Wabaya wa Sitta wafichuka

- Maandalizi kumg'oa ya muda mrefu
- Kikwete alinong'onezwa mapema
NJAMA za kumng'oa Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta ziliratibiwa na baadhi ya viongozi wa juu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), MwanaHALISI limedokezwa.
Taarifa zimeeleza kwamba maandalizi ya mashambulizi ya wajumbe wa vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), yamekuwa yakiandaliwa kwa muda mrefu sasa.
Lakini kilele cha maandalizi kilikuwa pale Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alipotua uwanja wa ndege wa Dodoma akitokea Dar es Salaam, tayari kwa vikao hivyo, wiki mbili zilizopita.
Imeelezwa kwamba mara baada ya rais kutoa mguu wa mwisho kwenye ndege, Katibu Mkuu wa CCM Yusuph Makamba alimweleza, “Mwenyekiti, safari hii uwaache wajumbe waseme.”
Taarifa zinasema hata kabla Kikwete hajatafakari alichokuwa ameambiwa, Makamba aliongeza, tena karibu na sikio lake, “…Mwenyekiti, tafadhali waachie wajumbe wazungumze.”
Mtoa taarifa anaeleza kuwa baada ya mfululizo wa “maombi” ya Makamba kutaka Kikwete aachie wajumbe kusema walichonacho, Rais Kikwete alimgeukia na kuuliza, “Una maana gani?”
Ndipo Makamba alinukuliwa akipasua, “Wajumbe wamenituma nikueleze mwenyekiti, kwamba wanataka wazungumze. Wana jambo lao, waache waseme tena watasema sana….”
Hiyo ndiyo siri ya mlolongo wa wajumbe, mmoja baada ya mwingine, waliomtuhumu Sitta kutumia bunge kudhoofisha chama na serikali na kutaka afukuzwe uanachama.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, wajumbe kutoka Zanzibar waliandaliwa mapema pia. Ujumbe wa watu wawili kutoka Dar es Salaam (majina tunayo) ulitumwa Visiwani kuandaa wajumbe kwa hoja za kumsulubu Sitta.
Mmoja wa wajumbe wa NEC ambaye hakuongea kwenye kikao hicho aliliambia MwanaHALISI, kwamba mpango huo ulikuwepo kwani hata rais Kikwete alionekana kuuthibitisha wakati wa kuanza vikao hivyo.
Kama asiyejua kuweka siri, wakati kikao cha NEC kinaanza, Kikwete alinukuliwa akisema, “Tumekuja hapa, nimesikia watu wamenoa mapanga. Wanataka kufyeka watu. Haya…”
Lakini katika hatua nyingine, mwishoni mwa kikao cha NEC, Rais Kikwete ambaye aliruhusu milipuko dhidi ya Sitta, alinukuliwa akisema, “…Nadhani wametusikia; tuwasubiri Novemba. Tutajua kama wametuelewa au hapana.”
Taarifa zimeeleza kuwa rais alisisitiza kauli yake kwa kusema, “…Wenzetu ninyi (Bunge) mnapokutana, hali ya hewa inachafuka. Mkimaliza inatubidi tupite tena upya ili kuweka mambo sawa.”
Akielekeza hoja hiyo kwa mjumbe, rais amenukuliwa akisema, “…Dk. Mwakyembe (Harrison Mwakyembe), kwa nini mnatafuta umaarufu binafsi badala ya umaarufu wa chama?”
Awali Dk. Mwakyembe akiunga mkono kazi anayofanya spika Sitta, alisema mgogoro ulioko ndani ya chana unatokana na makundi mawili – moja alinalopinga ufisadi na jingine linalounga mkono ufisadi.
“Ugomvi huu utaisha pale ufisadi utakaposhindwa. Zaidi ya hapo hakuna kinachoweza kumaliza ugomvi wetu,” alisema.
