Vikosi vya pili klabuni wizi mtupu!

AGIZO la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutaka klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kuwa na vikosi vya pili lilipokelewa kwa furaha kubwa na wadau wa soka nchini.
Kulikuwa na kila sababu kwa kila mpenda soka kufurahia agizo hilo, kutokana na umuhimu wa kuibua vipaji zaidi vitakavyokuja kulisaidia Taifa katika siku zijazo.
Hakika tuliamini kwamba sasa tungepumzika kusikia migogoro sugu kutoka kwa klabu hasa miamba ya soka nchini, Simba na Yanga kugombea wachezaji na hata kufikishana mahakamani ama kusababisha baadhi ya wachezaji kuishia kufungiwa kusakata kabumbu kwa muda.
Lakini tofauti la matarajio ya wengi, agizo hilo sasa limegeuka kuwa ni siasa za michezoni, ama tuite geresha toto au pengine ukipenda kiini macho tu kwani mpaka sasa hakuna klabu yoyote iliyojitokeza na kutangaza mipango ya ku-promote wachezaji wake wa kikosi cha pili yaani 'Timu B'.
Japo milango ya usajili haijafunguliwa rasmi, lakini tumekuwa tukisikia klabu kadhaa, hasa Simba na Yanga zikihaha kusaka wachezaji wa kuwasajili kutoka timu nyingine huku zikiwa kimya kuhusu vikosi vyao vya pili.
Sitaki kuamini kwamba katika wachezaji takribani 20 wa kikosi cha pili, klabu kama ya Simba, Yanga, Mtibwa, Kagera Sugar na nyinginezo kushindwa kabisa kupata hata wachezaji wawili wenye sifa ya 'kutia maguu' katika Ligi Kuu ya Vodacom.
Nashindwa kuelewa kama kweli TFF, iliibuka na hoja hiyo baada ya kufanya utafiti wa kina kupitia kamati yake ya Ufundi ama ni shinikizo kutoka kwa wadhamini wa Ligi Kuu kampuni ya Vodacom!
Kama kweli TFF ingekuwa na nia madhubuti ya kutaka kukuza vipaji vya soka nchini na kama kweli lingekuwa ni wazo safi kutoka kwao bila shinikizo basi naamini kabisa kwa nguvu ile ile shirikisho hilo lingeweka sheria kulinda agizo lake hilo.
Kama ilivyokuwa kwa sheria inayodhibiti idadi ya wachezaji kutoka nje ya nchi, basi nilitarajia TFF ingeweka utaratibu kuhakikisha kila klabu kabla ya kuanza Ligi Kuu iweke bayana idadi ya wachezaji na majina yao waliopandishwa kutoka kikosi cha pili.
Tena ingenoga zaidi hata kuziachia klabu kufukuza wachezaji wake wote na kukipandisha kikosi cha pili kuwa ndio timu rasmi itakayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu huo unaotarajiwa kuanza.
Kwa kufanya hivyo naamini kabisa kwamba lengo la TFF lingetimia na mafanikio yake yangeisadia mno hata timu ya Taifa. Na hivyo ndivyo inavyofanyika kwa nchi ambazo tunayatamani mafanikio yao kama Nigeria, Cameroon, Senegal, Ghana na hata Misri.
Kutoa agizo hilo kali kwa klabu bila kusimamia matunda yake, TFF hakika imechemsha kwa kiasi kikubwa na ndipo hasa hoja yangu inapojengeka kwamba lilikuwa ni wazo lao ama ni shinikizo kutoka kwa wadhamini?
Ikumbukwe kwamba zoezi la kupandisha wachezaji kwenye vikosi vya kwanza sio kitu cha kubahatisha na wala si tukio jipya kwani liliibuliwa tena na marehemu Tambwe Leya wakati akikinoa kikosi cha Yanga miaka ya 1990 baada ya utaratibu huo kuwa umepotea miaka ya nyuma.
Katika kipindi hicho, Tambwe aliweza kuwapa nafasi wachezaji wake wa kikosi cha pili akina Silvatus Ibrahim 'Polisi', Maalim Saleh 'Romario', Anwar Awadh na wengineo ambao waling'ara mno kwenye kikosi cha timu hiyo na kuonekana kama ni wachezaji wakongwe kwenye Ligi.
Nani asiyekumbuka uimara wa Silvatus kwenye ukuta wa Yanga kipindi hicho hadi kupachikwa jina la Polisi? Au nani asiyekumbuka umahiri wa Maalim kwenye ushambuliaji hadi kupewa jina la Romario kwa chenga zake za maudhi uwanjani? Hakika kwangu Tambwe alikuwa Arsene Wenger wa Tanzania.
Hakuishia hapo, Tambwe pia alionyesha mfano ambao makocha wengi wa sasa wanajifanya kuufumbia macho japo wanaukubali kiaina. Kocha huyo alithubutu kutoa nafasi kwa wachezaji kadhaa kutoka mchangani akiwamo Kalimangonga Ongala 'Kally' kutoka Abajalo ya Sinza.
Turudi kwenye mada, kwa mifano hiyo michache naamini kabisa TFF kama baba wa soka Tanzania ina kila nafasi na uwezo wa kuweka utaratibu utakaovibana vilabu kuweza kuwapandisha wachezaji chipukizi kutoka vikosi vya pili ili nao waonyeshe uwezo wao kwenye Ligi Kuu.
Bila shaka yoyote, wachezaji kutoka vikosi vya pili wana nafasi kubwa ya kucheza soka hata nje ya nchi hasa kwa kuzingatia kigezo cha umri mdogo wanaokuwa nao ambao unawapa nafasi ya kudumu kwa kipindi kirefu kwenye 'gemu' huku wakiendelea kufanya majaribio nje ya nchi.
Jambo lisilopingika miongoni mwa wadau wa soka ni hizi kelele za vilabu vikubwa kulumbana kuhusu wachezaji kana kwamba wachezaji ni wachache mno Tanzania. Kila kukicha utasikia Kaseja kutimka Yanga, mara Kaseja ataka Sh. 50 milioni asajili Simba, na kelele nyingine nyingi tu.
Hebu tufikirie kwa makini, hizo Sh. milioni 50 ambazo Simba na Yanga wanataka kuzitupa kwa mchezaji mmoja si zinatosha kabisa kutumika kwenye maandalizi ya kikosi cha pili na kupika wachezaji zaidi ya 100 wazuri kabisa!
Vile vile, kiasi hicho cha pesa, naamini kabisa zinaweza kuwalipa wachezaji chipukizi zaidi ya 50 kwa gharama ya Shilingi milioni moja kila mmoja na klabu kunufaika kwa kiasi kikubwa kuwa na wachezaji hao kwenye timu.
Wakati umefika sasa kwa TFF kuwa wabunifu na makini zaidi kwenye harakati za kuinua soka kama walivyo madhubuti kwenye udhibiti wa mapato kwenye Uwanja wa Taifa.
Ni matarajio yetu kama wadau wa soka kwamba utaratibu huu tutauona kwenye Ligi Kuu inayotarajia kuanza mwezi Agosti mwaka huu. Mungu Ibariki TFF, Mungu Ibariki Tanzania!