Wangwe ahusishwa na Dk. Kabourou


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 01 July 2008

Printer-friendly version
Yadaiwa ni mkakati wa CCM
MAKAMU  mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chacha Wangwe

MAKAMU mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chacha Wangwe, 'amejiweka kitanzi' kutokana na kukaidi ushauri aliopewa na Kamati ya Wazee ya chama hicho , MwanaHALISI limedokezwa.

Jumamosi iliyopita, Kamati Kuu (CC) ya CHADEMA chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe, ilimsimamisha uongozi Wangwe ikisubiri uamuzi wa mwisho wa Baraza Kuu.

Taarifa za ndani ya kikao zinasema Wangwe alikaidi agizo la Kamati ya Wazee iliyokuwa chini ya mwenyekiti Edwin Mtei, ilimuagiza kukana, kwa maandishi, tuhuma za kushiriki kwake kuandika taarifa zinazokikashifu chama na baadaye 'akazusha vurugu katika kikao.'

Awali Wangwe alikubali agizo hilo lakini baadaye alikataa kulitekeleza kwa madai kuwa hakupewa 'kabrasha lililokuwa na nakala za magazeti na vipeperushi vinavyokashifu CHADEMA.'

Wajumbe wengine wa Kamati ya Wazee, ni Bob Makani, Profesa Mwesiga Baregu, Balozi Christopher Ngaiza na Philemon Ndesamburo.

Miongoni mwa tuhuma hizo ni kushirikiana na wanaotajwa kuwa maadui wa CHADEMA, 'kugombana na viongozi wenzake na kuunda vikundi vya kuvuruga chama.'

Mtoa taarifa amesema ajenda iliyomwangusha Wangwe iliibuka katika CC baada ya Wangwe 'kugoma kutekeleza ushauri wa wazee, kutoa tuhuma na kufanya vurugu ndani ya ukumbi.'

'Pale hapakuwa na ajenda ya kumsimamisha. Hatua ilitokana na dharau na kiburi cha Wangwe,' alisema mtoa taarifa.

Alisema, 'CC ilipokea taarifa kutoka kwa Kamati ya Wazee, ambayo ilimtuhumu Wangwe kuwa na uhusiano na wanaoandika na kutawanya taarifa za kukikashifu chama.'

Baada ya majadiliano yaliyodumu kwa saa kadhaa, Kamati ya Wazee ilimtaka Wangwe kukana kwa maandishi vipeperushi na kile kilichoitwa na wazee, 'kazi za kishetani za kuangamiza upinzani.'

Wanaotuhumiwa kushirikiana na Wangwe kuvuruga chama, ni pamoja na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam waliosimamishwa na ambao wanadaiwa kuongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Amani Warid Kabourou ambaye sasa amejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hivi sasa, Dk. Kabourou ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. MwanaHALISI halikuweza kumpata Dk. Kabourou kuzungumzia tuhuma hizo.

Mbali na kukutana na Wangwe, Kamati ilikutana na Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa.

Imeelezwa kuwa kwanza Wangwe, baada ya kukataa kukana 'maandishi ya kishetani' kwa mandishi, CC ilimtaka atoe maelezo kwa nini alikuwa anakaidi agizo.

Ni katika hatua hii Wangwe alisema hakupewa kabrasha husika na kuanza kutoa tuhuma dhidi ya Dk. Slaa, Mbowe, Chiku Abwao na mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu.

Wangwe amenukuliwa kumwambia Mtei, 'Wewe ni muasisi, lakini ni sawa na mimi. Nimeshafika juu, hakuna wa kunirudisha. Hivi ni vita vya uchaguzi, nami natangaza rasmi kupambana na Mbowe (Freeman Mbowe).'

Baada ya kubanwa kukana machapisho na kufuta kauli dhidi ya viongozi, ndipo Wangwe alitetea vipeperushi vya kashfa akisema, 'Kama ninyi mnajiona tofauti na mnavyoandikwa, basi wananchi na wanachama wanawaona hivyo.'

Wakati baadhi ya wajumbe walikuwa na maoni kwamba afukuzwe kwenye chama, wengine waliona asimamishwe uongozi. Lakini kuna waliokuwa na mawazo kuwa ajiuzulu mwenyewe ili kulinda hadhi ya chama.

Mjumbe mmoja baada ya mwingine walimsihi Wangwe ajiuzulu. Alikataa. Ndipo kikao kikaamua kupiga kura kuhusu kumsimamisha uongozi; huku wajumbe 24 kati ya 31 wakiafiki asimamishwe.

Ndani ya kikao, Wangwe ananukuliwa akisema 'Dk. Slaa, pamoja na kuonekana mahiri bungeni, lakini hafanyika kazi zake kikamilifu na hana uwezo wa kushika nafasi ya katibu mkuu.'

Ni kauli hiyo ya Wangwe iliyozidi kuwatibua wajumbe. Lakini hasira zilipanda zaidi pale Wangwe anapodaiwa kutaka kumpiga Tundu Lissu.

'Ilipofika hapo, hata wale waliokuwa wanataka asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kukaidi agizo la Kamati ya Wazee, walikuja juu,' alisema mtoa taarifa mwingine.

Lissu alithibitishia MwanaHALISI kutokea tafrani kati yake na Wangwe. Alisema chanzo chake kilitokana na yeye kumueleza kuwa ni 'mtu anayependa ugomvi.'

Imeelezwa kwamba mjadala wa kumuondoa Wangwe ulidumu kwa zaidi ya saa tano. Ulianza saa 5 usiku na kulimalizika saa 9 alfajiri.

Wangwe aliliambia MwanaHALISI, Jumapili kuwa amefunga mjadala, amekubaliana na uamuzi na kwamba nguvu zake zote anazielekeza jimboni kwake Tarime.

Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari vimeeleza kuwa Wangwe anatarajia kupinga uamuzi wa CC mahakamani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: