Wezi wa Dowans hawa

MAFISADI watatu waliojipanga kuchota Sh. 185 bilioni kutoka serikalini, zikiwa fidia kwa kuvunja mkataba wa kampuni ya kufua umeme ya Dowans, wamefahamika.
Vyanzo mbalimbali vya habari ndani ya serikali na nje ya nchi, vinawataja wanaojiita wamiliki wa Dowans kuwa wote ni Watanzania.
Tarehe 15 Novemba mwaka huu, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC), iliagiza Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) kulipa fidia ya Sh.185 bilioni kampuni ya Dowans Holding Tanzania Limited.
Wanaojiandaa kuchukua kitita hicho wametajwa kuwa ni pamoja na mfanyabiashara mmoja nchini ambaye pia ni mbunge. Mwingine ni mwanasiasa mmoja aliyewahi kushika madaraka ya juu serikalini.
Anayetajwa kuwa mmiliki wa tatu wa Dowans, ni wakili mashuhuri nchini ambaye amewahi kutetea serikali katika kesi mbalimbali na mwenye mahusiano na makampuni ya uwakili nchini Uingereza.
MwanaHALISI lina majina yote ya wamiliki watatu, lakini linayahifadhiwa kwa sasa hadi hatua muwafaka za serikali ziwe zimechukuliwa.
Ili wamiliki hao waweze kutapa fedha hizo, sharti kwanza hukumu ya ICC juu ya kesi hii, isajiliwe katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Lakini waziri mmoja mwandamizi katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ameliambia MwanaHALISI kuwa ama usajili utachukua muda mrefu au utashindikana kufanywa kutokana na sababu mbili.
Kwanza, miongoni mwa wamiliki kuna wawili ambao hawataki, piga ua, majina yao yahusishwe na Dowans kwa kuwa wako karibu na kile kinachoitwa “jikoni.”
Hawa wangependa kutumia ushawishi ili walipwe fedha hizo bila kufuata utaratibu wa kusajili hukumu mahakama kuu, au ikibidi, basi “fedha hizo zipotee.”
Pili, wangependa kukamilisha mradi wao wa kusajili Dowans katika moja ya nchi za nje ambako iliwahi kudaiwa miaka mitano iliyopita kuwa ndiko ilisajiliwa.
Nchi hiyo imetajwa kuwa ni Costa Rica.
“Hatua yeyote ya kuisajili kesi hii katika mahakama za ndani, itasababisha kufumka kwa msululu wa mambo yaliojificha. Hata wamiliki halisi wa Dowans watajulikana,” ameeleza waziri huyo.
Kufahamika kwa wamiliki wa Dowans, kumekuja siku tatu baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kueleza wahariri wa vyombo vya habari nchini kuwa Dowans ni “genge la watu wachache wanaofahamika.”
Hata hivyo, Pinda hakutaja majina ya wamiliki hao, badala yake alisema wamiliki hao ni wale walioamua kutafuna rasilimali za taifa bila huruma.
Pamoja na kujua hivyo, Pinda hakusema ni hatua gani serikali itawachukulia watu hao, isipokuwa alisema, ikibidi serikali italipa fedha hizo.
Aidha, kufumuka kwa taarifa za wamikiki wa Dowans, kumekuja wiki mbili tangu spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta kunukuliwa akisema, “Dowans ni genge la watu watatu wanaotaka kutumia fedha hizo kutafuta urais mwaka 2015.”
Kauli za Pinda na Sitta zinaonyesha kuwa wahusika wanafahamika vema. Lakini hakuna hata mmoja wao ambaye anataja majina yao.
Kufahamika kwa “matajiri” wa Dowans kwa Pinda na Sitta kuna maana kwamba kunafahamika pia kwa Rais Kikwete ambaye ni mteule wao; vinginevyo wangekuwa wanahujumu serikali yake kwa kujua jambo kama hili na kushindwa kumwambia.
Wachunguzi wa mambo wanasema kauli za viongozi hao wawili zinaweza kuwa zinalenga kumshawishi Rais Kikwete kujenga ujasiri na kuwataja hadharani kabla wao hawajamuumbua.
Hata hivyo, kujulikana kwa vigogo wa Dowans, kumekuja siku tatu baada ya Edward Hoseah kuripotiwa na vyombo vya habari vya nje, akimtuhumu Rais Kikwete kuwakinga watuhumiwa wa ufisadi nchini.
Mkurugenzi mkuu huyo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), amenukuliwa na mtandao wa WikiLeaks akisema, “Kikwete amekuwa mgumu kushughulikia viongozi wa serikali na wale wa vyombo vya dola wanaotuhumiwa kwa rushwa.”
Mtandao wa Wikileaks ulinukuu mazungumzo kati ya Hoseah na mwanadiplomasia mmoja wa Marekani, Purnell Delly akidai, “Kikwete hataki kuwa wa kwanza kuweka utaratibu wa kuwafikisha mahakamani viongozi wa zamani kwa makosa waliyofanya wakiwa madarakani.”
Madai hayo ya WikiLeaks yalichapishwa katika gazeti la The Guardian la Uingereza, juzi Jumamosi.
Kauli inayodaiwa kuwa ya Hoseah kwa Delly, inaelekea kuthibitishwa na msimamo wa Kikwete alioutoa kwa wahariri wa vyombo vya habari mwanzoni mwa mwaka 2007 pale aliposema, “Si vema kuanza kuwachimbua viongozi wastaafu.”
Rais Kikwete alikuwa akijubu swali lililoulizwa na MwanaHALISI, iwapo serikali yake inaweza kumchukulia hatua, mtangulizi wake, rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa tuhuma za kufanya biashara akiwa ikulu; jambo linalopingana na utawala bora.
Katika mazungumzo yake na Delly, Hoseah andaiwa kusema, “Unapotaka kushughulika na viongozi hawa wakubwa, inajengwa picha kwako kwamba unachotaka kukifanya ni jambo la hatari…Hao unaotaka kuwashughulikia ndiyo waliokupa wadhifa…”
Mjumbe mmoja wa Kamati Teule ya Bunge ya Richmond ameliambia MwanaHALISI juzi Jumatatu, kamati yake inaweza kuthibitisha kwamba “Richmond na hata Dowans ni makampuni feki.”
Amesema Bunge liliwahi kujulishwa na Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Costa Rica, ambaye ndiye Msajili wa Makampuni, Mei 2008 kuwa katika nchi hiyo hakuna kampuni yenye jina Dowans Holding SA Limited.
Msingi mkuu wa kupinga malipo kwa Dowans, ni kuvuja kwa taarifa zinazoeleza kuwa hadi Aprili 2010, hakukuwa na kampuni ya aina hiyo nchini humo; kuibuka kwa Dowans kulikuja mwaka mmoja baada ya serikali kuvunja mkataba.
Taarifa zinasema, tayari baadhi ya wanasiasa wakiwamo viongozi wandamizi serikalini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani, wamejipanga kuhakikisha kampuni hiyo hailipwi mabilioni hayo ya shilingi.
Waziri mwingine ndani ya serikali ya Rais Kikwete ameliambia MwanaHALISI, juzi Jumatatu, “Nakuhakikishia Dowans haitaambulia chochote. Kama chama kupasuka, basi kipasuke.”
Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na jopo la wasuluhishi, Gerald Aksen, Swithin Munyantwali na Jonathan Parker, Serikali inatakiwa kuilipa Dowans dola za Marekani 24,168,343 na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka.
Malipo mengine ni dola 19,995,626 ambazo zinatakiwa kulipwa tokea 15 Juni 2010 hadi fidia hiyo itakapokuwa imelipwa.
Kiasi kingine ni cha dola 39,935,765 na riba ya asilimia 7.5; na dola za 36,705,013.94 ambazo zinatakiwa kulipwa kuanzia 15 Juni 2010 na dola 750,000 ambazo zinatakiwa kulipwa kwa wasuluhishi.
Dowans wanatakiwa kulipwa kiasi kingine cha dola 1,708, 521 ikiwa ni gharama za uendeshaji wa kesi.
Katika mazungumzo yao, Delly anamnukuu Hoseah akikiri kuwa rushwa ilitumika katika ununuzi wa rada ya kijeshi iliyonunuliwa wakati wa utawala wa Mkapa.
Anasema taasisi yake imegundua kufanyika ufisadi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), lakini wahusika wanalindwa na Kikwete.
Wakati Hoseah akizungumza na Delly mwaka 2007, tayari kashfa ya ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya BoT, tayari ilikuwa imefumuka.
Hadi leo watuhumiwa wakuu wa wizi katika EPA, akiwamo mmiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, ambayo ilichota zaidi ya Sh. 40 bilioni, ama hawajakamatwa au hawajafikishwa mahakamani.
Katika mazungumzo yake na Delly, Hoseah anadaiwa kusema miongoni mwa wahusika wakuu katika kesi ya rada, ni maofisa wa wizara ya ulinzi pamoja na maofisa wa ngazi za juu katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWT).
“Hoseah alisema pasi na kuficha kuwa kesi zozote zinazomhusu rais au waziri mkuu hazijadiliki. Zinawekwa kapuni. Na wale wote walio karibu nao huwa hawagusiki,” inasema taarifa hiyo ya Delly kwa serikali ya Marekani.
“Kama utahudhuria mikutano iliyoandaliwa na hao watu wa karibu na rais au waziri mkuu, utaona wana tabia ya kuonyesha kwamba, bila wao wewe si chochote na kama utawageuka, basi maisha yako yatakuwa hatarini,” Hoseah amedaiwa kusema kwa mujibu wa WikiLeaks.
Akizungumzia madai hayo ya Hoseah, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyamamu alisema kama kweli mkuu huyo wa TAKUKURU aliyasema hayo, basi hakusema ukweli.
Alisema Rais Kikwete amefanya makubwa katika kupambana na rushwa kuliko rais mwingine yeyote aliyepita, na ushahidi wa takwimu na hali halisi unathibitisha hilo.
Alisema idadi ya kesi za watuhumiwa wa rushwa imeongezeka mahakamani, huku TAKUKURU ikiongezewa meno, utaalamu na bajeti yake ikipanda kuliko wakati mwingine wowote.
Hata hivyo, Salva aligoma kuzungumzia kauli ya Kikwete ya kulinda viongozi wastaaafu.
“Sasa sijui mlitegemea mheshimiwa rais afanye nini zaidi ya hapo. TAKUKURU imepewa kila kitu na imepewa meno; au mlitaka rais aende mwenyewe kukamata watu ndiyo juhudi zake zionekane,” alisema Salva akijibu madai ya Hoseah.
Alisema, “Kama hilo ndilo mnalolitaka haliwezekani. Rais ni muumini mkubwa wa utawala wa sheria ambao unaviachia vyombo na taasisi za kisheria kufanya kazi zake.”
Tayari ubalozi wa Marekani nchini umefanya uchambuzi wa mazungumzo kati ya Hoseah na Delly kubainisha kuwa inawezekana mkuu huyo aliamua kufuatilia rushwa katika suala hilo la rada kwa vile tu Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO) ilimletea mafaili yenye taarifa zisizo na shaka kuhusu suala hilo.
Taarifa ya Hoseah inachukuliwa na wachambuzi wa mambo ya kisiasa kuwa Rais Kikwete anamfahamu mmiliki wa Dowans, lakini anashindwa kumchukulia hatua kwa kuwa anahusishwa na mmoja wa maswahiba zake.
tanzania ni nchi yenye amani kwa sababu watu wake hawajui haki zao, laiti wangelijua ni nini viongozi wao wanafanya nadhani maandamano yasingeisha. Dowans hakuna kulipwa hizo fedha.
Sasa umefika wakati kwa watanzania kuamka.Tusiache taifa letu liangamie kwa sababu ya watu wachache wenye roho za kinyama.MUNGU anlipenda taifa letu ndio maana amewainua MWANAHALISI ili kufichua maovu yaliyojificha.Dowans ni zigo lisilobebeka na kuvumilika.MUNGU wabariki Mwanahalisi kwa kazi yenu.
Majina hayo si mageni na kila mtu anayafahamu, labda tu huyo mwanasheria mkongwe namhisi kama mtu wa musoma vile?! Anyway, all in all, tunaomba serikali isilipe fedha hizo. Pili, Rais aseme wazi wahusika na wafilisiwe kila kitu kwa uhujumu walioufanya. Katiba mpya lazima itoe fursa ya kuundwa Tume huru ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mkurugenzi wake asiwajibike kwa tu yeyote ila kwa Bunge na Tume iwe na uwezo wa kupeleka hoja Bungeni ya kumwondolea kinga Rais iwapo atafanya madudu kama haya!! Hapo ufisadi utapungua kama siyo kuisha kabisa!!
KIKWETE ANATUSIKITISHA SANA KWA KUWA MTAWALA MBOVU NA MLINDA MAOVU NA UDINI.
Najua inauma sana, lakini muhimu sana usipoteze umakini ili hasara isiwe kubwa zaidi. Kutaja majina ya watu peupe tutaponzana mkuu.Wenyewe ukiwgusa tu na wakapata nafasi ya kukutesa hawata acha.
Nawapongeza Mwanahalisi sana kwa kazi ya kulinusuru Taifa hili teule la Afrika.
Binafsi sioni kama ninaweza eleza yote yaliyo moyoni mwangu kwani zitakuwa kurasa zisizohesabika. Tayari kazi hiyo iko mikononi mwenu na langu ni kuzidi kununua makala kwa ajiri yangu na pia kwa rafiki zangu. Kilia nayepata kulisoma mwanahalisi hatoweza kuacha nunua mpaka mwisho wa maisha yake. Na hii iwe ndio kampain kwani zipo nayakati zaja fisadi mmoja tanunua nakala milioni azichome ili zisiwafikie wananchi.
