- Ni hasira ya watuhumiwa ufisadi
KUNA mkakati wa makusudi wa kuhakikisha wabunge zaidi ya 30 wanasukumwa nje ya Bunge katika uchaguzi mkuu ujao, MwanaHALISI limeelezwa.
Taarifa zinasema mkakati huo umepangwa na kusukwa kwa ustadi na baadhi ya wanamtandao wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi.
Wabunge ambao wameundiwa mkakati ni pamoja na Anne Kilango (Same Mashariki), Dk. Harrison Mwakyembe (Kyera), Hilda Ngowe (Viti Maalum), Samwel Sitta (Urambo Mashariki) na Michael Laizer (Longido).
Wengine ni John Malecela (Mtera), Christopher ole Sendeka (Simanjiro), Victor Mwambalaswa (Lupa), Batrice Shellukindo (Kilindi), Elisa Mollel (Arumeru Magharibi), Anthony Dialo (Ilemela) na Felix Mrema (Arusha Mjini).
Orodha ya wabunge wanaotakiwa kusukumwa nje ili kupunguza presha ya watuhumiwa wa ufisadi ni, Aloyce Kimaro (Vunjo), Lucas Selelii (Nzega), James Lembeli (Kahama), Said Mkumba (Sikonge) na Lazaro Nyaranda (Singida Kaskazini).
Wengine ni Profesa Mark Mwandosya (Rungwe Mashariki), Herbert Mtangi (Muheza), Injinia Stella manyanya (Viti Maalum), Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki), Lucas Siyame (Mbozi Magharibi) na Benson Mpesa (Mbeya Mjini).
Hatua hii inalenga kuzuia wabunge hao kuingia bungeni ili kusiwe na sauti za upinzani dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi katika uchaguzi ndani ya CCM mwaka 2012 na uchaguzi mkuu 2015.
Baadhi ya wanasiasa wanaotajwa kuwamo katika mtandao huo, ni Nazir Karamagi, Rostam Aziz, Kingunge Ngombale-Mwiru na Edward Lowassa.
Kwa majina ya wahusika, mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameita umoja huo kwa mkusanyiko wa herufi mbili za kila jina kuwa ni KAROKILO.
Kwa mujibu wa walioona orodha na taarifa zake mbalimbali, kundi hilo nina muundo wa chama cha siasa. Kuna kile kinachoitwa Kamati Maalum na Kamati Kuu.
Kwa mfumo wa CCM, Kamati Maalum huwa inafanya kazi Zanzibar na Kamati Kuu ndicho kikao cha nchi nzima kinachojumuisha watu wachache wanaotokana na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na wanaoteuliwa na mwenyekiti.
Taarifa kutoka vikao ambavyo tayari vimefanyika zinaonyesha kuwa Kamati Kuu, ambayo ni kikao cha juu, ina wajumbe wachache na Kamati Maalum ndiyo yenye wajumbe wengi.
Kufahamika kwa mtandao wa KAROKILO kunafuatia kuvuja kwa taarifa nyingi za mtandao wa MSALO uliolenga 'kusafisha' majina ya watuhumiwa wa ufisadi.
'Inaonekana itaundwa mitandao mingi. Kila siri zitakapokuwa zinavuja, itabidi wahusika wakane, waweke mtandao chini na kuunda mwingine,' ameeleza mtoa taarifa.
Kutajwa kwa Ngombale katika mtandao wa sasa bado kuna utata. Kuna taarifa kwamba wakati mtandao unalenga 'kumpiku Rais Kikwete na wenzake,' ni Kingunge aliyepigania kuteuliwa kwa Kikwete na kuendelea kumlinda kwa hoja hadi sasa.
Mtoa taarifa amesema kama Ngombale atakuwa katika kundi hilo, badi ni kwa makusudi ya 'kuwachota akili' kwani hawezi kumsaliti Kikwete.'
Kwa uchambuzi mwanana, wabunge wanaosukiwa zengwe ni wale wenye hoja nzito, kali na ambao wamejitambulisha na maslahi ya umma.
