Watoro bungeni ni sawa na wezi, mafisadi waadhibiwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 30 June 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Maoni ya Mhariri

MWANZONI mwa mwezi huu, tulitoa rai kwa wabunge wote kwamba washiriki kikamilifu katika mkutano wa 20 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watoe hoja zenye nguvu.

Tulitoa rai hiyo kutokana na mabadiliko ya ratiba ya vikao vya Bunge kwamba badala ya kuchukua miezi mitatu, mkutano huo ulioanza Juni 8, mwaka huu utakuwa wa wiki tano.
Muda huo umepunguzwa ili kupata muda wa kutosha wa kushughulikia mambo mengine ya kitaifa na hasa uchaguzi mkuu wa viongozi. Bunge hilo linatarajiwa kuvunjwa Julai 16 mwaka huu.

Tunasikitika kusema kuwa pamoja na rai hiyo ambayo tukiitoa kwa nia njema, tumeshuhudia wabunge wengi wakiacha vikao na kurudi kwenye majimbo yao kwa ajili ya kampeni na kugawa zawadi zenye harufu ya rushwa.

Lakini wengine, wamekuwa wakiacha kuingia kwenye vikao vya mkutano huo ili kutazama kwenye televisheni mechi za fainali za Kombe la Duni zinazofanyika Afrika Kusini.

Matokeo yake, baadhi ya vikao vinahudhuriwa na watu wachache kiasi kwamba, naibu Spika wa Bunge, Anne Makinda, Juni 11 alishindwa kuendesha kikao cha alasiri kwa mujibu wa sheria.

Hali hiyo, ilijitokeza pia katika kikao cha kupitisha makadirio na matumizi ya fedha za Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambapo wabunge 105 tu ndio waliohudhuria. Akidi inahitaji nusu ya wabunge.

Baadhi ya vikao vinahudhuriwa na wabunge wachache hasa walijioandikisha kwa ajili ya kuchangia hotuba za mawaziri. Uchache wa wabunge umesababisha baadhi ya makadirio ya matumizi ya wizara kukosa akidi ya wabunge wa kupitisha maombi ya wizara kama wizara iliyotajwa hapo juu.

Sisi tunajiuliza, hivi kweli, fainali za Kombe la Dunia ni muhimu kuliko Bajeti ya Serikali? Hivi wabunge wasingeweza kuona marudio ya mechi hizo kwenye vyumba vyao, baada ya majukumu ya kitaifa?

Hivi ni kweli, kipindi hiki muhimu ndicho cha kurejea kwenye majimbo kugawa pikipiki, baiskeli na kupanga mipango ya maendeleo kwa mwaka 2010/11? Je, huu si wizi wa muda? Walikuwa wapi muda wote hadi saa ya mwisho ndipo wanakurupuka na kwenda kugawa ‘rushwa’?

Tunatoa wito kwamba wabunge wanaopita pita kutoa zawadi, kugawa pikipiki, baiskeli katika kipindi hiki cha Bunge la mwisho katika uhai wake waadhibiwe kwa kutochaguliwa kwani ni sawa na wezi, mafisadi na wasiolitakia mema taifa.

Hawa ni wachumia tumbo, wanajali maslahi yao na si kazi ya uwakilishi bungeni na kutatua kero za wananchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: