Waliopitia JKT majasiri wa ufisadi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 17 August 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

HOTUBA ya makadirio ya matumizi ya fedha ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo iliyowasilishwa na Dk. Emmanuel Nchimbi ilijadiliwa na wabunge wengi kwa hisia kali.

Wabunge wengi walijitosa kuzungumzia kuporomoka kwa maadili ya taifa, wengine walizungumzia kukiukwa kwa maadili ya uandishi wa habari na baadhi walitetea hadhi ya vijana.

Waliozungumzia maadili ya taifa, kwa dhati walilaani vijana kutembea nusu uchi wakidai kuwa maadili ya taifa hayaruhusu. Wakati huohuo, waliwasifu Wamaasai kwa kuendeleza utamaduni wao.

Nikashangaa ukigeugeu huu. Nijuavyo, uvaaji wa asili wa Wamasai, hasa kundi la vijana walinzi (morani), ni kuacha upande mmoja wazi. Kwa asili morani huvaa lubega nyekundu peke yake bila kaptura.

Uvaaji unaozingatia maadili ya kitaifa ukoje ili wanaovaa kinyume waonekane wameukiuka?

Wabunge wengine walikwenda mbali na kutoa pendekezo kwamba lirejeshwe jando la kitaifa ili wafundishwe ukakamavu, ujasili, mwenendo, maadili, nidhamu na uzalendo kwa taifa lao.

Walisema ukiona mtoto anamwambia mtu mzima kuwa ni mwongo basi ujue huyo amepata suna hospitalini na si kwenye majando ya asili ambayo hufundisha adabu, heshima na namna ya kuishi na watu. Jando ambalo wabunge wamependekeza lirejeshwe ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili vijana wote wakajifunze ukakamavu, ujasiri, na uzalendo. Uzalendo?

Hivi vijana wote waliopita JKT ni wazalendo kwa nchi yao? Je, ni kweli jando hilo liliwajenga vijana kuthamini nchi yao na kuilinda? Je, ni kweli wanaotoka kwenye jando hilo ni wakakamavu, jasiri na wenye maadili mema?

Mwalimu Nyerere akitambua umuhimu wa mafunzo hayo, akawa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda JKT. Hata hivyo, ushahidi upo kwamba watu wote wanaosakamwa kwa rushwa, uhujumu wa uchumi na kukosa uzalendo ni waliopitia JKT.

Orodha ni ndefu. Baadhi yao ni walionunua kivuko kibovu, waliofilisi mashirika ya umma, na waliofuta miiko ya Azimio la Arusha ili wajilimbikizie mali.

Wengine ni waliozidisha bei katika ununuzi wa rada, waliojiuzia nyumba za serikali, walioiba kupitia EPA, Meremeta, Tangold, na walioingia mikataba mibovu ya madini.

Na mbunge aliyesema katika wizara ya nishati na madini kuna mdudu anaitwa David Jairo amepita jando lipi? Au kwa vile ni wa chama cha CCM?

Ni nani kati ya hao hakupitia JKT? Uzalendo uko wapi kwa walioanzisha kampuni ya kutapeli kama Richmond/Dowans? Je, uzalendo ni kutia ndani fedha kutokana na ubinafsishaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA)? Kuuza kinyemela ekari 800,000 wilayani Mpanda?

Kwa kuwa watu walipitia JKT ndio wanaifisidi nchi bila kificho ni sahihi kusema JKT imejenga ujasiri wa kifisadi na uhaini. Ipo mifano hai.

Kwanza, kundi la kwanza kukosa uzalendo ni mwaka 1969 waliotuhumiwa kutaka kuipindua serikali ya Mwalimu Nyerere. Nani amesahau kilichowapata John Lifa Chipaka, mdogo wake, Eliya Dunstan Chipaka, pamoja na Bibi Titi Mohamed, Michael Kamaliza, na wanajeshi wanne?

Pili, mwaka 1983 kundi la vijana wanajeshi, akiwemo hayati Eugene Maganga, lilitiwa nguvuni kwa jaribio la kutaka kuipindua serikali ya Mwalimu Nyerere. Halafu kuna kijana aliteka ndege kwa kutumia embe.

