'Wapambanaji' wanapogeuka wasaliti
KUNDI la wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwamo wabunge waliojipachika jina la "wapiganaji," limesaliti umma na kujisaliti lenyewe.
Wajumbe katika kundi hili hawana tena mahali pa kushika. Wanaelea. Wanapwaya. Wamepondekapondeka. Itabidi watembee huku wameziba nyuso zao, angalau kwa miezi kadhaa.
Wabunge hawa waliiachia serikali kufanya itakavyo juu ya lile sakata la Richmond. Umma haujafurahishwa na mgeuko wa wawakilishi hao. Umesalitiwa.
Hisia za kusalitiwa zimeibuka kwa nguvu kwa sababu umma ulilishwa maneno ya baadhi ya wabunge waliosema, kwa vinywa vyao, “Tutakufa na Richmond.”
Hawa ni wale waliojipambanua kuwa hawataki kusikia lugha nyingine yoyote mpaka serikali itekeleze kwa kina maazimio 23 ya Bunge.
Walionyesha kuchukia ufisadi, kukwazwa na wizi wa mali ya umma; na kwa hiyo kutamka kuwa wamejitoa muhanga kusimamia haki.
Hivi ni viapo vilivyotolewa Februari 2008, vikaendelea hadi Februari 2009, vikazidi kutolewa; lakini ilipowadia Februari 2010, umma ukapatwa na mshangao mkubwa.
Jumatano ya 10 Februari 2010, wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, William Shelukindo, alipotoa maelezo ya kamati yake bungeni kuhusu taarifa ya serikali ya kutekeleza maazimio juu ya Richmond, alikuwa amelowa.
Kamati iliyokuwa inaungwa mkono, kwa nguvu zote, na wabunge wengi, tena wa chama tawala, ikanyosha mikono juu kana kwamba kuna makubaliano yaliyofikiwa kati yake na serikali.
Kama kwamba hii siyo ile kamati iliyokuwa kali ikitaka kila azimio la Bunge litekelezwe. Ikaishiwa pumzi.
Lakini la kushangaza zaidi, hata wabunge ambao si wajumbe wa kamati hii, hawakutaka wala kujionyesha kwamba wanaijua Richmond.
Ukiacha mbunge wa Karatu, Dk. Wilibrod Slaa, ambaye alisimama hadi dakika ya mwisho, wengine wote hakuna aliyeonyesha msimamo thabiti katika hili.
Walioonekana kuleta mwanga mpya, matumaini na pambazuko jipya ili kuwa mwanzo wa kujenga kizazi adilifu, wameyeyuka.
Jumatano ya 10 Februari 2010, umma ulipata ufunuo, huu si mwingine bali ni ule wa kufunuliwa kwamba hakika mabadiliko ya kweli ndani ya nchi hii hayawezi kuletwa na walewale ambao ni sehemu ya matatizo lukuki yaliyopo.
Kwa maneno mengine, CCM yenye wanachama wengi na viongozi wengi ambao wamekuwa sehemu ya mchezo mchafu ndani ya nchi hii, haiwezi kuwa mkombozi wa taifa hili.
Viongozi wa CCM ambao wamekuwa katika kila kashfa chafu ya kuiba mali ya umma, kuingia mikataba tata, kufilisi nchi na kila aina ya uchafu unaoweza kutajwa, kamwe hawawezi kuwa wakombozi wa taifa hili.
Waliotaka kuthibitisha ujasiri, kumbe hawana ubavu wala ujasiri wa kusimamia hayo wanayotamka kwa vinywa vyao.
Wamethibitika ni watu dhaifu. Waoga na wasioweza kujitegemea nje ya CCM. Ni mateka kama mateka wengine. Wanaona kashfa ya Richmond kama mkwe! Haishikiki, haikamatiki; wamegwaya wote.
Kilichotokea ni kitu kimoja tu, kwamba wabunge wapambanaji sasa wamerejea kwenye ngome yao. Wamekumbuka gome lao, wamerudi nyumbani kuendelea na dini yao.
Baada ya kueneza kiini macho, kwa kupora hoja ya ukombozi wa rasilimali za nchi kutoka kambi ya upinzani, sasa wamerejea kundini; wanakula na kukumbatiana.
Wabunge wamerejea kundini kwenda kuchaguana; lakini wakiwa wamoja: wachafu kwa wasafi, walafi kwa walioshiba kwa ngeli.
Hawa hawawezi kuleta mapinduzi kama wachafunzi ni wao au wamo ndani yao, au ni wenzao wanaokumbatiana na kuridhiana kama “kifo” cha Richmond kilivyodhihirisha.