Wasaliti wamemwangusha Nchimbi TFF

MGOMBEA nafasi ya makamu wa pili wa rais katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), John Nchimbi ameshindwa lakini amebaki akijipongeza: “Kwa kweli nastahili pongezi.”
Nchimbi alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kukubali matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Kwa kampeni za mwezi mmoja na kuvuna idadi hii ya kura, napaswa kujipongeza. Kwa kweli nastahili pongezi,” alisema Nchimbi.
Katika uchaguzi huo mdogo, Nchimbi aliyejitosa kwa mara ya kwanza kuwania nafasi hiyo aliambulia kura 47 huku mshindi Ramadhani Nassib akiondoka na kura 54 yaani kura saba zaidi. Nassib alikuwa anatetea nafasi hiyo kupitia klabu ya Mtibwa Sugar wakati Nchimbi alidhaminiwa na Majimaji ya Songea.
Katika nafasi ya mjumbe wa kamati ya utendaji kutoka kanda ya tano ya TFF, Brass Kiondo aliibuka mshindi akiwabwaga Samson Mkisi na Gwamaka Mwaihojo au Prince Mwaihojo.
Lakini mvutano ulikuwa katika nafasi ya makamu wa pili wa rais ambako kulikuwa na kambi nzito, imara na zilizokuwa zinajua fitina za uchaguzi. Kambi zote mbili zilitegeana na kwenye ukumbi wa mkutano hakuna upande uliothubutu kuuliza swali.
Kwa nini? Kwa sababu ya hofu ya kuumbuana. Katika kipindi chote cha kampeni, siku mbili au moja kabla ya kufanyika uchaguzi ndizo zilihitimisha ubishi wa nani anafaa kushika nafasi hizo.
Wapambe wa Nassib walijipa ‘dole lakini wapambe wa Nchimbi, ambaye awali alifikiriwa angetupwa kiulaini walibadili kibao na kumweka katika wakati mgumu Nassib.
Kijana huyo, mdogo wake Naibu Waziri wa Jeshi la Wananchi Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa, Emmanuel Nchimbi alifanikiwa kujikingia wajumbe 55 kati ya 101 wa mkutano mkuu wa uchaguzi. Endapo wajumbe hao wangempigia kura, angemwachia Nassib kura 46.
Hilo ndilo kosa la mwisho lililomgharimu Nchimbi na atakuwa anajilaumu kwa nini hakuwakumbatia wajumbe wote asubiri huruma yao. Maana wasaliti wanane kati ya hao 55 ndio waliosabaisha akapigwa dafrao.
Katika kipindi chote cha kampeni yeye ndiye alikuwa na kazi ya kubadili fikra za wapiga kura ambao walielemea kwa Nassib na sababu kubwa ni kwamba zimwi likujualo halikuli likakwisha.
Kwa hiyo Nassib amefaidika kutokana na msemo huo baada ya wajumbe hao wanane kumsaliti Nchimbi. Isitoshe kati ya hao wanane, alikuwa anahitaji kura tu ambazo zingemwezesha kujikingia kura 51 (47 + 4) na kumwacha Nassib akifikisha kura 50.
Kosa la kwanza la Nchimbi alilifanya mwanzo kabisa. Baada ya kudhaminiwa na klabu ya Majimaji kuwania nafasi ya makamu wa pili wa rais, hakuwaona wenye soka mkoani yaani Chama cha Soka mkoa wa Ruvuma (FARU).
Mwenyekiti wa FARU, Joseph Mapunda akaungana na wenyeviti wengine wanne wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga na Dar es Salaam. Amin Bakhressa wa Dar akawa kinara wa kuchukua na kurejesha fomu kwa ajili ya Nassib.
Hata hivyo, Mapunda alikuja kuwa miongoni mwa wajumbe waliobadili msimamo na kuanza kumpigia debe Nchimbi. Hivyo basi, usaliti ukaingia, kambi ya Nassib ikavurugika.
Mvurugiko wa kambi ya Nassib na kuanza kushamiri kwa kambi ya Nchimbi kuliwaibua wazee wa soka au ‘football fitina’. Hao walishupalia kijana huyo ajitoe na alipokataa wakadai hakuwa na uamuzi wake binafsi juu ya kuwania nafasi hiyo nyeti ndani ya shirikisho.