Wafanyakazi waheshimiwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 28 March 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI imeamua kuasi wafanyakazi. Wakati tayari imekuwa ikiwadhulumu kwa kuwatoza kodi kubwa kuliko makundi mengine, inataka kuzidi kuwadhulumu.

Imebuni mpango wa kuchukua akiba zao za uzeeni kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii. Inaleta mapendekezo hasi ya kurekebisha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Na. 8 ya 2008.

Wakati inaanzisha mamlaka hii (SSRA), lengo kuu lilikuwa ni kumaliza matatizo ya wafanyakazi. Viwango vidogo vya pensheni ni mojawapo.

Pensheni zimekuwa hazilingani hata kwa watumishi wanaofanya kazi zinazofanana au mishahara inayofanana. Viwango hivi vinategemea mfanyakazi yupo mfuko upi.

Mapendekezo mapya yanalenga kuilazimisha mifuko ilipe tozo kutokana na jumla ya mapato yao yanayohusisha michango ya wanachama – wafanyakazi – na mapato ya uwekezaji.

Ikumbukwe, mapato yatokanayo na uwekezaji, huongeza thamani ya michango ili pale mfanyakazi anapostaafu imsaidie kupata malipo yanayokaribia au kulingana na mapato anayopoteza sasa akiwa hana mshahara.

Hivi serikali inafikiriaje inapotaka kuchukua akiba za wafanyakazi na kuzitumia kwa kazi za kuangalia mifuko wakati jukumu hilo linalaswa kugharamiwa na kodi zinazokatwa kwenye mishahara yao!

Lakini pia, mapendekezo yanalenga kuondoa baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Mamlaka wenye elimu na ujuzi wa masuala ya hifadhi ya jamii. Bila shaka, lengo hapa ni kudhoofisha uwezo wa Bodi hiyo kusimamia mamlaka.

Sasa, iwapo mamlaka inataka kujiendesha bila usimamizi imara wa bodi, bodi za mifuko zinazoumiwa kutowajibika vilivyo kulinda maslahi ya wanachama, zitabadilika vipi?

Tunahofu serikali inatengeneza mgogoro na wafanyakazi; ambao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu, mishahara duni, huku gharama za maisha zikipanda kwa kasi.

Pensheni ndiyo tumaini pekee lililobaki kwao wanapostaafu. Ndio hili serikali inataka kuliua. Haioni huko ni kutaka kuwavuruga kiakili wafanyakazi?

Wakishavurugwa, hawatazalisha kwa tija, hawataitii serikali na watatafuta njia mbadala kuishi. Yaweza kuwa hujuma na migomo mfululizo. Wasifikishwe huko.

Serikali itambue inahitaji wafanyakazi ili kujenga taifa. Basi iache kuwalaghai na kuwaghilibu kupitia mfumo wa sheria.

Iondoe kasoro katika sheria ili kuimarisha maslahi ya wafanyakazi, ikiwemo kudhibiti ufisadi katika mifuko.

Tunasihi jumuiya za wafanyakazi, pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi bungeni, wazuie mapendekezo hasi ya mamlaka. Wakatae tamaa za watendaji wa mamlaka zinazotishia maslahi ya wafanyakazi. Wakomeshe ghiliba na ulaghai wao.

0
No votes yet