- Wamkalia kikao Dar kummaliza, kuidhoofisha serikali
- Wawalenga pia Sitta, Makinda, Dk. Mwakyembe, Membe
BAADHI ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza mkakati wa kudhoofisha utendaji wa serikali kwa kumwandama na "kumchafua" Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
MwanaHALISI limefahamishwa kwamba mwendelezo wamjadala mkali kuhusu hadhi ya Zanzibar ni mojawapo ya mikakati inayotumiwa na baadhi ya wabunge hao ili kutimiza lengo lao la kuifanya serikali iendelee kujielekeza katika suala hilo na kuacha mambo mengine ya msingi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mjini Dar es Salaam na Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, tayari wabunge hao wamejikusanya na kujadili jinsi ya kuishughulikia serikali.
Taarifa za kuaminika zinasema, wabunge waliopanga mkakati huo, wanatoka katika kundi la Mtandao Maslahi. Baadhi yao walikutana Jijini Dar es Salaam Ijumaa na Jumamosi kuweka mikakati yao dhidi ya Pinda.
Kikao cha Dar es Salaam kilifanyika ofisini mwa mmoja wa wanachama wa kundi hilo. Ni katika kikao hicho, ilikubalika kwamba "mtandao usambae nchi mzima kuidhoofisha serikali."
Inaelezwa kwamba wajumbe wamepata nguvu zaidi kutokana na kuzuka hoja ya Zanzibar kama ni nchi au la, na kwamba kwa kuanzia, hoja hii itumike kuwaonyesha wananchi udhaifu wa serikali.
"Ndiyo ...katika hili, tumeamua kuendeleza mjadala wa Zanzibar, ili kudhoofisha nguvu ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni," alisema mtoa habari wetu, akinukuu mmoja wa wajumbe waliohudhuria mkutano wa Dar es Salaam.
Hata hivyo, mtoa taarifa amesema alichokisema Pinda kuhusu Zanzibar ndicho kilichomo katika katiba. Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inasema 'Tanzania ni Jamhuri ya Muungano na ni nchi moja.'
Mmoja wa wabunge aliyehudhuria kikao hicho cha kumlenga Pinda na serikali ni mwenyeji wa mkoa wa Kigoma. Kwa sasa MwanaHALISI litaghifadhi jina na jimbo la mbunge huyo.
"Hili ni kundi kubwa na lililoenea karibu nchi mzima. Lina lengo la kudhoofisha serikali ili iachane na hoja ya msingi ya kupambana na ufisadi," alisema mjumbe mmoja wa kundi hilo aliyeamua kuasi na kutoa siri.
Alisema, "Hata kazi unaiona sasa, imetokana na mkusanyiko huo. Lengo ni kuhakikisha watuhumiwa wote wa ufisadi wanasafishwa ili kuwaweka katika mazingira mazuri ya kisiasa katika siku zijazo."
Wajumbe wengi wa kundi hilo wanatokana na kundi lililojipa jukumu la kumsafisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na wenzake wanaohangaika kujitengenezea jina jipya baada ya kutuhumiwa katika miradi mingi ya kifisadi kwa muda sasa.
Mbali na wabunge, wajumbe wengine wa kundi hilo ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, wenyeviti wa CCM wa mikoa, makatibu, wakuu wa wilaya na baadhi ya mawaziri.
Inaaminika ni kupitia jitihada hizo za kusafisha watuhumiwa, baadhi ya wajumbe wamejipa jukumu jingine la kumchafua Spika wa Bunge, Samwel Sitta, kazi ambayo imeshaanza kufanyika.
Katika kundi linalotafutwa kuangamizwa wamo pia Naibu Spika, Anna Makinda, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii.
Wengine ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole-Sendeka, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Sababu hasa za kuwaandama wabunge hawa hazijaelezwa waziwazi, lakini wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini wanasema zinatokana na "ukali" wa baadhi ya walengwa dhidi ya ufisadi, hasa tangu Bunge ilipounda kamati iliyochunguza na kuibua ufisadi katika tenda ya umeme wa dharura kati ya serikali na kampuni feki ya Richmond.
