarudi barabarani ambako kuna makorongo yaliyojaa maji – madimbwi. Kizingiti cha pili.

Kilomita moja kabla ya kufika geti la mgodi, lori linaonekana mbele. Linakuja kwa kasi. Dereva wa msafara wa mbunge anasimama kupisha lori.

Lakini dereva wa lori naye anasimama kama mita kumi mbele. Baada ya takriban nusu dakika, dereva huyo anaondoa lori lake kwa kasi na kubamiza gari la mbunge kwa upande wa dreva. Kizingiti cha tatu.

Lori hilo la tani 15, mali ya Tancan, lenye namba ya usajili, T 207 BJT, limebeba kifusi. Linaendeshwa na Mkwisa Olimbaga Mwakibete.

Polisi: Kwanini unatugonga makusudi?

Mkwisa: Gari langu halina breki.

Polisi: Kwanini unaendesha gari lisilokuwa na breki?

Mkwisa: Huku ni porini bwana; breki za nini?

Polisi: Kwani porini ndio unatakiwa uendeshe gari lisilokuwa na breki?

Mkwisa: Maswali yote ya nini? Kwani ninyi mmefuata nini huku?

Mwandishi: Kwani huku watu hawaji?

Mkwisa: Kimya.

Polisi: Lete leseni yako.

Mkwisa: Sina leseni hapa; iko Mwanza ofisini kwetu.

Polisi: Kwanini unaendesha gari bila leseni?

Mkwisa: Leseni porini ya nini?

Mara wanaingia waendesha pikipiki watano; kila pikipiki ikiwa imebeba watu wawili – wote kwa pamoja 10. Vitisho. Kizingiti cha nne.

Hawa walivaa sare za walinzi wa mgodi, akiwemo aliyejitambulisha kuwa “mkuu wa ulinzi,” Kejo Yoram.

Ndipo dereva Mkwisa akaachia mdomo: “Mnatafuta nini huku? Hamnifanyi chochote ninyi. Kama mmekuja kwa shari semeni.”

Akitazama waliokuja kwa pikipiki, aliendelea, “Nenda kawaite wote (walinzi) ili tuwaonyeshe. Wamefuata nini huku?” Hakuna aliyeondoka.

Msafara wa mbunge ulikwenda hadi kwenye geti. Hapa ulikutana na Kaimu Meneja Mkuu, Robert Headlam. Alichosema ni kwamba meneja mkuu hayupo naye hawezi kujibu baadhi ya maswali. Kizingiti cha tano.

Hata hivyo, mmoja wa askari wa wanyamapori alininong’oneza kuwa kuna eneo jingine zaidi ya tulipokuwa, na kwamba huko kuna wafanyakazi, mahema, magari na uwanja wa ndege. Msafara haukuruhusiwa kwenda huko.

Akijibu swali la Prof. Kahigi kama wameanza kuchimba dhahabu, Headlam alisema “bado tunafanya uchunguzi.”

“Lakini haiwezekani utafiti ufanyike kwa miaka minane wakati humu kulikuwa na wachimbaji wadogo wakichokonoa dhahabu kwa vijiti na majembe,” alishangaa Prof. Kahigi.

Naye diwani Sudi Ntanyagala alitaka kujua Watanzania ambao wanashirikiana na mwekezaji kutoka Canada,  lakini meneja Headlam aligoma kutoa maelezo kwa madai kuwa ataingilia masuala ya ofisi kuu aliyosema ipo Mwanza.

Kwa vitisho na vikwazo hivi vya Tancan, usiri unaongezeka na migodi inakuwa sehemu ya nchi nyingine na siyo Tanzania.

0
Your rating: None Average: 4.2 (6 votes)