Uwazi na fasihi ya EPA


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 16 September 2008

Printer-friendly version

SUALA la wizi wa mabilioni ya shilingi kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT), lingali bichi.

Ubichi unatokana na mambo mengi. Leo tujadili kukosekana kwa uwazi: Nani alihojiwa na Timu ya Rais, alihojiwa nini na alisema nini.

Ni muhimu kusisitiza mapema kuwa uwazi ni muhimu pia kwa kuwa suala la uteketeaji fedha za EPA siyo suala la mtu binafsi.

Hapa kuna taarifa kuwa Timu ya Rais Kikwete ya kufuatilia wizi wa Sh. 133 bilioni kutoka akaunti ya madeni ndani ya BoT “haikuwahoji” watu muhimu.

Kuhoji watu “muhimu” ni suala moja na hoja ya kwanza. Hoja ya pili ni Timu kutafuta kuona iwapo fedha za EPA zilitumika katika kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Haikutegemewa rais atoe hadidu za rejea kwa hoja ya pili; na hakika hakufanya hivyo. Bali huko, na kwingine, ndiko kuna kila sababu ya kujengea mashaka.

Lakini kupatikana kwa taarifa za Timu ya Rais, juu ya waliowahoji na majibu yao, kungesaidia kuondoa ukungu juu ya nani aliiba, vipi, kwa njia zipi na lini.

Leo twende kwa uchambuzi wenye sura ya hisia ili kutafuta chembechembe za hoja zinazoweza kusaidia kuleta fununu juu ya “siri ya EPA.”

Kuna madai kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Phillip Mangula hakuhojiwa na Timu ya Rais. Ni kweli au ni hisia?
 
Je, leo akitokea Mangula na kusema aliitwa Dar es Salaam kutoka nyumbani kwake Njombe ili aweze kuhojiwa, nani atambishia?

Je, Mangula akisema alikwenda Dar es Salaam lakini kabla ya kuonana na Timu ya Rais alikwenda kwa rais mstaafu, Benjamin Mkapa kupata ushauri. Nani atambishia?
 
Je, Mangula akijitokeza na kudai kuwa Mkapa  alimkataza kujiwasilisha kwa Timu ya Kikwete kwa kusema, “Wanachunguza nini wasichojua,” nani atambishia?

Nani atabisha? Na hata akiwepo wa kubisha, atapata wapi ushahidi wa kile kinachoitwa “asilimia 40” ya michango ya wafanyabiashara kwa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama kizee?

Ubishi utasaidia nini katika kupata nyaraka na vikaratasi vya ruksa (memo) kati ya Gavana Daudi  Balali na Mangula katika sarakasi hii ya EPA?

Niliwahi kuuliza “Balali akirudi itakuwaje?” Alifariki kabla ya kurejea nchini. Leo Mangula yupo na buheri wa afya. Nani atambishia? Hebu furahia umuhimu wa uwazi katika utendaji serikalini.

Twende mbele. Je, akijitokeza Mkapa na kusema “vijana” walikwenda kwake na kuomba ushauri juu ya kupata fedha za kuendeshea kampeni na yeye akawalekeza jinsi ya kufanya, nani atambishia?

Je, akisema waliporudi kwake alisikitika kuona kuwa walikuwa wanataka fedha nyingi sana na yeye akawaambia wazipunguze. Nani atamtilia mashaka? Tatizo ni kufanyia kazi za umma gizani.

Na akijitokeza na kusema aliruhusu njia mbalimbali, na kuzitaja njia hizo, ili zitumike kupata fedha za kufanyia kampeni za CCM mwaka 2005, na njia hizo ni pamoja na matumizi ya fedha za EPA, yuko wapi mwenye ubavu wa kumpinga kwa kile akijuacho?

Turejee kwenye kibwagizo: Kuhoji watu wote waliokuwa kwenye ulingo, kueleza walivyohojiwa, maswali waliyopewa na majibu yaliyopatikana, ni muhimu ili kuondoa uvumi, shutuma na tuhuma.

Kukataa kuhoji mkubwa – rais, rais mstaafu, waziri mkuu, waziri, mfanyabiashara mkubwa au hata sheikh na askofu, ni kukuza woga usio na msingi na kuwaingiza wahusika katika lawama ambazo huenda hazistahili kuwaelemea.

