Viongozi wa dini wajitazame upya


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

RAIS wangu, tunasoma kuwa ‘waswahili’ walimjaribu Yesu Kristu kwa kumuuliza, “Je, ni halali kulipa kodi?” Kabla hajawajibu akataka wamwonyeshe fedha (dinari) waliyokuwa wakiitumia kulipa kodi.

Walipomwonyesha akawauliza, “Ina picha ya nani?” Wakamjibu “Ya Kaizari” naye akawajibu, “Mpeni Kaizari yaliyo yake Kaizari na mpeni Mungu yaliyo yake Mungu”.

Wiki iliyopita niliandika kuwa Rais wangu ulifanya kosa kiimani kwenda kupiga siasa madhabahuni. Kanisani ni mahali pa sala na kamwe pasitumike na mtu yeyote kufanya siasa. Kwa vile maaskofu walidai uliwadhalilisha ilikupasa uwe mnyofu ukawataka radhi au ukaelezea kwa ufasaha kile ambacho ulitaka kuwaambia.

Rais wangu viongozi wetu wa dini zetu zote na labda na sisi waumini wao tumeonekana kuvutika zaidi na mambo ya kidunia kwa nyakati hizi na hivyo kujikuta tunachanganya mambo ya kiimani na ya kidunia. Mipaka ya Kaizari apewe Kaizari na ya Mungu apewe Mungu viongozi wetu wa dini wameivuruga.

Viongozi wetu wa dini watuambie Kaizari wetu wa sasa ni nani? Kaizari alikuwa mtawala wakati wa Bwana Yesu. Sijui ndugu zetu Waislamu kama wanaweza kutuambia iwapo Mtume Mohammed (S.A.W) katika siku zake kama aliwahi kumtukuza Kaizari aliyekuwapo wakati wake.

Lakini uhusiano wa utawala wa Kaizari na Kristu Yesu ulikuwa wa upanga. Kama Kaizari alivyomwona Bwana Yesu kuwa tishio kwa utawala wake, ndivyo hivyo makaizari wote wanavyowaona viongozi wa dini kuwa tishio kwa utawala wao. Hapa kwetu hakuna tofauti.

Kaizari ataimba udini hata kama haupo! Alipoibuka mtu mmoja na kusema Jakaya Kikwete, ni chaguo la Mungu, viongozi wetu wa dini hawakujitokeza kuukana wehu ule. Waliogopa!

Maaskofu wengine waliogopa kuwa iwapo wataikana kauli ile wangefikiriwa kuwa wanaikana kwa sababu Kikwete ni Muislamu.

Tumemsikia Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitetea ulanguzi na unyang’anyi wanaofanyiwa Watanzania kwenye kodi zao kupitia posho. Kama hawa wanaofanya ulanguzi huu na unyang’anyi huu hawataacha na kutubu, hawastahili heshima yoyote nchini.

Wanaowalangua wananchi maskini walipa kodi kwa kuwachukulia Sh. 2,500 kwa lita moja ya mafuta ya magari yao hawapaswi kuingia katika nyumba za ibada! Imeandikwa “Nyumba ya baba yangu siyo pango la walanguzi na wanyang’anyi. Viongozi wa dini zetu wengi wamekosa ujasiri wa kuwakemea viongozi wa serikali na wanasiasa wanapofanya dhambi kama hizi.

Kama viongozi wa dini wananyamaza nani atawasemea waumini wao?  Nani ametengeneza Bunge la wananchi kuwa Bunge la kifisadi?

Rais wangu, mauaji yanayofanywa na polisi ina maana yanafanywa na serikali. Amri ni ya Kaizari. Tungali tunalia na mauaji ya kinyama yaliyofanywa na serikali ya Kaizari kwa wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge na dereva teksi mmoja wa mkoa wa Dar es Salaam.

Tungali tunalia pia kwa mauaji ya kinyama yaliyofanywa na serikali kwa watu watatu mkoani Arusha wakati wa maandamano ya amani kabisa ya CHADEMA!

Tungali tunazililia roho za ndugu zetu wa Nyamongo waliouawa na serikali walipoitaka raslimali yao waliyowekewa na Mwenyezi Mungu! Mbarali kuna mauaji!

Je, ni kweli tunatawala kwa mtutu wa bunduki?  Kama viongozi wa dini hawatasimama kuikemea serikali kwa mauaji haya nani atawakinga wananchi na risasi za Kaizari?

