Visa, vituko na filamu ya ziara ya Al-Adawi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 02 March 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
January Makamba

WATUNZI wa filamu ni watu makini sana. Hupanga visa vikasisimua; huteua wahusika kulingana na nafasi zao; na huchagua maeneo ya kuigizia ili kusawiri kinachoelezewa na filamu yenyewe.

Wapo wahusika wanaoigiza kama majambazi, malaya, polisi, mabondia, walevi, waasi au wamiliki wa biashara fulani. Hata hivyo, hata yasisimue au yatie simanzi vipi, matukio yote katika filamu huwa si halisi. Ni usanii tu.

Katika sanaa hii, wenye kazi kubwa zaidi huwa ni waongozaji na wapigapicha za matukio. Ndio huelekeza wahusika cha kusema na wakati gani, wakaeje – wakae, wasimame au walale? Huelekezwa hata namna ya kufanya penzi au kuonyesha hisia kali.

Waongozaji wa filamu ndio hasa wanaojua filamu husika itamalizikaje.

Yameshuhudiwa haya katika filamu ya karibuni kabisa iliyoandaliwa nchini kwa ajili ya “Ziara ya Brigedia Jenerali mstaafu Sulaiman Mohammed Yahya Al-Adawi.”

Waongozaji wa filamu hiyo walifanya kazi yao kwa umakini. Wao pekee ndio wanaojua kwanini ilipaswa kuandaliwa kipindi hiki cha sasa.

Ilikuwa hivi: Al-Adawi alikuja kisanii; alidai alialikwa na serikali, mara akasema alialikwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO); akaonana na wahariri maalum; akaenda mitamboni; na akaondoka nchini huku watu wakibaki na maswali yasiyokuwa na majibu.

Kwanini?

Wakati muhimu wa kuja nchini kuangalia mazingira na usalama wa uwekezaji katika ‘miradi’ yake, mtu huyo anayedaiwa kumiliki kampuni ya Dowans, hakuonekana.

Hata wakati wa kurithi mkataba wa uzalishaji umeme kutoka iliyoitwa kampuni ya Richmond, hakunyanyua mguu kutoka Oman.

Aidha, baada ya kampuni hiyo kushukiwa na kuhusishwa na ufisadi, na mkataba wake wa kufua umeme ukasitishwa kwa vile iliurithi kibatili, ‘tajiri’ huyo hakutia mguu wake nchini.

Mambo yote, hata ile hatua ya Dowans kushitaki TANESCO kwenye mahakama ya kimataifa ya usuluhishi migogoro ya kibiashara (ICC), yalifanywa na Rostam Aziz, mfanyabiashara na mwanasiasa anayemiliki mamlaka ya kisheria- power of attorney- ya kusimamia kampuni hiyo.

Kilicho kibaya zaidi ni kwamba Al-Adawi hakuwahi hata kuja Tanzania kutazama ustawi wa mradi wenyewe.

Lakini katikati ya kizungumkuti cha malipo ya Sh. 94 bilioni ambazo Dowans inaidai TANESCO kutokana na mkataba wake kukatishwa, kukaandaliwa filamu ambayo sasa imethibitisha ililenga kumuonesha Al-Adawi alivyo steringi (muongozaji) wa kushinikiza serikali ilipe tuzo hiyo.

Pia waongozaji walijisahau na kudhani mvuto wa visa au matukio ndiyo hali halisi ya filamu; wakafikiri filamu hiyo ilitosha kumwondoa Rostam kwenye tuhma za kutajwa kuwa ndiye ‘Mr Dowans’ na mipango yote ilifanyika ikulu.

Ndiyo maana, waongozaji walitaka Al-Adawi, yuleyule aliyewahi kukana kumiliki Dowans, afike ikulu ya Tanzania, akaonane na Rais Jakaya Kikwete ili amjue na ‘wamalizane’.

Kwa utuki tu, Rais Kikwete alikwenda zake Mauritania kushughulikia uluhishi wa mgogoro wa Ivory Coast. Leo, inaoneshwa kuwa hawakuonana maana rais aliporejea nchini, Al-Adawi ambaye alipigwa picha kisanii vilevile, - kwa kuviziwa tu ikidaiwa hakutaka – alishaondoka.

Serikali ilijua ziara ya mtu huyu? Ilijiandaa kuzungumza naye? Je, hiyo ingeondoa ukweli kwamba Dowans ilirithi mkataba feki wa Richmond? Je, kujitambulisha kwake kungehalalisha ukiukwaji wa sheria uliofanywa na serikali kurithisha mkataba bila kupitia mchakato wa zabuni? Na bila ya TANESCO, wahusika wakuu wa mkataba, kuidhinisha?

Vioja

Kiasili, filamu hazikosi vioja. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba ndiye mtu pekee aliyeonekana kushupalia kuwa Al-Adawi alionana na viongozi wa TANESCO, waziri na Makamu wa Rais, Mohammed Gharib Bilal. Lakini waliotembelewa walikanusha.

Makamba ndiye mtu pekee aliyeshupalia kuwa Al-Adawi ameiandikia serikali kueleza kusudio la “kampuni yake” kusamehe sehemu au kufuta tuzo yote.

Mtu wa pili kuzungumzia suala hilo ni Mkurugenzi wa Fedha wa Dowans, Stanley Munai. Kwanini Al-Adawi mwenyewe hakueleza hili kwa uwazi?

Ili kunogesha filamu, TANESCO na serikali wamejiweka kando wakidai hawaijui ziara hiyo. Wanatilia shaka kuwa ni filamu inayotisha? Wanahofu wameingizwa mjini?

Filamu huigizwa na wasanii, na hubuni visa, matukio au mikasa kwa malengo maalum na watu wenyewe huachiwa kazi ya kubaini ujumbe. Kila kisa huwa na ujumbe fulani na kuna matukio yenye maudhui mchanganyiko.

Kwa tafsiri yangu, inayoweza kutofautiana na yako na ya mwenzako, filamu ya ziara ya Al-Adawi imeonyesha ukomo wa fikra kwa viongozi wetu. Wamebanwa katikati na ufisadi kiasi kwamba hawawezi kujinasua.

Ndiyo maana hata kikao cha baraza la mawaziri alichokiongoza Rais Kikwete kilimalizika bila ya kuamuliwa yanunuliwe majenereta au ikodi. Kikao hakikuamua serikali ikodi au inunue majenereta ya Dowans.

Kwa makusudi uliachwa mwanya ili yale yaliyolengwa katika filamu yatimie. Hatua ya viongozi wakuu wa wizara ya nishati na madini na wale wa TANESCO kukwepa kueleza kwa ufasaha masuala haya muhimu ni uthibitisho mkubwa.

Makamba, huyu mtoto wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndiye steringi hasa wa filamu hii. Ndiyo, tunaona alivyolivalia njuga suala hili. Haoni kama serikali ina maisha bila ya Dowans. Serikali na watu wamesimama kufikiri mambo mengine isipokuwa Dowans.

Filamu hii ilianza mwaka 2006 – pale serikali ilipojadili Richmond, mwaka 2007 Richmond/Dowans, 2008 Dowans, 2009 Dowans, 2010 Dowans. Na mwaka 2011 bado tunaletewa filamu ya Dowans? Haikubaliki.

Bungeni

Serikali ilijua, kama hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, kuhusu sakata ya kampuni ya Dowans ingepitishwa na kujadiliwa bungeni, ingeharibu maandalizi ya filamu ya “Ziara ya Al-Adawi.”

Ikafanya ushawishi, Spika wa Bunge, Anna Makinda, akaifutika kwa kisingizio kuwa suala hilo liko mahakamani, hivyo haliwezi kujadiliwa bungeni. Kafulila akafungwa mdomo kutumia chombo halali kujadili Dowans.

Nje ya Bunge serikali na kamati ya nishati na madini, ambayo kazi yake ni kutoa ushauri tu kuhusiana na masuala ya madini na nishati, wamebeba mafaili ya Dowans; wakilala, Dowans; wakinywa chai, Dowans; na wakikohoa, Dowans.

Kila kikao huingiza Dowans. Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) wamejitosa kutetea Dowans. Wafanyacho CTI ni kumtetea mfanyabiashara mwenzao, maana katika kipindi ambacho mitambo ya IPTL iliyoko Tegeta, haina matatizo yoyote, wangeshupalia ipewe mafuta ya kutosha iwake kwa ukamilifu na kuzalisha umeme. Wanalilia Dowans.

Je, kubeba Dowans ndio kuondoa ukame na giza? Wanahaha kuokoa maslahi ya Mr Dowans yupi? Rostam, mwenye power of attorney tangu 28 Novemba 2005? Au Al-Adawi aliyewahi kukana hamiliki Dowans?

Kwanini serikali ‘inashangilia’ mgogoro wa kuokoa kampuni yenye madeni? Inapuuzaje kilio cha wananchi cha kutaka ipunguze mzigo wa gharama za maisha?

Si bure. Watetezi wote wa Dowans, serikalini na bungeni, na wanasheria, inaonyesha wanamaslahi na Dowans. Na hii ndiyo gharama ya serikali iliyoingia madarakani kifisadi: haiwezi kukemea mfumo mchafu ulioizaa bali itautetea ikiwa mfukoni mwa mafisadi.

0
Your rating: None Average: 4.7 (10 votes)
Soma zaidi kuhusu: