Wastaafu kama Mkapa wafutiwe pensheni


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version

WAZAMBIA walipotunga sheria inayombana Rais Mstaafu kujihusisha na masuala ya “siasa za kila siku”, walilenga mambo mengi. Sheria hii kila mtu anaielewa kivyake.

Wapo waosema ilitungwa kuwabana wastaafu “wanoko”. Wale wasiokubali kulala usingizi huku wakiona mambo yanaharibika.  Wanatungiwa sheria kubanwa, kwa sababu “wanawakosesha usingizi” viongozi walioko madarakani. Wanafungwa gavana kupunguzwa kasi. Wanazibwa midomo ya kukemea maovu ya wanaotawala sasa.

Mfano wa wastaafu wa aina hii ni Julius Nyerere, baba wa taifa la Tanzania. Huyu hakuficha hisia zake pale alipoona mambo yanakwenda kombo. Hakustka kuikosoa serikali ya mrithi wake, Ali Hassan Mwinyi kwa mambo mbalimbali hadi akaandika kitabu—Uongozi wetu na hatima ya Tanzania.

Hata ulipofika wakati wa “kijana wake”, Benjamin Mkapa, rais wa awamu ya tatu, Nyerere alijitokeza kukemea mambo yaliyokwenda halijojo. Mfano mzuri ni jinsi alivyokemea uuzaji wa mashirika ya umma ambayo yalikuwa bado yanafanya biashara.

Huo ni upande mmoja wa sheria, ambao kwa baadhi ya watu wa Zambia, wanasema ilitungwa kuwalenga akina Keneth Kaunda na Frederick Chiluba.

Lakini wako wanaosema sheria hiyo ni “takatifu”, kwamba iliwataka wastaafu wapumzike na kula “kuku kwa mrija”. Iliwapa fursa ya kuachana na mikikimikiki ya kila siku ya kisiasa na kula pensheni yao bila usumbufu.

Kwa sheria hiyo, rais mstaafu nchini humo anastahili kunyimwa pensheni, pale inapobainika kwamba anajihusisha na siasa za kila siku.

Lakini, Rais mstaafu wa hivi karibuni nchini humo, Rupiah Banda ni kama alikuwa anapima ukali wa sheria hiyo. Aliposema ataendelea kujihusisha na siasa za kila siku, kukipigania chama chake cha Movement for Multi-party Democracy (MMD), serikali ikatangaza kumbinya kwa  kunyimwa pensheni hiyo. Wiki iliyofuata Banda akatangaza kuachana na siasa za kila siku.

Kwa mantiki ya pili ya sheria hii, kuwaacha wastaafu kupumzika, ni nzuri na kwa maoni yangu inastahili kuigwa hata na Tanzania.

Sioni sababu ya viongozi waliolitumikia taifa letu kwa kipindi fulani, mathalan miaka 10 inayotajwa na katiba, kuendelea kujihusisha na siasa za kila siku.

Viongozi hawa, hawastahili tena kushiriki minyukano ya kisiasa inayoambatana na kutupiana maneno, kulaumiana, kukejeliana na kufedheheshana kwenye majukwaa ya siasa.

Yawezekana hii ndiyo mantiki iliyotumiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwaondoa marais ambao ni wenyeviti wastaafu wa chama hicho, kutoka kwenye vikao vya juu vya chama—Halmashauri Kuu na Kamati Kuu, na kuwaundia Baraza la Ushauri.

CCM wameona hapo ndipo panapowafaa wazee hawa -- kukishauri chama, badala ya kushiriki moja kwa moja katika vikao na kuwa sehemu ya maamuzi. Bila shaka waliona kuwa, jambo hili limekuwa likiwafedhehesha, au linaweza kuwafedhehesha wazee hawa, hasa endapo maamuzi ya vikao husika hayatakuwa mazuri kwa maslahi ya nchi.

Kwa upande mwingine, kwa kuona hilo, serikali ilipeleka muswada bungeni na kutungwa Sheria ya mafao ya Viongozi wa Kisiasa, ambayo iliwatengea fungu nono viongozi wastaafu wa juu, ili wanapomaliza muda wao wa utumishi wasianze kuhangaika kama “watu ambao hawajawahi kulisaidia taifa”.

Pia mafao haya yalilenga kusaidia viongozi wastaafu wasishawishike kirahisi kujiingiza katika vitendo vya rushwa kwa kufikiria “ugumu wa maisha” baada ya utumishi wao (hili sina uhakika linatekelezwa kwa kiwango gani. Linahitaji mjadala mwingine).

Viongozi hawa wastaafu walitengewa mafao haya ili kuwapa nafasi ya kujijenga zaidi kitaifa na kimataifa ili wabaki kuwa kisima cha fikra badala ya kugeuka wachuuzi wa mitaani wakiwa na lengo la kujiongezea kipato na kutafuta utajiri.

Tunayo mifano ya viongozi waliotulia na kuendelea kuthaminiwa kwa elimu na nafasi walizowahi kushika, kama Mzee Mwinyi, Jaji Joseph Warioba, Salim Ahmed Salim, Cleopa Msuya na wengineo.

Lakini kinyume na matarajio ya wengi, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa anaonekana kujitenga katika kundi hilo na hatua ya kujitokeza mara kwa mara katika “siasa za majukwaani”, hasa pale anapotumika katika kukipigia kampeni chama chake cha CCM.

Mkapa ambaye baada ya kipindi cha utawala wake amekuwa akituhumiwa kwa mambo mbalimbali ya kujinufaisha akiwa ikulu, ameshindwa kujizuia kupanda majukwaani. Jambo hili badala ya kumjenga na kumpatia heshima, limezidi kumdhoofisha na kumdhalilisha.

Mathalan, tukio la karibuni la kupanda jukwaani na kumshambulia Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, kuwa anatumia jina la Nyerere kujinufaisha kisiasa, limemfedhehesha.

Katika tuhuma hizo, Mkapa alienda mbali akisema kwa kuwa kwake karibu na familia hiyo na kufanya kazi na Nyerere, hakuwahi kusikia jina la Vincent katika familia hiyo, kauli ambayo imepingwa na familia hiyo, huku ikithibitisha kuwa mbunge huyo ni mwanafamilia. Madaraka Nyerere, alisema Vincent alizaliwa na mdogo wake Mwalimu Nyerere, Kiboko Nyerere.

Kutokana na kitendo hicho, Vincent alipata fursa ya kujibu mashambulizi dhidi ya Mkapa, huku akihoji suala la kifo cha Mwalimu Nyerere ambalo linaweza kuzua hisia mbaya, hasa kuhusu lengo la kiongozi huyo ‘kulazimisha’ Mwalimu apelekwe kutibiwa Uingereza licha ya yeye kukataa.

Nionavyo mimi, Mkapa anatakiwa kusoma alama za nyakati. Ni wakati wa kuanza kukataa kutumika katika majukwaa ya kisiasa. Kwa uwezo wake, bila shaka anatambua madhara ya yeye kusimama kwenye majukwaa hayo, na mbaya zaidi kutumia mdomo wake kutamka maneno yanayoweza kushusha staha yake.

Lakini Mkapa atakataaje wito wa CCM? Chama kimeona hakina mtu mwingine wa kusimama na kukitetea hadharani zaidi yake. Alikwenda Igunga, akakisema kikafanikiwa. Na sasa kimemwomba aende Arumeru Mashariki, angekaataje? Sawa, angeweza kwenda na kutamka maneno yenye sifa za rais mstaafu, siyo yale ya ukada wa chama ambayo yamemrudi na kumwonyesha kama kiongozi asiyefaa kwa kuwa hasemi ukweli.

Kwa hotuba aliyotoa Arumeru wakati wa ufunguzi wa kampeni hizo, imeonyesha dhahiri kuwa kiongozi huyo hana ubavu wa kukataa maombi ya CCM. Pia ametumia nafasi hiyo kukamilisha mkakati wake, kwani mbali na kumnadi Siyoi Sumari, Mkapa alikuwa anatafuta fursa ya kujibu tuhuma dhidi yake.

Amerushiwa tuhuma za kujiuzia Kiwira, kufanya biashara akiwa Ikulu, serikali kuhusika na wizi wa fedha za EPA, ufisadi katika ununuzi wa rada, ndege ya rais na nyingine. Amezinyamazia hadi zikaonekana za kweli.

Nafasi aliyopata sasa aliitumia ipasavyo. Amejitetea na kujisafisha kwa tuhuma za kuwamilikisha ardhi walowezi, na bado anayo mengi ya kueleza.

Lakini kwa upande mwingine, kiongozi huyo amelazimika kutumika kukitetea chama chake kwa kuwa nacho kinamtetea. Serikali ya chama hicho inamhifadhi na kunyamazia tuhuma kibao dhidi yake. Haitaki kuchunguza wala kuchukua hatua. Ni lazima naye alipe fadhila.

Kwa mtindo huu, sisi Watanzania tunaendelea kumlipa Mkapa pensheni kwa ajili ya kukitumikia chama kimoja cha siasa ndani ya mfumo wa vyama vingi. Ni vizuri sheria zikaangaliwa upya ili watu kama yeye wafutiwe pensheni na kuwa huru kuendelea kuwa makada wa vyama vyao.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)