Timu ya Rais haikumhoji Salome Mbatia Mweka Hazina wa CCM na kiongozi wa makusanyo yote ya fedha za kampeni mwaka 2005. Timu iliundwa baada ya Salome kufariki katika ajali ya gari.

Hata hivyo, Salome alikuwa na la kusema juu ya fedha zilizokusanywa kwa ajili ya kampeni za CCM: Nani alichangia, kiasi gani, ziliwasilishwa na nani na kama mtoaji alikuwa amekamilisha kiwango chote cha ahadi yake.

Itakuwaje pale mwanasheria anayejulikana kwa jina la Sanze wa kampuni ya uwakili ya Malegesi Law Chambers akijitokeza leo na kusema aliitwa na Timu ya Rais lakini hakuandikisha ushahidi? Itakuwaje?

Akijitokeza Sanze na kusema alipata wateja wanaotaka kusajili makampuni na kupata huduma mbalimbali za kitaaluma na akawahudumia; na mmoja wao ni Rostam Aziz anayetajwa kuhusika na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, nani atambishia? Si atakuwa anajua hivyo?

Je, Sanze akienda mbali na kueleza nani alikuwa akifika ofisi za Malegesi kusainisha nyaraka na nani alikuwa akipokea fedha kupitia matawi ya benki ya CRDB? Si atakuwa anamfahamu vema?

Kutowahoji watu muhimu kama huyu, au kutoweka rekodi ya kile wakijuacho, ama ni kutojua madhara yake au ni kuwatosa makusudi katika tuhuma nzito.

Leo hii akijitokeza Rostam Aziz na kusema hakuitwa na Timu ya Rais nani atabisha? Je, akitoa madai mazito kwamba aliteuliwa na jopo la watu watatu: Mkapa, Ballali na Basil Mramba kupewa fedha za EPA kupitia Kagoda, nani atambishia?
 
Vipi akijitokeza Jitesh Ladwa, mtoto wa mmiliki wa hoteli ya Golden Tulip ya jijini Dar es Salaam na kusema naye alikuwa ameomba fedha za EPA lakini alinyimwa. Nani atambishia?

Je, akienda mbali na kusema alichokuwa ameomba ndicho walimpa Jeetu Patel, mfanyabiashara anayedaiwa kuwa mmoja wa wachotaji wakuu wa fedha za EPA, nani atasita kukubali madai hayo?

Kuwahoji watu wa kada mbalimbali na kutangaza walichosema, ni muhimu kwa kuwa tabia hiyo hujenga imani miongoni mwa wananchi kwamba serikali yao ina roho nyeupe.

Kuna watu wengine muhimu hapa. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuchunguza na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Huyu anasema nini juu ya EPA? Alikuwa wapi wakati wa ukwapuaji huu usiomithilika?

Tatizo hapa ni kwamba Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU amefanywa mmoja wa wajumbe wa Timu ya Rais. Huu ni msiba mkubwa. Taarifa zitapatikanaje? Atahojiwa na nani? Atajihoji?

Kuna aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (TISS) wakati huo. Alikuwa wapi? Anajua nini juu ya ukwapuaji na wakwapuaji?

Usipowahoji watu hawa na ikafahamika kuwa walihojiwa na walichosema ni kipi, basi huwasaidii. Unawaangamizia kwenye uvumi, umbeya mchafu na masimango.

Kuhoji na kutoa taarifa, hakika hakudhalilishi mtu yeyote. Kunalenga kupata ukweli na kupata ushahidi sisisi juu ya kinachochunguzwa. Lakini kuacha kuhoji kunazika ukweli na kufuta hadhi ya wote wanaotajwa mitaani.

Katika suala la EPA kuna orodha ndefu ya watu wa kuhoji ili wasije kujitokeza baadaye na kusema, ama kwa ghadhabu au kwa ulokole, kuwa walishiriki au waliona fulani akishiriki.

Nani atawabishia wakati huo? Si waliokataa kuwahoji ndio watakuwa wameumbua waliowatuma kazi? Fedheha kiasi gani? Si watawala “wataziba nyuso zao kwa viganja kwa aibu kama nyani?” (Shaaban Robert)

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: