Waliopita, waliobebwa kura za maoni CCM


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 August 2010

Printer-friendly version
Gumzo

HALMASHAURI Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imepitisha wanachama 238 kugombea ubunge wa majimbo Tanzania Bara na Visiwani.

Miongoni mwa waliopitishwa, wapo waliotabiliwa na wale waliobebwa. Baadhi ya waliobebwa, ni Hamisi Kigwangala, aliyepitishwa kuwania ubunge katika jimbo la Nzega mkoani Tabora.

NEC imepitisha jina la Kigwangala baada ya kumuondoa katika kinyang’anyiro hicho, Hussein Bashe aliyeibuka kidedea katika kura za maoni.

Kuondolewa kwake kulitokana na kile Rais Jakaya Kikwete alichoita, “utata wa uraia wake.” Kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni, Kigwangala alishika nafasi ya tatu nyuma ya Bashe na Lucas Selelii.

Hivyo basi, aliyestahili kupitishwa kuchukua nafasi ya Bashe, alikuwa Selelii ambaye alishika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha kura za maoni.

Hadi sasa, hakuna anayejua sababu za NEC kutompitisha Selelii na kumbeba Kigwangala. Kinachofahamika kwa wengi ni kwamba Kigwangala ni mtumishi wa WAMA – taasisi inayoongozwa na mke wa rais, Mama Salma Kikwete.

Wengine wanasema uamuzi wa Kikwete wa kutomrudisha Selelii umelenga kufurahisha maswahiba zake, Rostam Aziz na Edward Lowassa, ambao wamedaiwa kusikika wakiapa kuwa Selelii hatarejea tena bungeni.

Sasa wachunguzi wa masuala ya siasa ndani ya CCM wanasema Kikwete aliona kwamba hatua yeyote ya kumrejesha Selelii, ingepanua ufa kati yake na maswahiba zake hao wawili.

Mbali na Bashe, mwingine ambaye hakutarajiwa kuteuliwa ni Justin Salakana aliyepitishwa kuwania jimbo la Moshi Mjini.

Kwanza, katika kinyang’anyiro cha kura za maoni, Salakana alishika nafasi ya tatu nyuma ya Athuman Ramole na Thomas Ngawaiya.

Pili, Salakana hana ubavu wa kupambana na mbunge wa CHADEMA katika jimbo la Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo.

Tatu, kumpitisha mtu ambaye si chaguo la wanachama wenzake na ikitiliwa maanani kwamba hana ubavu wa kushindana, ni kudhoofisha chama na kudidimiza demokrasia.

Nne, mwaka 1995 Salakana alikuwa mbunge wa Rombo kupitia CHADEMA, lakini katika uchaguzi uliofuata alishindwa vibaya na mbunge wa sasa, Basil Mramba kutokana na kile kilichodaiwa kuwa “kugeuza ubunge wake kuwa sehemu ya familia yake.”

Wachunguzi wa siasa wanasema Salakana kwa Ndesamburo, hata kama waliwahi kuwa chama kimoja, ni sindano na shoka. Wanasema amewekwa ili ashindwe na kupotea kisiasa.

Mwingine ambaye amepitishwa baada ya kumwagwa katika kura za maoni, ni Gerson Lwenge anayewania ubunge jimboni Njombe Magharibi. Alikuwa mtu wa tatu nyuma ya Thomas Nyimbo na Yono Kevela.

Hatua ya NEC ya kumuengua Nyimbo ambaye aliibuka kidedea, tayari imeleta kizaazaa ndani ya chama hicho. Nyimbo na wanachama wenzake kadhaa wa chama hicho, wamejiengua na kujiunga na upinzani ambako akigombea, hasa kupitia CHADEMA, ana uwezekano mkubwa wa kushinda.

Kwa zaidi ya miaka 10 Nyimbo amekuwa akituhumiwa na viongozi wake ngazi ya taifa kwa kudhoofisha chama, tuhuma ambazo zimekanushwa na viongozi wake wa mkoa.

Hata hivyo, hata kama madai ya Nyimbo yamebaki hai, NEC haikuwa na sababu za msingi za kutompitisha Kevela ambaye amekuwa mbunge katika jimbo hilo kwa kipindi kimoja tu. Badala yake imembeba aliyeshika mkia.

Orodha ya waliopitishwa na ambao hawakustahili ni ndefu. Lakini kubwa zaidi hapa ni hili: Kinyang’nyiro hiki, kimethibitisha kwa mara nyingine tena, kwamba rushwa ni dondandugu ndani ya CCM.

Hata ndani ya mkutano wa NEC, madai ya rushwa yaliibuka. Baadhi ya viongozi wa CCM, akiwamo mtendaji mkuu wa chama, Yusuph Makamba walituhumiwa kuvuruga uchaguzi kwa maslahi binafsi.

Tuhuma dhidi ya Makamba zilitolewa na wajumbe wengi akiwamo mwanasiasa machachari, Nape Nnauye. Akiongea kwa lengo la kukinusuru chama chake, Nape alisema Makamba alijipa mamlaka ya kubadilisha taratibu za uchaguzi bila idhini ya NEC.

Alisema jambo hilo linatafsiriwa na wengi kuwa mtendaji wa chama “alihongwa” ili kubeba baadhi ya wagombea. Makamba hakujibu tuhuma hizo.

Hata hivyo, wiki moja kabla ya mkutano wa NEC Makamba alinukuriwa akisema, “Kila mgombea wa ubunge na udiwani ametoa rushwa, isipokuwa walizidiana viwango.”

Ukiondoa haya mawili, jingine linaloonekana katika mchakato huu, ni kuwa wagombea wengi waliopitishwa ni wapya.

Kwa mfano, katika mkoa wa Morogoro, kati ya wabunge 10 waliokuwapo katika Bunge lililopita, ni wabunge watatu tu waliorejeshwa kuwania tena ubunge.

Waliorejeshwa ni Celina Kombani (Ulanga Mashariki), Shabiby Ahmed (Gairo) na Mustafa Mkullo (Kilosa).

Mbunge wa Viti Maalum katika Bunge lililopita, Dk. Lucy Nkya kutoka mkoa wa Morogoro, sasa amepata jimbo. Amepitishwa kuwania ubunge katika jimbo la Morogoro Mashariki.

Wabunge ambao wameshindwa katika kura za maoni na ambao NEC imebariki kutokomea kwao kisiasa, ni Dk. Juma Ngasongwa (Ulanga Magharibi) na Dk. Omari Mzeru (Morogoro Mjini).

Wengine ni Sulemani Sadiq (Mvomero), Clemence Liyamba (Mikumi), Casto Ligalama (Kilombelo), Hamza Mwenegoha (Morogoro Kusini Mashariki) na Sameer Lotto (Morogoro Mashariki).

Wabunge wapya waliopitishwa kuwania nafasi hiyo, ni Aziz Abood (Morogoro Mjini), Lucy Nkya (Morogoro Mashariki), Innocent Kalogeris (Morogoro Kusini),
Amos Makala (Mvomero), Abdulsalaam SAS (Mikumi), Hadji Mponda (Ulanga Magharibi) na Abdul Rajabu Mteketa (Kilombero).

Katika mkoa wa Kagera, kati ya wabunge 10 waliokuwapo katika Bunge lililopita ni wabunge watano tu, waliopitishwa kuwania tena nafasi zao.

Hao ni pamoja na John Magufuli (Chato), Balozi Khamis Kagasheki (Bukoba Mjini), Eustace Katagira (Kyerwa), Gosbert Blandes (Karagwe) na Oscar Mukasa (Biharamulo).

Waliofungiwa nje ni Willison Masilingi (Muleba Kusini), Diodorus Kamala (Nkenge), Nazir Karamagi (Bukoba Vijijini), Ruth Msafiri (Muleba Kaskazini) na Profesa Fetham Banyikwa (Ngara).

Katika majimbo hayo wagombea waliopitishwa ni Assumpter Mshama (Nkenge), Jasson Rwekiza (Bukoba Vijijini), Charles Mwijage (Muleba Kaskazini), Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini) na Deogratias Ntukamazina (Ngara).

Mkoani Tabora, kati ya wabunge wanane wa zamani, ni watatu tu waliorejeshwa katika kinyang’nyiro. Hao ni Samwel John Sitta (Urambo Mashariki), Said Nkumba (Sikonge) na Rostam Aziz (Igunga).

Dk. James Msekela (Tabora Kaskazini), Teddy Kasela-Bantu (Bukene), Siraju Kaboyonga (Tabora Mjini), Lucas Selelii (Nzega) na Tatu Ntimizi (Igalula), hawakurejeshwa kutetea nafasi zao.

Wagombea waliopitishwa kuchukua nafasi za wabunge hao wa zamani, ni Ismail Aden Rage (Tabora), Rostam Abdulrasul Aziz (Igunga), Athuman Mfutakamba (Igalula), Sumar Mamlo (Tabora Kaskazini), Seleman Zedi (Bukene) na Hamisi Kigwangala (Nzega).