Tatu, kansa kubwa inayotafuna ofisi nyingi za serikali na za umma tangu miaka ya 1970 ni matumizi ya rushwa ndipo mtu kupata ajira, au mtumishi kupata uhamisho.

Nne, ugonjwa mwingine unasosubiri tiba kwa mafunzo ya JKT ni uchelewaji mkubwa wa watumishi kazini. Hata bungeni wengi husaini tu kwa ajili ya kujihakikishia posho. Wakishatia saini, hao wanatoweka.

Tano, kila mwaka, Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) hukagua hesabu za wizara, halmashauri na idara mbalimbali. Mabilioni ya shilingi hukutwa yamefujwa.

Sita, askari na polisi na wa jeshi la ulinzi, watu waliofunzwa ukakamavu, ujasiri na uzalendo kwa nchi yao, leo wanashiriki vitendo vya ujambazi na baadhi ya viongozi hukata posho za maofisa wa chini bila ya ridhaa yao.

Uko wapi uzalendo kumlipa ofisa wa polisi Sh. 100,000 badala ya Sh. 150,000 zilizoidhinishwa kisheria? Uko wapi uzalendo wa kukata Sh. 5,000 kwa michango ambayo polisi anaambiwa fedha zikishakatwa? Uko wapi uzalendo iwapo wapiganaji na maofisa wa JWTZ wanapunjwa posho zao za madaraja, likizo na chakula?

Wabunge wanaweza kuzungumzia faida ya mafunzo hayo kinadharia, lakini hali halisi JKT, kama sehemu ya jando, haijafanikiwa kwa kiwango hicho kujenga maadili, nidhamu na uzalendo.

Kwenda shule kusoma ni jambo moja, lakini kuelimika ni jambo jingine. Kwenda JKT kupata mafunzo ni jambo moja lakini kuiva kimaadili na kuwa mzalendo kwanchi yako ni jambo jingine kabisa.

Upande wa pili, kuna wabunge wanaolalamikia kushuka kwa maadili bila ya kujua wanachotaka. Aliyewahi kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Muhammed Seif Khatibu ni mfano wa wabunge hao.

Mwanasiasa huyu anayemiliki kampuni ya Zanzibar Media Corporation (ZMC) inayoendesha kituo cha redio cha Zenj FM na gazeti la Nipe Habari alilaani ukiukwaji wa maadili ya uandishi wa habari lakini mwishowe akatetea gazeti lililoyakiuka.

Alisema mhariri aliyeandika maoni ya “Dk. Slaa kamwe hawezi kuwa Rais” alikuwa sahihi maana alikuwa “anatabiri tu.”

Hilo ndiyo tatizo la viongozi na wabunge wa CCM – kudhani uchochezi ni pale gazeti linapowasakama viongozi wa chama hicho tu. Wanasahau kuandika au kutoa kauli inayoonesha kundi fulani katika jamii au chama fulani cha siasa hakiwezi kushinda uchaguzi, pia ni uchochezi tena mbaya na wa hatari.

Mbunge huyo wa Uzini alitoa majibu kuficha uso kwa vile serikali ya chama chake iuchi. Alisahau mwaka 1995 kituo cha televisheni cha DTV kiliadhibiwa kwa kosa la ‘kutabiri’ kwamba Maalim Seif Shariff Hamad aliibuka mshindi.

DTV waliadhibiwa kwa sababu utabiri wao ulionesha anguko kwa rais wa serikali ya CCM, “Komandoo” Dk. Salmin Amour Juma ambaye huteua Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kwa Tanzania bara, chombo cha serikali kisingeweza kuadhibiwa kwa vile kilikuwa kinatoa msimamo mzito dhidi ya upinzani kwamba Rais Jakaya Kikwete asingeweza kushindwa.

Falsafa hii ni nyepesi kwamba baridi ina mzizimo mkali kwa kondoo asiye na manyoya. DTV alikuwa kondoo asiye na manyoya akaadhibiwa kwa sheria ileile ambayo chombo cha serikali kimeachwa huru na kinasifiwa kwa kufanya utabiri mzuri. Na huo ikawa ndio utendaji jasiri na unaojali uzalendo!

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)