Waziri Sitta ‘anakaa kwa Makinda?’


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

WAZIRI wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta amekuwa sehemu ya mjadala bungeni. Ni kuhusu nyumba iliyokodishwa na serikali kwa ajili ya makazi maalum ya spika wa bunge.

Nyumba hiyo ipo Barabara ya Buzwagi, Masaki, Dar es Salaam, ilikodishwa na serikali kwa ajili ya makazi rasmi ya spika, lakini bado inaendelea kukaliwa na Sitta.

Mjadala juu ya Sitta kung’ang’ania nyumba ya serikali, uliibuliwa bungeni Alhamisi, wiki iliyopita, na Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA, Iringa Mjini).

Alimuuliza waziri mkuu kupitia kipindi cha maswali ya papo kwa papo, ni lini Sitta ataondoka katika nyumba hiyo aliyodai imekodishwa kwa dola 8,000 za Marekani (zaidi ya Sh. 12 milioni) kwa mwezi.

Fedha hizi ni nje ya malipo ya gharama za kila siku za mafuta kwa ajili ya uendeshaji wa jenereta pamoja na umeme, maji na walinzi.

Hata hivyo, Pinda hakupata fursa ya kujibu swali hilo. Lilijibiwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye hivi karibuni amejipa jukumu la kujibia serikali.

Alisema, “Ndiyo maana wakati mwingine mnanisema najibia serikali, wala Pinda swali hili halimhusu. Malipo ya spika mstaafu hayafanywi na serikali. Yanafanywa na Bunge. Sitta anaishi katika nyumba hiyo kwa kuwa yeye ni spika mstaafu….”

Lakini si sahihi kwa Sitta kuendelea kuishi kwenye nyumba iliyoandaliwa maalum kwa makazi ya spika, wakati yeye si spika.

Sababu ni nyingi: Sitta hajastaafu wadhifa wa spika, bali aling’olewa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi ndani ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hii ilikuwa baada ya Kamati Kuu (CC) kuibuka na sifa ya ziada ya kutaka spika mwanamke; sifa ambayo Sitta asingeweza kuipata.

Sitta hakuelezwa hilo na chama chake kabla na baada ya kujitosa katika kinyang’anyiro hicho. Wala hakuelezwa asichukue fomu au aondoe jina lake kama ilivyofanyika kwa nafasi nyingine ikiwamo ya naibu spika.

Angalau hayo yangefanyika na akatangaza kutogombea, pengine ingeweza kuhalalisha hicho kinachoitwa na Makinda, “Sitta spika mstaafu.”

Kama ilivyo kwa Edward Lowassa kwamba hakustaafu, bali alilazimishwa na Bunge kujiuzulu baada ya kutuhumiwa kuingiza nchi katika mkataba tata wa Richmond, ndivyo ilivyo kwa Sitta.

Hata kama wapo watakaoleta utetezi na kumuita Sitta “spika mstaafu” na hivyo kustahili kupata anachopokea, bado utetezi huo hauwezi kuhalalisha kinachotendeka.

Sheria ya mafao ya viongozi wastaafu wa siasa haisemi mahali popote spika mstaafu anapewa nyumba na serikali. Sheria inatamka spika mstaafu kupewa gari moja ambalo atalihudumia mwenyewe, na dereva.

Gari hilo litahudumiwa na bunge kwa matengenezo; na atapewa lita 70 za mafuta kwa ajili ya gari hilo.

Lakini Sitta ni mbunge wa Bunge la Muungano. Kwa nafasi hii, kila mwezi analipwa na serikali lita 1,000 za mafuta kwa bei ya Sh. 2,500 kwa lita.

Serikali inamlipa posho za kujikimu kwa kila anapokuwa kwenye mikutano ya Bunge au kamati za bunge. Hili si kwa Sitta pekee. Mawaziri wote na manaibu wao wanalipwa posho ya vikao vya bunge.

Mawaziri na manaibu wanapewa gari na serikali, wanapewa nyumba; na kwa wale wanaoishi katika nyumba zao, hulipwa na serikali fedha kama fidia ya gharama za nyumba.

Kisichofahamika wazi, ni iwapo Sitta analipwa na serikali fedha za nyumba, wakati yeye tayari anaishi katika nyumba ambayo gharama zake zinalipwa na bunge.

Inawezekana kama spika Makinda angempa fursa waziri mkuu kumjibu Mchungaji Msigwa, labda haya yangeweza kufahamika.

Lakini kinachofahamika ni hiki: Serikali imemuuzia nyumba mke wa Sitta, Margareth. Nyumba ya Mama Sitta iko Oster Bay, Dar es Salaam. Haikaliwi na Sitta. Yeye na mkewe wanaishi katika nyumba ya serikali.

Tatizo la Sitta ni kule kuwa na sura mbili. Sura ya kutaka kuonekana mtetezi wa maslahi ya wanyonge, lakini papo hapo akiishi maisha ya anasa.

Hata mjini Dodoma, Sitta anaishi katika nyumba ileile yenye hadhi ya spika, badala ya kuishi kule wanakoishi mawaziri wenzake.

Lipo jingine: Uamuzi wake kung’ang’ania nyumba ya serikali umehalalisha uamuzi wa Makinda kuendelea kuishi katika nyumba yake binafsi, jambo ambalo linaigharimu sana serikali.

Kwa uamuzi huo, serikali imelazimika kumpa fedha Makinda ili kukarabati nyumba yake iliyoko Kijitonyama ili iweze kuendana na hadhi ya cheo chake.

Taarifa zinasema tayari uamuzi huo wa Sitta umeibua mgogoro kwa Makinda. Baadhi ya majirani zake wanamlalamikia kufunga barabara ili kuifanyia matengenezo nyumba yake.

Kimsingi, hakuna utetezi unaoweza kuhalalisha hatua hii. Kama serikali inataka kutekeleza kaulimbiu yake ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania,” sharti iachane na utamaduni wa kila aliyestaafu kuruhusiwa kubaki katika nyumba aliyokuwa akiishi awali.

Hili likiruhusiwa, taifa litalazimika kila baada ya miaka mitano au kabla ya hapo, kujenga makazi mapya ya viongozi wake wapya wanaoingia madarakani. Gharama zilioje!

Kwa mfano, serikali italazimika kujenga ikulu mpya kwa kuwa iliyopo itaendelea kukaliwa na Rais Jakaya Kikwete. Italazimika kujenga makazi mapya kwa waziri mkuu kwa kuwa Pinda ataendelea kuishi anapoishi sasa.

Italazimika kujenga makazi kwa ajili ya makamu wa rais, kwa kuwa haya ya sasa yataendelea kubaki mikononi mwa Dk. Mohammed Gharib Bilal hata baada ya kustaafu. Hii ni hatari kwa uchumi na maslahi ya wananchi.

Utaratibu wa sasa wa posho na mafao una upogo. Kuna wanaopata mishahara mara mbili. Kwa mfano, wabunge wanaotokana na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, wanalipwa mishahara Zanzibar na wanalipwa kwenye Bunge la Muungano. Wanalipwa posho za mafuta Zanzibar na wanalipwa Bara.

Yanahitajika mabadiliko. Wala si kwa Sitta pekee; kwa mawaziri, wabunge na watendaji wakuu serikalini. Keki ya taifa haigawanywi sawa.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: