Wako wapi waliosema Afrika haiwezi?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 July 2010

Printer-friendly versionSend to friend

HISPANIA imetwaa taji la ubingwa wa dunia katika fainali za soka zilizofanyika nchini Afrika Kusini mwaka huu; lakini mshindi wa jumla wa michuano hiyo ni bara la Afrika.

Kabla ya michuano hiyo kuanza, vyombo vya habari vya nchi za magharibi vilikuwa vikitoa picha kwamba Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla havikuwa tayari kwa ajili ya kuandaa michuano hiyo.

Sote tunakumbuka namna vitendo vya uhalifu, hata vile vidogo sana, vilivyokuwa vikitokea Afrika Kusini vilivyokuwa vikiripotiwa kwa nguvu huko Ulaya na Marekani.

Hali hiyo ilifikia katika hali ya ‘uchizi’ Januari mwaka huu, wakati kikosi cha timu ya taifa ya Togo kiliposhambuliwa nchini Angola wakati wa michuano ya Kombe la Mataifa Huru ya Afrika.

Tukio hilo likawa sababu ya watu wa nje ya Afrika kuzidi kupiga kelele. Wakipiga kelele kana kwamba New York, London, Madrid na kwingineko hakukuwahi kutokea vitendo vya kigaidi. Hali ikawa mbaya kwelikweli.

Lakini tangu kwa kuanza kwa michuano hiyo mwezi uliopita, mambo yamekwenda vizuri kuliko kawaida na pengine taswira ya bara la Afrika inaweza kuwa imebadilika moja kwa moja.

Michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu ilikuwa ya mafanikio makubwa na kuna sababu kubwa mbili za kusema haya; nje na ndani ya uwanja.

Ngoja tuanze na mambo ya ndani ya uwanja. Jambo kubwa kuliko yote ni ule ukweli kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya karibuni ya michuano hiyo, timu iliyopewa nafasi kubwa ya kushinda ilishinda.

Kwa kawaida, timu ambayo imekuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa dunia kabla michuano kuanza imekuwa ikikwama kufanya hivyo. Lakini Hispania ilibadili hilo mwaka huu.

Uzuri mwingine ni kwamba timu hiyo ndiyo iliyokuwa ikicheza kandanda safi kuliko timu nyingine zote zilizoshiriki katika michuano hiyo. Pasi za uhakika, umiliki wa mpira wa kiwango cha juu na mchezo usio wa rafu.

Pengine dunia sasa itafumbuka macho na kuanza kuthamini umuhimu wa kucheza mpira mzuri. Na kama hili litafanikiwa, sifa zitakwenda kwa bara la Afrika lililoandaa fainali za mwaka huu.

Kwa waliosikia kuhusu uhudhuriaji wa mechi katika michuano hii, watakuwa wamesikia kwamba idadi ya watu waliohudhuria mechi za michuano hiyo ilizidi kidogo watu milioni tatu.

Katika historia ya Kombe la Dunia, ni mara mbili tu idadi ya wahudhuriaji ilizidi watu milioni tatu; mwaka 1994 wakati michuano hiyo ilipofanyika nchini Marekani na mwaka 2006 nchini Ujerumani.

Tofauti kubwa na fainali hizo mbili kabla ya hii ya Afrika Kusini ipo kwenye maeneo mawili makubwa; hali ya kiuchumi ya wakati husika na taarifa za hasi au chanya kabla ya michuano.

Mwaka 2006 wakati michuano hiyo ilipofanyika nchini Ujerumani, hali ya uchumi wa dunia ilikuwa katika wakati mzuri. Hakukuwapo na kitu kinachoitwa mtikisiko wa kiuchumi na watu wengi walikuwa na uwezo wa kwenda kuhudhuria.

Mwaka huu, fainali hizi zimefanyika katika kipindi ambacho dunia bado inaugua katika mtikisiko wa kiuchumi. Kwa hiyo, ukiondoa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika katika miaka ya 1930 wakati uchumi wa dunia ulipokuwa katika hali mbaya.

Katika mzingira kama haya ya kiuchumi na kutokana na uandishi mbaya wa habari za Afrika katika nchi zilizoendelea, ni wazi kwamba Afrika imefanya kazi kubwa sana na ya mafanikio makubwa katika fainali hizi.

Kama michuano hii ingefanyika wakati dunia ina hali nzuri ya kiuchumi kama ile iliyokuwapo mwaka 2006 na huku nchi za Ulaya zikitenda haki katika uandishi wao wa habari za Afrika, bila shaka, mahudhurio yangevunja rekodi mwaka huu.

Nje ya uwanja, kuna mambo mengi ya kujivunia kuonyesha michuano ya mwaka huu ilikuwa ni ushindi kwa bara la Afrika. Kwanza hakukuwapo na vitendo vya kihalifu kama ilivyokuwa ikisemwa kabla michuano haijaanza.

Hakuna aliyelalamika kung’atwa na nyoka au ng’e kama ilivyokuwa ikiandikwa sana na vyombo vya kigeni kwamba Afrika kuna idadi kubwa sana ya nyoka, hasahasa katika viwanja ambavyo nchi washiriki walikuwa wamepangwa kufanyia mazoezi.

Maandalizi pia yalikuwa ya kiwango cha juu. Hakuna aliyelalamika kuhusu usafiri na viwango vya makazi ya timu shiriki na washabiki waliohudhuria michuano.

Kabla ya michuano hiyo, kulikuwapo na mawazo kwamba Afrika haina uwezo wa kihoteli na huduma nyingine za jamii kuandaa michuano hiyo. Kilichotokea Afrika Kusini ni ushahidi kwamba uwezo wa namna hiyo upo.

Lakini ninaamini wazungu walishangazwa zaidi na aina ya viwanja walivyokutana navyo Afrika Kusini. Uwanja wa Soccer City unabeba watu wengi kuliko hata Wembley wa Uingereza.

Na katika nchi yoyote ya Ulaya, sijawahi kuona kiwanja kilichojengwa kiustadi na katika namna na mazingira ya kipekee kama ule wa Nelson Mandela Bay uliopo katika mji wa Port Elizabeth.

Uwanja huo upo pembezoni mwa bahari na umeonyesha maendeleo makubwa ya kiuhandisi na kiubunifu yaliyofikiwa na bara la Afrika linalopigwa vita kila kukicha na nchi zilizoendelea.

Inawezekana kwamba Afrika Kusini hailingani sana na nchi nyingine za kiafrika kwa mambo mengi. Wapo watakaosema kwamba pengine nchi hiyo haina sifa ya kuitwa nchi ya Afrika.

Lakini hao ni wale walioshikwa na haya baada ya kuona kile kilichotokea mwaka huu. Hii ni kwa vile, kabla ya michuano hiyo kuanza, sote tulichukuliwa kuwa ni kitu kimoja; kwa nini sasa tutengwe baada ya Afrika Kusini kufanikiwa?

Afrika Kusini ni sehemu ya Afrika na kilichotokea mwaka huu ni ushindi wa kusherehekewa kote. Leo na pengine miaka mingi kutoka sasa. Kama Mungu akiniweka hai, nitakuwa na mjukuu wakati michuano mingine itakaporejea tena barani Afrika.

Na wakati huo, mambo yatakuwa safi kuliko wakati mwingine wowote. Afrika Kusini imetutia moyo.

0
No votes yet