Rais wangu, nilimsikia Baba Askofu Valentine Mokiwa akisema anangoja kukamatwa. Nikajiuliza serikali imeingiaje kanisani? Baba Askofu Mokiwa alipokuwa anamsimika askofu mpya mkoani Arusha alikuwa anafanya kazi yake ya kitume, Mkuu wa Mkoa ulimwita wa nini?

Mmeiingiza wenyewe serikali ndani ya kanisa. Mwanasiasa kuwa mgeni rasmi katika kazi za kichungaji anahusika vipi? Maaskofu mnayataka wenyewe. Tumefikia mahali hata Mary Chatanda tu anawakashfu maaskofu wetu akitaka wavue majoho yao! Kaizari anaona sawa tu, anafurahi!

Rais wangu, kama Baba Mokiwa aliamini kuwa alikuwa anafanya kazi ya Mungu kwa mapenzi ya Mungu, basi angemsimika uaskofu na angempangia jimbo. Kushindwa kumpa jimbo kwa kuogopa amri ya mahakama ni kukiri upungufu katika imani.

Kazi ya Mungu haiwezi kufanywa nusu nusu. Lazima ifanywe katika utimilifu hata kama itabidi kutundikwa katika mti wa Msalaba kama Bwana wetu Yesu Kristu. Viongozi wetu wengi wa sasa imani  yao ni haba.

Niliwahi kushuhudia tukio kubwa la kiimani katika maisha yangu, lililoonyesha jinsi viongozi wa dini zamani walivyokuwa na imani kubwa.

Mwaka 1960, hakimu wa  mahakama ya mwanzo Kamsamba Ndugu Sichalwe, alitoa hukumu kuvunja ndoa. Mumemtu akadai kuwa hakimu hana uwezo wa  kuivunja ndoa yake kwa sababu ilifungwa kanisani.  Hakimu akasema  hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Akatoa amri padri aitwe mahakamani aivunje ile ndoa. Alipofika mahakamani padri alikataa kuivunja ndoa kwa maelezo kwamba ndoa iliyofungwa kanisani haina talaka. Hakimu akamwambia ana mamlaka ya kumtia ndani kama hataivunja ndoa ile mahakamani. Padri akajibu, “Siwezi kuzuia mamlaka yako lakini elewa kuwa naitii mamlaka ya aliye juu kwa kuwa imeandikwa, alichoungansha Mungu mwanadamu asikitenganishe! Wewe huna mamlaka ya kuivunja ndoa iliyofungwa kanisani”.

Akatoka nje ya mahakama, akafungua kitabu chake cha sala akawa anasoma huku akielekea misheni kwake. Mapadri wa zamani walitumia muda wao mwingi katika kusali. Hakimu akasema kwa mamlaka ya mahakama ile ndoa imevunjwa.

Rais wangu, hakimu Sichalwe alikuwa ndugu yake mama. Kwa kuwa hakuwa anakaa Kamsamba kila alipokuja alifikia kwetu akilala juu ya kitanda chetu na sisi tukilala chini kwenye mkeka.

Saa tisa alasiri Hakimu aliletwa nyumbani akiwa amebebwa machela. Alikuwa akilalamika mbavu zinamuuma. Alivuja jasho jingi na kutoka povu mdomoni. Alipokata sauti wazee wa baraza walimkimbilia Padri kumwombea sakramenti ya mwisho.

Padri aliwaambia wamwambie kuwa hakumkosea yeye  bali yule aliyempeleka. Atubu na kumwomba yeye amsamehe.

Walipofanya alivyowaelekeza hali ya hakimu ilirudi kuwa kawaida kabisa. Nilikuwa kijana mdogo lakini nalikumbuka tukio lile kama vile lilitokea jana. Nataka kuonyesha jinsi imani ya viongozi wetu wa dini zamani ilivyokuwa kubwa.

Viongozi wa dini zetu zote wa sasa wanahitaji kujitazama upya. Siyo wote siku hizi ni wa ukweli. Na wengine wamechakachuliwa na siasa na utandawazi kwa kutamani vyeo na mambo ya  kidunia. Tuwaache viongozi wa kisiasa wabaki katika siasa.

Viongozi wa dini shikamaneni na dini zenu. Anayetaka kufanya  dua zake msikitini awe ni yule aliyesilimu, vivyo hivyo anayetaka kwenda  kanisani kusali awe ni yule aliyebatizwa.

0713334239, ngowe2006@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: