Wazanzibari msidanganyike, semeni NDIYO


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 21 July 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Kalamu ya Jabir

RAIS Amani Abeid Karume anataka kuhakikisha dhamira yake inatimia. Dhamira gani hiyo? Kujenga siasa za maridhiano katika visiwa vya Unguja na Pemba kabla ya kuachia madaraka mwisho wa mwaka huu.

Ni dhamira aliyoiweka mwenyewe. Alikuwa na sababu zake. Angali nazo hata sasa, miezi minane tangu pale alipoamua kuzungumzia umoja na mshikamano wa kweli na amani na utulivu imara.

Hili lilithibitika 5 Novemba mwaka jana alipokutana kwa faragha na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, Ikulu ya mjini Zanzibar.

Mazungumzo yao yalitandika msingi imara wa kuanza kwa hatua za kuleta mabadiliko ya mfumo wa utawala Zanzibar, nchi ya visiwa iliyoathiriwa na migogoro na mivutano kutokana na siasa chafu zilizochochea chuki na uhasama miongoni mwa wananchi.

Hali mbaya imezidi tangu ulipofanyika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, baada ya mfumo huo kurudishwa. Zanzibar ilikuwa na siasa za ushindani tangu miaka ya 1950 wakati wazalendo wakitamani kujitawala.

Katika hali hiyo ya migogoro na mivutano, Rais Karume anajua fika kuwa wapo viongozi wenzake Zanzibar wasiopenda mpango wa kujenga siasa za maridhiano.

Anajua kwamba wanachukia kila wanaposikia mafanikio katika hatua mbalimbali za kuutekeleza. Anajua wanaupinga mpango huo na wanampinga yeye binafsi kwa hatua zake. Anajua wanakasirika na wanachukua hatua kumkwamisha.

Isitoshe, anajua pia kuwa baadhi ya wapinzani wa mpango wake huo, ni wasaidizi wake katika chama – yeye pia ni makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar – na katika serikali anayoiongoza.

Tena wapinzani hao ni watu aliowateua mwenyewe kumsaidia kazi ya kujenga nchi, wakiwemo wale aliowateua tangu alipoingia madarakani mara ya kwanza mwaka 2000, baada ya uchaguzi.

Kwa kulijua hilo, anaendelea kuwasema na kuwalaumu. Anawataja kuwa ni watu wabaya wasioipenda nchi yao na wananchi wenzao.

Lakini huyu ni kiongozi anayeonyesha ushupavu. Tayari amefanikiwa kushinda vikwazo vingi vilivyojitokeza katika mpango huo ambao tamati yake itaanza na uundaji serikali ya umoja wa kitaifa. Serikali hii itatokana na vyama vitakavyoshiriki uchaguzi ujao.

Sasa kipo kikwazo kingine. Hiki ni kura ya maoni inayolenga kupata sauti ya wananchi kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya mfumo wa utawala yaliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi kufuatia hoja binafsi iliyowasilishwa na kiongozi wa upinzani barazani, Abubakar Khamis Bakary (mwakilishi wa Mgogoni, Pemba).

Kura hii itapigwa tarehe 31 Julai hii (Jumamosi ya wiki ijayo) chini ya usimamizi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Ni fursa kwa wananchi wote walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar ya kufanya uamuzi wa wanachokitaka.

Mgawanyiko ndani ya CCM umechochea upinzani kuhusu mpango wa Rais Karume. Lipo kundi halitaki mabadiliko na linaeneza kampeni ya kuyapinga wakitaka wananchi waseme HAPANA.

Sababu zao ni za kibinafsi zaidi kuliko kufikiria mustakbali wa kweli wa nchi yao. Wanasingizia eti mabadiliko hayo yatafuta mapinduzi ya 12 Januari 1964. Bali hawaelezi kama mapinduzi hayo yamekwama kutimiza malengo yake kutokana na mivutano yao na kati yao na vyama vya mageuzi.

Karume anaendelea kushika kijiti na kuonyesha njia. Anawasema na kuwasema wanaompinga. Anataka wananchi wawashangae viongozi wanaojali zaidi maslahi binafsi kuliko kutangulia kuweka mbele maslahi ya nchi na wananchi wake.

Ushahidi wa namna wasaidizi wake wanavyomsaliti, ni mawaziri wake wengi kutomuunga mkono katika mpango wake huo.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa ni mawaziri wawili tu katika serikali anayoiongoza wanaunga mkono kura ya maoni. Ni Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman.

Wanaeleza wazi ni muhimu wananchi wapige kura ya NDIYO ifikapo 31 Julai. Kauli zao zimo kwenye hotuba za makadirio ya matumizi ya mwaka wa fedha wa 2010/11 kwa wizara wanazoongoza.

Wanasema dhana ya maridhiano imeletwa na CCM wenyewe walipopitisha azimio la kutaka hoja ya mabadiliko ya kiutawala Zanzibar ipelekwe kwa wananchi.

Ni CCM walioazimia muafaka kati yao na CUF upelekwe kwa wananchi chama hicho kilipofanya vikao vya juu kijijini Butiama, Machi mwaka 2008.

Kwa hivyo, wanasema ni jukumu la kila kiongozi wa serikali na CCM kuhimiza wananchi wapige kura ya NDIYO siku itakapofika. Kuwa muwazi ni kujiheshimu.

Akihutubia wanachama wa CCM wa mikoa miwili ya kisiwani Pemba katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Gombani ya Kale, nje kidogo ya mji wa Chake Chake, Jumamosi wiki iliyopita, Rais Karume alisema:

“Lugha ya hapana inastahili kusikika katika kampeni ya kuondoa malaria, dawa za kulevya, kuvuta bangi. Haya ni maradhi hayafai umoja tunauhitaji nchini. Hatuwezi kukataa amani na utulivu (wa kweli) ndio maana nitawashangaa wote watakaokataa serikali ya umoja wa kitaifa.”

Alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa kupokea mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, na mgombea mwenza wa Jakaya Kikwete katika uchaguzi ujao wa rais Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Tabaan, Zanzibar haiwezi kurudi nyuma kwani kufanya hivyo ni sawa na binadamu kupigana na upepo akitumainia ashinde. Haiwezekani.

Dhamira njema ya maridhiano ambayo Rais Karume na Maalim Seif waliafikiana kuijenga na vyama vyao kuidhinisha, lazima ipewe nguvu na kila mpenda umoja na mshikamano; nguzo ya maendeleo ya jamii.

Dhamira yao hiyo imeshabadilisha hali ya mambo. Ile tu wao viongozi wakuu wa vyama kuafikiana kushirikiana; kusameheana na kuendeleza maridhiano imeleta utulivu mkubwa.

Sasa watu wameanza kufuata; wanaminiana na kushirikiana.

Wanajua wanatakiwa kupiga kura ya NDIYO ili kuidhinisha mabadiliko yaliyokusudiwa kwa ajili ya maslahi yao na nchi yao. Kwao hilo wala si mtihani unaowahangaisha.

Tatizo ni vipi sauti zao zitatafsiriwa pale ikiingia magharibi ya siku ya kupiga kura. Pita kote Unguja na Pemba, unachosikia watu wanakisema ni kutii viongozi wao hao wawili.

Wanajua kuridhiana na kushikamana kati ya watu katika jamii yoyote ile, ni msingi muhimu wa kufikia maendeleo. Nani wa kuwarudisha nyuma? Asilani abadan.

Katika hilo, wala hawajali kama wamepewa elimu ya vipi wapige kura. Wazanzibari ni weledi kwa kushiriki uchaguzi. Wanajua wanachokitaka. Hawahitaji visingizio.

Kazi ni moja tu tarehe 31 Julai: Kuweka alama kwenye kisanduku cha NDIYO. Na huo ndio uamuzi wa kujenga dhamira njema.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: