Viongozi wasipobadilika tutabaki masikini milele


Sophia Yamola's picture

Na Sophia Yamola - Imechapwa 18 May 2011

Printer-friendly version

ZIPO sababu za Tanzania kutambuliwa kama miongoni mwa nchi masikini sana duniani.

Inashangaza kwamba rais Jakaya Kikwete hajaelewa ukweli huu. Karibuni, waziri mkuu, Mizengo Pinda naye amesema haelewi hasa sababu ya Tanzania kuwa nchi masikini.

Kabla ya mtu kujua sababu ya kuwa masikini, anapaswa kutazama nini kinachomweka mwingine kuwa tajiri na mwingine masikini.

Nchi tajiri zina viongozi wanaotambua wajibu wao. Wanajua ni mambo gani wanapaswa kuyafanya kuinua uchumi wa nchi zao na kustawisha hali za watu wao.

Katika nchi kama hizo, viongozi wanajipa muda wa kufikiri kabla ya kuamua. Wanapanga na kuchagua lipi ni jema kwa watu wao walifanye, na lipi halina maslahi waliache.

Viongozi hao wanajenga dhamira ya kuendeleza nchi wanazoongoza. Wanatumia vizuri raslimali haba au nyingi zilizo katika nchi hizo kujenga uchumi na mtandao wa huduma za jamii.

Hawako tayari kutumia vibaya madaraka yao kuumiza wananchi. Wanajali shida za wananchi na kujitahidi kuzipatia ufumbuzi.

Hayo ni mambo ya kuzingatiwa na viongozi wa nchi masikini kama Tanzania. Je, wanatambua wajibu wao katika kutumikia wananchi wanaowaongoza?

Je wanatumia vema raslimali zilizopo katika nchi zao kujenga uchumi na mtandao wa kuhudumia jamii? Wanajali watu wanaowaongoza? Wanakumbuka shida zao?

Katika matumizi ya fedha za serikali zinazotokana na kodi, wanatumia kwa uadilifu? Wanaziba mianya inayovujisha mapato ya serikali? Wao wenyewe wanapinga kwa vitendo matumizi ya anasa?

Kuna upande mwingine. Hivi viongozi wa nchi masikini kama Tanzania wanakubali kutenda shughuli za serikali kwa misingi ya sheria na uwazi?

Kwa viongozi wa serikali katika nchi tajiri au zilizoendelea, anayetuhumiwa kufanya ufisadi hata wa kiwango kidogo huchukuliwa sawa na yule aliyefanya ufisadi wa mamilioni ya shilingi.

Maana yake mbele ya sheria, watu wote ni sawa, bila ya kujali mtu ana hadhi gani kiuongozi au katika shughuli zake ndani ya jamii.

Hapa nchini petu hali ikoje? Ni vipi viongozi wetu wanayatazama hayo? Je, wanaruhusu sheria kufuata mkondo wake panapotokea tatizo? Wanajali dhana ya uwazi katika kufanya kazi za serikali?

Kwa mfano, ni vipi viongozi wetu wanateuliwa kushika nyadhifa katika serikali na taasisi zake. Hili wenzetu hulifanya kwa vigezo maalum na inapobainika kuna uteuzi uliofanywa kwa misingi ya upendeleo na kujuana kindugu, mhusika anachukuliwa hatua.

Tanzania viongozi wanateuliwa kwa sifa au kwa misingi hiyo ya kujuana na kupendeleana? Sisi tunao viongozi waliohusishwa na ufisadi katika matukio tofauti, lakini wanaendelea na nafasi zao serikalini, tunapata picha gani?

Katika nchi za Skandinavia – Denmark, Sweden na Norway – katiba zinaweka vigezo vya namna viongozi wa taasisi mbalimbali za umma wanavyopaswa kuteuliwa.

Nchini Sweden, kiongozi mtendaji ambaye ni waziri mkuu haruhusiwi kuteua ndugu yake au mtu aliyewahi kusoma naye. Inapotokea ipo haja ya mtu mwenye sifa zinazotakiwa ni ndugu au walisoma pamoja na mteuzi, kuna vigezo maalum.

Hali ikoje nchini petu? Hakuna viongozi walioteuliwa kutoka familia au marafiki wa mteuzi? Hakuna viongozi walioteuliwa kwa misingi ya kujuana?

Uwajibikaji ni nguzo muhimu katika utumishi wa umma. Katika nchi zilizo tajiri, nguzo hii hutumika kama dhana muhimu kwa kila kiongozi, kwa kila mtumishi wa umma.

Ofisa yeyote wa umma anayeshindwa kuwajibika anachukuliwa hatua zifaazo bila ya kucheleweshwa. Je, nchini petu hatua zinachukuliwa? Kwa wakati unaofaa?

Iwapo mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kila mwaka anapiga kelele kulalamikia ukiukaji wa kanuni za matumizi ya fedha za serikali lakini bado viongozi wanaendelea kutotii kanuni tusemeje?

Hakuna uwajibikaji. Lakini wanaoshindwa kuwajibika wanachukuliwa hatua? Jibu rahisi ni kuwa hawachukuliwi bali hulindwa; ndio maana kasoro za matumizi zinaendelea kutokea mwaka hadi mwaka.

CAG huwa anahimiza kitu kinachoitwa value for money popote pale zinapotumika fedha za serikali. Je, ndani ya serikali yetu hili linazingatiwa? Ofisa anapopewa jukumu la kusimamia mradi wa maendeleo anatambua dhana hii?

Jibu rahisi ni kwamba wengi hawawajibiki kwa dhana hii ndio maana wananchi wamekuwa wakisikia na kushuhudia madaraja yakiwa na nyufa hata kabla ya kukabidhiwa. Juzi tu Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli alikataa kukabidhiwa barabara ya Kilwa alipogundua haikufikia kiwango kinachotakiwa.

Mawaziri wangapi wanatambua hilo na kuchukua hatua kama hiyo inapotokea katika wizara zao?

Kwenye eneo la matumizi pana tatizo kubwa. Serikali imekuwa ikilaumiwa na viongozi wa upinzani na wahisani kwamba inatumia vibaya fedha za umma. Inajulikana yapo matanuzi ya kupindukia mpaka serikalini.

Kipindi sasa, waziri mkuu Mizengo Pinda amekuwa akikemea utamaduni huu na kutaka uangalifu utumike wakati serikali inapotaka kutumia fedha kwa jambo lolote lile.

Lakini wakati alipokabidhiwa gari la bei mbaya kwa ajili ya matumizi yake, baada ya kulikataa, aliagiza apewe ofisa mwingine. Utawala bora hautaki hivyo.

Kilichotakiwa ni Pinda kuagiza gari hilo la ghali isivyo kawaida lipigwe mnada ili fedha zinazopatikana zitumike kununua gari la bei afadhali na zinazobaki zitumike kwa shughuli nyingine za manufaa kwa wananchi.

Mpaka leo bado serikali imeshindwa kuwadhibiti kinidhamu maofisa waandamizi waliohusika na kashfa ya mkataba wa Richmond uliolenga kufua umeme wakati wa ukame. Je, huo ndio uwajibikaji?

Hali iko hivyohivyo kwa wafanyabiashara waliotuhumiwa kuiba kisanii fedha zilizohifadhiwa katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Ni sasa tunamsikia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wa Serikali, Eliezer Feleshi, akitoa kauli – miaka kadhaa tangu ugunduzi wa ufisadi huo ulipofanyika – ya kutaka mwenye ushahidi wa ufisadi huo apeleke kwake ili achukue hatua.

Hebu tujiulize, ni kweli DPP hajapata ushahidi wa tukio ambalo ni serikali yenyewe iliyotoa taarifa ya kugundulika kwa ufisadi huo? Unaona dhahiri hapa ni uwajibikaji wa kisanii.

Kwa sababu hakuna uwajibikaji na hakuna nidhamu katika utumishi wa umma, wafanyabiashara mafisadi wamefanikiwa kupenya ndani ya mfumo wa uongozi baadhi wakilaghai watumishi kwa hongo za viwango vikubwa na kufanikisha matakwa yao.

Matokeo yake ni elimu duni, maji haba, afya duni, kilimo cha jembe la mkono, mfumo mbaya wa kununua mazao ya wakulima, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, udanganyifu.

Wajawazito hawapati huduma nzuri, wakijifungua salama bado wanakabiliwa na hatari ya kifo pamoja na vichanga vyao. Tanzania itabaki masikini milele iwapo viongozi wa umma hawatabadilika. Na hayo ndiyo mambo yanayochangia isiendelee.

0715 221208
0
No votes yet