Wiki mbili zilizopita, NEC ilitoa azimio la kutaka hoja kuhusu ufisadi zisijadiliwe bungeni bali kwenye vikao vya chama ili kuepusha kunufaisha upinzani na kudhoofisha chama na serikali (soma makala uk.5).
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati aliwaambia waandishi wa habari baada ya kikao cha NEC, “Tumesema inatosha. Hapa tulipofika tusiendelee mbele. Wanaoropoka ovyo ni walevi na tumeona kuna kundi dogo ambalo linajiona kama ni wateule wa kuzungumzia ufisadi.”
Kauli hii ya CCM ililenga wabunge jasiri ambao wamekuwa wakiikosoa serikali, miswada yake na kutaka watuhumiwa wa ufisadi kuchukuliwa hatua.
Alipopewa nafasi ya kuzungumza, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, William Kusila alinukuliwa akisema, “…Wanachokifanya wabunge kwa upande wa serikali ni kama uhaini…”
Miongoni mwa waliopata fursa ya kumshindilia Sitta alikuwa John Guninita, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam.
Amenukuliwa na mtoa habari wetu akisema, “Ukimwachia mnyama aliyejeruhiwa, atakujeruhi wewe. Mwenyekiti, huyu mtu tumemwonya mara mbili, hajasikia. Tukimwacha leo atakuja kukung’oa wewe. Tumalizane naye hapahapa.”
Baada ya wajumbe zaidi ya 40 kumtuhumu, kumtishia na kumkejeli, mwishoni Sitta alikiambia kikao, “Nimewasikia. Mimi ni mtu mzima. Tuiachie kazi kamati iliyoundwa.”
Sitta amethibitishia MwanaHALISI kuwa taarifa za awali kwamba aliomba radhi hazikuwa sahihi. Ameuliza, “Niombe radhi kwa kitu gani?”
Taarifa zinaeleza kuwa rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ndiye alisema katika kikao hicho kuwa “kufanya kosa si kosa, bali kosa ni kurudia kosa.”
Sitta aliwaambia wananchi kwenye tamasha la kwaya la wakriso katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora mwishoni mwa wiki, “Uongo sasa umekuwa biashara. Watu wanatumia uongo kuficha mambo. Nchi haiwezi kubaki katika uongo kwa kuwa uongo ni laana.”
Alisema kumeibuka tabia ya waovu wanaosambaza “uongo uliopakwa asali; hugeuza uongo huo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo. Siwezi kukubaliana nao kwa sababu ni waovu," amesisitiza Sitta akiwalenga waliotaka avuliwe uanachama wa CCM.
Alisema, “Ninajua kuwa Mungu peke yake ndiye anayenilinda, kwa hivyo sitatetereka hata kidogo." Aliapa kupambana na mafisadi hadi ushidi upatikane.
Alisema hivi sasa kumeibuka tabia ya baadhi ya watu nchini, kulazimisha yale wanayoyafanya wao yaonekane kuwa ndiyo ya ukweli kabisa hata kama ni ya uongo.
Naye mke wake spika, Margaret Sitta ambaye ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto amenukuliwa akisema kuwa “maisha ni mpito na kifo ni faida.”
Alikuwa anaunga mkano hoja ya mumewe, akinukuu kauli ya Askofu Norbert Mtega wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Songea, alipokuwa akizungumza katika msiba wa baba wa Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama.
"Kauli ile ya Askofu Mtega tunaichukua na sasa tunaifanya kuwa falsafa ya maisha yetu, kwa maana hiyo kwetu sisi sasa maisha ni mpito tu na kifo kwetu ni faida," alisema waziri huyo.
Kikao cha NEC kiliunda kamati ya watu watatu kutafuta kiini cha kile kilichoita mgogoro miongoni mwa Bunge, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, serikali na CCM na jinsi ya kuuondoa.
Kamati hiyo iliyoko chini ya rais mstaafu Mwinyi inahusisha aliyekuwa spika wa bunge la Jamhuri, Pius Msekwa na aliyekuwa spika wa Baraza la Kutunga Sheria la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana.