Vita vya makundi CCM vyamwandama Kikwete

- Mwakyembe amkomalia Chiligati
- Mkuchika kuvaana na Makamba
VITA vya makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, sasa siyo siri tena. Sasa vinaelekezwa moja kwa moja kwa Rais Jakaya Kikwete, MwanaHALISI limeelezwa.
Taarifa kutoka serikalini na CCM zinasema sasa hakuna uwezekano tena wa makundi yanayopingana kukaa meza moja bila kuparurana.
Katika hali ambayo haikutarajiwa, mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati “alimwaga ugali hadharani.”
Chiligati, akizungumza katika mkutano wa Kamati ya Kanuni za Bunge, uliofanyika ofisi za Bunge mjini Dar es Salaam na kushirikisha wenyeviti na makamu wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, alisema hafurahishwi na “malumbano yanayofanyika baina ya viongozi waandamizi wa CCM na wabunge.”
Akizungumza kwa ukali, Chiligati alisema hatua hiyo ya wabunge wa chama chake kutoleana macho inaleta sifa mbaya kwa Bunge na kwa jamii.
Alitishia kutumia vikao vya kamati za wabunge (party caucus) kudhibiti wale “wanaojifanya kimbelembele.”
“Tutalazimika kutumia vikao vya chama bungeni kuulizana kuhusu haya,” alisema Chiligati na kuamsha mguno miongoni mwa wabunge waliokuwepo.
Kauli ya Chiligati ilijibiwa papohapo na mbunge wa Kyela na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk. Harrison Mwakyembe, kwamba Chiligati ameibuka kutokana na kile alichoita, “Gwiji limeguswa.”
Dk. Mwakyembe alisema, “Viongozi wetu wanashtuka pale gwiji moja ndani ya CCM linapoguswa. Lakini viongozi haohao wanakuwa kimya wakati gwiji hilo linaendesha mtandao wa magazeti yanayomsulubu Spika (Samwel Sitta) kila siku.”
Alisema viongozi wanakaa kimya pia wakati gwiji hilo linamwandama Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge kuhusu mkataba wa Richmond, wajumbe wa Kamati na baadhi ya wabunge wengine waliosimama kidete kupambana na ufisadi.”
Wajumbe wa kikao, huku wakitazamana, walinong’onezana na minong’ono kusikika kuwa gwiji lililokuwa likitajwa lilikuwa Rostam Aziz mwenye msululu wa magazeti na ambaye ameyatumia hivi karibuni kupambana na akina Mwakyembe.
Mwakyembe alisema anasubiri kwa hamu vikao hivyo ndani ya chama. “Tutakutana huko. Tuko tayari kujibu mapigo na kusema kila tulichonacho,” alinukuliwa akisema.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe hakutaja gwiji hilo kwa jina.
Mkutano wa Kamati ya Kanuni ulishirikisha wenyeviti wote wa Kamati za Bunge wakiwamo wale wanaotoka upinzani, jambo ambalo limedhihirisha kuwa Chiligati alikosa uvumilivu kwa kuyasema hayo mbele ya wapinzani wa chama chake.
Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo, ni Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Hamad Rashid Mohammed (Wawi-CUF), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Bunge, Philip Marmo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Mary Nagu, Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Emmanuel Nchimbi na Profesa Mark Mwandosya.
Mkutano huo ulifanyika chini ya uenyekiti wa Naibu Spika, Anna Makinda.
Katika siku za hivi karibuni, Dk. Mwakyembe amenukuliwa akimtuhumu mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kwa kusema ameanzisha magazeti kushambulia viongozi wenzake katika chama na serikali.
Msuguano kati ya Rostam na Dk. Mwakyembe na wenzake unadaiwa kuchochewa na hatua ya Kamati ya Nishati na Madini kushinikiza serikali kutonunua mitambo ya Dowans inayotajwa kumilikiwa na Rostam na kampuni zao kugombea eneo la kuwekeza mradi wa umeme wa upepo mkoani Singida.
Huku makundi hayo yakiendelea kutafunana, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amemfuta kazi Katibu Msaidizi Wilaya ya Hanang, Daniel ole Porokwa, siku 40 baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo.
Porokwa, ambaye kabla ya uteuzi huo aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UV-CCM) Wilaya ya Hanang, alijulishwa kuteuliwa kuwa katibu msaidizi wa CCM wilaya kwa barua rasmi ya 30 Januari 2009 yenye Kumb. Na. CMM/PF. 36236/2, aliyoandika Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, George Mkuchika.
Kwa uteuzi huo, Porokwa alikuwa moja kwa moja ndiye mhasibu wa CCM wilaya, kwa mujibu wa barua hiyo iliyotumwa pia kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha.
Taarifa zinasema katibu wa CCM mkoani Manyara, Katherine Ndahani, alipokea ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kutoka kwa Makamba ukielekeza kufutwa kazi kwa Parokwa.
Ndahami alithibitisha Parokwa kuajiliwa, lakini aligoma kuzungumzia kuondolewa kwake kazini, akidai kuwa msemaji katika hilo ni Makamba. “Muulize katibu mkuu wetu (Makamba) yeye ndiyo msemaji wa chama,” alisema.
Lakini katika hatua iliyoshangaza wengi, Mkuchika alifuta uteuzi wa Porokwa bila kueleza sababu yoyote. Taarifa za ndani ya CCM mkoani Arusha na Ofisi ndogo Dar es Salaam, zimesema hilo siyo tukio la kawaida.
Uteuzi wa Porokwa ulifutwa kwa barua ya 11 Machi 2009, yenye Kumb. Na. CMM/PF. 36236/3 iliyosainiwa na A.S. Eriyo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Bara, ambayo imenakiliwa kwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na Katibu wa NEC, Idara ya Uchumi na Fedha, Makao Makuu, Dodoma.
“Nimeelekezwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi nikujulishe kwamba uteuzi huo sasa umefutwa mpaka hapo utakapojulishwa vinginevyo,” imesema barua hiyo.
Taarifa zilizofikia MwanaHALISI kuhusu hatua ya kufutwa ghafla kwa uteuzi wa Porokwa, zinasema maelekezo yalitokana na ushawishi wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ambaye amedaiwa kuwasiliana na Mkuchika na kumwambia kama angemshirikisha, basi (Mkuchika) asingemteua Porokwa.
“Baada ya Mkuchika kugoma kushawishika, inaonekana juhudi zilifanywa kumtumia Katibu Mkuu (Makamba) ambako yalitoka maelekezo ya kufutwa kwa uteuzi wa Porokwa,” kimesema chanzo cha habari.
Hatua ya kumruka Mkuchika, taarifa zimeeleza, imezaa kutoelewana kati yake na Makamba na kwamba huenda ikasababisha mazingira magumu ya kazi kwa viongozi hao wawili.
Porokwa na Lowassa walipata kuwa katika mvutano. Kada huyo kijana alitaka kugombea ubunge wa Monduli lakini akishinikizwa na Lowassa kumuachia kwa maelezo kwamba wangempatia nafasi nyingine. Hata hivyo, ahadi hiyo haikutekelezwa.
Kutokana na hali hiyo, taarifa zinasema Porokwa amejiandaa kukabiliana na Lowassa katika uchaguzi ujao jimboni Monduli.