Profesa Juma Kapuya ambaye alikuwa mbunge wa Urambo Magharibi jimbo lake limehamishiwa mkoa mpya wa Katavi. Jimbo lake linafahamika kama jimbo la Kaliua.

Mkoa mwingine ambao umevunja rekodi ya kupata wagombea wapya ni Iringa. Wabunge wa zamani waliopita katika kinyang’anyiro cha sasa ni watano tu kati ya 11 waliokuwapo katika bunge lililopita.

Waliorejea ni Monica Mbega (Iringa Mjini), Peter Msolla (Kilolo), William Lukuvi (Ismani), Binilith Mahenge (Makete) na Anne Makinda (Njombe Kusini).

Wagombea wapya, ni Wiliam Augustino Mgimwa (Kalenga), Deo Filikunjombe (Ludewa), Hassan Mohamed Mgimwa (Mufindi Kaskazini), Mendrad Lutengano Kigola (Mufindi Kusini), Deo Sanga – Jahpeople – (Njombe Kaskazini) na Gerson Hosea Lwenge (Njombe Magharibi).

Je, hatua hii ina maana gani? Kwanza, inaonyesha kwamba kinyang’anyiro cha uspika kitakuwa kikali baada ya uchaguzi. Hii ni kwa sababu, kila anayetaka nafasi hiyo atalazimika kushawishi wabunge wapya watakaoingia baada ya uchaguzi.

Hata hivyo, iwapo atatokea mgombea mwanamke kujitosa katika kinyang’anyiro hicho, kuna uwezekano mkubwa wa mgombea huyo kushinda, hasa iwapo ataungwa mkono na wanawake wenzake.

Tayari naibu spika wa sasa, Anne Makinda amenukuliwa akiwaambia baadhi ya marafiki zake, kwamba amekataa ofa aliyopewa na kundi la wapinzani wa spika wa sasa Samwel Sitta.

Makinda amenukuliwa akisema alifuatwa ili kuombwa kugombea nafasi hiyo, lakini kutokana na mahusiano yake mazuri na Sitta, amekataa ombi hilo.

Haijulikani kundi hilo litamfuata nani baada ya karata yao hiyo ya kwanza kuchanika. Bali kwa ushindi mkubwa wa upinzani na wingi wa wabunge wapya ambao wanaelewa alichokuwa akifanya Sitta, uwezekano wa spika wa zamani kurudi kwenye nafasi yake bado upo palepale.

Pili, vigogo wanaotaka kujiimarisha kufanikisha malengo yao ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kujijenga kwa wabunge wapya.

Tatu, CCM kitakabiliwa na kibarua kigumu mbele ya wananchi, pale wagombea wake watakapokutana na wagombea wa upinzani.

Hii ni kwa sababu, katika orodha ya wagombea waliopitishwa na NEC, wengi watakuwa hawana rasilimali za kutosha, hasa majigambo ya kufanikisha miradi ya maendeleo.

Sita, katika orodha iliyopitishwa, wagombea wengi wana uwezo mdogo wa kuchambua na kuainisha mambo, jambo litakalofanya CCM kupata wakati mgumu wa kuuza wagombea wake. Wanafahamika hata kwa majina.

Saba, kupitishwa kwa wagombea hawa kunaweza kuwa ni anguko jingine kwa Lowassa. Tofauti na mwaka 2005 ambapo wagombea wengi waliopitishwa walitokana na kundi la mtandao, waliopitishwa katika kinyang’anyiro hiki ama hawana upande, au ni vigumu kuwatambulisha na kundi lake.

Jingine ambalo limejitokeza katika mchakato huu, ni kuibuka kwa mbunge wa zamani wa jimbo la Tarime, Kisyeri Chambiri ambaye sasa amepitishwa kuwania ubunge katika jimbo la Babati Mjini.

Haikutarajiwa kwa kiongozi ambaye anadaiwa kuvuruga mkoa wa Mara, hadi kuotesha makundi yaliyosababisha mtafaruku mkubwa wa uongozi, kupitishwa kuwania ubunge katika jimbo hili.

Ni Chambiri huyuhuyu aliyesababisha jimbo la Tarime Mjini kuangukia upinzani. Ni yeye na kaka yake, Enock Chambiri waliokuwa wanatuhumiwa kuhubiri “ukabila na uzawa.”

Yawezekana yaliyomkumba Chambiri huko Tarime yakamrudia Babati ambako ni mhamiaji. Bali harakati zake za kurejea bungeni kupitia mbali na nyumbani, zimeonyesha ujanja au ujasiri wa aina yake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: