Utajiri wote unavunwa na wageni North Mara


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 28 April 2010

Printer-friendly version

UNATAKA kujua kampuni ya Barrick inayomiliki mgodi wa dhahabu wa North Mara inapata shilingi ngapi kwa siku, mwezi au mwaka?

Ni rahisi. Chunguza kiasi wanachopata vijana wa eneo la Nyamongo kwa kuchakata vipande vya mawe visivyohitajiwa tena na mwekezaji katika machimbo ya Nyabirama.

Au, zunguka mji wa Nyamongo na kuona kila kilichomo ambacho kimetokana na mauzo ya dhahabu zilizopatikana kwa njia ya uokotezaji na uchakataji mawe yaliyotupwa nje ya mgodi.

“Maduka, magari, pikipiki, nyumba, biashara – vyote unavyoviona hapa – vimetokana na kuokoteza tu mawe, siyo kuchimba,” anaeleza Maguta Sasi.

Sasi ambaye ni mkazi wa Kewanja, kata ya Kemambo, wilaya ya Tarime anahoji, kama mji wa Nyamongo umejengwa kwa kuokoteza dhahabu, “...jiulize, wenye mgodi wanavuna shilingi ngapi?”

Akiwa amepanda pikipiki anayosema alinunua kutokana na fedha za kuuza dhahabu, Sasi anasisitiza, “Hatuwezi kuacha kuchukua mawe hayo na kuyachakata kwa sababu maisha yetu yanategemea madini.”

Uchakataji ndiyo shughuli pekee ya kuwaingizia kipato wakazi wa Nyamongo yaliko machimbo ya dhahabu ya Nyabirama, Nyabigena na Gokona katika eneo la mgodi, mkoani Mara.

Nyamongo ni eneo lenye utajiri mkubwa wa miamba yenye hazina ya dhahabu. Wakazi wake huhangaika kila siku kuchakata mawe ili kupata dhahabu.

Baadhi yao wanachimba dhahabu katika maeneo ya Itandora, Musege na Kerende kwa nyenzo duni; bali wengi huchukua mawe wanayodai yametupwa katika eneo la Nyabirama.

Kabla ya eneo la Nyabirama kuuzwa kwa mwekezaji katika mazingira ya kutatanisha, wakazi wa Nyamongo walikuwa wakichimba dhahabu kwa kutumia vijiti, majembe, sululu na chochote chenye ncha.

Wachimbaji hao wadogo walipata dhahabu na mamilioni ya shilingi. Walijenga nyumba, wakafanya biashara, wakanunua vyombo vya usafiri, wakaoana na kuzaa watoto, na kujitosheleza katika maeneo kadha wa kadhaa.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa uchimbaji dhahabu kuwa kazi ya kila siku na kuchukua nafasi ya kilimo. Uchimbaji ulikuwa neema kwao.

Lakini utajiri huu uliporwa kwa njia ya mkataba uliotiwa saini kinyemela na viongozi 15 wa vijiji vitano. Mkataba ulipora miliki ya wachimbaji wadogo.

Leo hii wachimbaji wadogo wametupwa nje na wachakataji mawe yenye mabaki ya dhahabu huishi kwa kukimbizana na polisi wanaolinda mgodi wa Nyabirama.

Ingawa nyaraka mbalimbali zinaonyesha kuwa kampuni ya Afrika Mashariki Gold Mines (AMGM) au East Africa Gold Mines (EAGM) ilianza kufanya mikataba ya hila mwaka 1995, ripoti zinasema ilianza kufanya utafiti mwaka 1996.

Ripoti ya serikali na hata mtandao wa kampuni ya Barrick iliyorithi miliki ya mgodi huo inaonyesha uchimbaji wa uzalishaji ulianza mwaka 2002; mwaka mmoja kabla ya AMGM kuuza hisa zake kwa kampuni nyingine, Placer Dome.

Kitabu cha “Tanzania: Opportunities for Mineral Resource Development” kinasema kuwa uzalishaji ulianza mwaka 2002 na kwamba uzalishaji kwa mwaka ni aunzi 140,000 sawa na tani 4.3 za dhahabu kwa mwaka.

Ripoti nyingine ya serikali inaonyesha mgodi wa North Mara una hazina ya tani 116.23 na huzalisha tani 8.51 (aunzi 267,000) kila mwaka.

Hadi kufikia 2005 mgodi ulilipa serikalini dola 9.58 milioni kama mrabaha na ulilipa dola 20.92 milioni “kama kodi mbalimbali.”

Katika huduma za jamii mgodi umetumia dola 4.22 milioni hadi mwaka 2005.

Ripoti ya Barrick inayojumuisha taarifa za mapato ya migodi yote duniani, ukiwemo wa North Mara inaonyesha kwa muhula wa mwisho mwaka 2009, kulikuwa na ongezeko la asilimia 118 ya mapato hadi dola 604milioni kutoka dola 277 milioni.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba baada ya kuondoa gharama mbalimbali za uendeshaji, pato kamili kwa muhula huo lilikuwa dola 215 milioni.

Ukadiriaji uliofanywa 31 Desemba 2002 chini ya EAGM, mgodi wa North Mara una hazina ya tani 2.94 milioni za dhahabu.

Makadirio mengine yaliyofanywa 31 Desemba 2004 chini ya Placer Dome yalionyesha eneo hilo kuwa na hazina ya aunzi 3.9 milioni.

Hiyo ilitokana na upanuzi wa mgodi uliowezesha kuongeza uchimbaji kutoka tani 2.0 milioni hadi 2.8 milioni. Gharama ya dhahabu ilikuwa kati ya dola 200 na 252 kwa aunzi moja.

Hii ndiyo hali halisi. Dhahabu inampa raha na faraja mwekezaji wa kigeni; lakini inakuwa laana kwa mwananchi anayefukuzwa katika eneo lake na haruhusiwi hata kuokota mawe yaliyotupwa nje ya mgodi.

Kuwepo ripoti inayoonyesha hazina kubwa ya dhahabu kuliwapa nguvu wajumbe wa kamati ndogo ya maridhiano kati ya wananchi na kampuni ya Barrick inayomiliki mgodi.

Kamati iliundwa na kuketi tarehe 21 Oktoba 2008 kujadili namna vijiji jirani na mgodi huo vitakavyonufaika na utajiri wa ardhini.

Kamati hiyo iliyokuwa na wanavijiji na wanasheria wa Barrick, ilipendekeza vijiji husika kuteua wajumbe watakaoshiriki kuhakiki mapato.

Wajumbe hao wakishirikiana na wataalam wengine walitarajiwa kuruhusiwa kuhakiki mawe ya dhahabu yaliyochimbwa, yaliyosagwa, dhahabu iliyopatikana, iliyosafirishwa na mauzo yake ili kuwepo malipo ya ubia (siyo mrabaha) “yatakayotolewa bila mapunjo.”

Msingi wa pendekezo hilo ni kutaka kujua asilimia moja (1%) inayopaswa kutolewa na kampuni kwenye mfuko wa dhamana wa elimu ni kiasi gani.

Ilipendekezwa siku hiyo pia kwamba wachimbaji wadogo waingizwe kwenye mpango wa Barrick wa kuwasaidia ili waendelezwe kielimu na kiuchumi.

Vilevile ilipendekezwa kampuni ijenge nyumba za walimu, madarasa, vituo vya afya, sekondari hadi kidato cha sita, ipeleke maji na umeme hadi vijiji vinavyohusika.

Aidha, Barrick imeendelea kuwa “chimongo” – mtafunaji – wa hazina ya madini ambayo Mwenyezi Mungu amewapa Wanyamongo.

0
No votes yet