Mwanahalisi ni gazeti teule na ninafikiri ni gazeti pekee la karne kwa nchi ya Tanzania na zaidi afrika ya Mashariki.
Mungu yupo pamoja na nyie na hakuna jambo lolote mwanadamu atweza watenda. Ninani iliyetoa uhai wake kwa taifa?Ni nani yupo tayari kuachana na pesa za hongo kwa ajiri ya mtu mwingine?Bila shaka si kwa uwezo wenu bali Mungu ailiyetugawia vipaji na hilo ndio kusudi hasa. Tujuze habari na taifa litapona.
Nitamwelezea Saed Kubenea kama mwanaharakati bora wa karne hapa Tanzania.
Heko Mwanahalisi na harakati zitaendelea, msiogope asema Bwana Mungu!
ccm is soon going to be 185 bn richer!!! hii ni hela ya chama! jaji werema kasema hela italipwa na teyari tanesco wameishafungua akaunti ya kukusanya hela hizi!
weeeezi wakubwa hawa hawana haya hata kidogo. wanafikiri hizo fedha watakufa nazoooo? wanatusababishia maisha magumu yasio eleweka wenzao huku wao wakikosa hata pa kuzipeleka pesa hizo. EEEH MUNGU TUNAKUOMBA CHUKUA ROHO ZAO HAO WOOOTE WATATU ILI TUSALIMIKE NA UDHALIMU WAO. INSHAALHA.
TUCTA na CHADEMA wanataka kuandamana. Wanataka kupinga utawala mbovu. Na hata CUF wana msimamo kama huo. Na watanzania wote kilio ni hicho hicho. Ni sawa! Lakini jamani, hivi watanzania tungepiga kura kwa uangalifu, tungekuwa na sababu ya kuandamana? Si tuliyataka wenyewe? Tulipiga kura kama vipofu, sasa tunalalama kama vichaa! Na bado tutaandamana kama vipofu na kujikuta tunajikuna maji ya kuwasha kama vichaa!
Watanzania kilio cha nini? Hivi kweli maaandamano tu ni suluhisho? Suluhisho lilikuwa ni kura zetu. Lakinmi kwa ajili ya vitisheti na vikofia vya njano tukakosea! Tukakumbatia utawala mbovu na kuurudisha madarakani. Sasa tukubali tulikosea, tufikiri upya!
Kama kweli ipo nia thabiti ya kupinga utawala mbovu, dawa madhubuti kwa sasa ni migomo ya nchi nzima kila kona ya nchi, hiyo ndiyo funga kazi! Maandamano hayana tija! Si mtaambulia maji ya kuwasha tu? TUCTA walipanga kugoma miezi kadhaa iliyopita, wakatishwa, wakanyamaza! Sasa wanaparamia maandamano. Kwa maoni yangu, iwapo migomo haiwezekani, basi watanzania kaeni kimya mnyolewe vizuri! Maandamano tu sio suluhisho!
Ni afadhali hiyo bei ya umeme ingepanda kwa asilimia mia na saba ili tupate akili, kwa kuwa siasa za Tanzania zimekuwa mithili ya ushabiki wa Yanga na Simba bila kuangalia uhalisia wa maisha. mak.ralph@yahoo.com
Hongera Ndugu yangu.Ama hakika nakubaliana na wewe na umesema kweli hasa.Lakini kidogo niongezee ukweli wako ndugu yangu,Wanaojua na wenye uwelewa nchi hii ni kidogo sana.Na kwa udogo wetu huwa tunaambulia kuandika kwenye magazeti tu.Walio wengi ni hawa wanao vaa nguo za msimu za kugaiwa.Haidhuru ndio wanao athirika na maisha,lakini wapi Yaliomwagika hayazoleki.Sasa la kufanya tusichoke na tuwaombe waanahabari watembelee mashuleni na wazishawishi taasisi za elimu ziweke somo kwenye mitaala yao kuhusiana na Ufisadi na Mafisadi.Huenda baaadae wenetu wakaamka kwenye usingizi mzito tulionao sisi watu tulio kwenye umri wa kuanzia miaka 18....
NDUGU YANGU KUBENEA KWANZA NAKUPONGEZA PILI NAOMBA UWE MWANGALIFU SAAANA, HAWA WATU SIYO WAZURI.
kweli Tanzania imeoza na matatizo haya yanatokana na upeo mdogo wa viongozi wetu.Kila kiongozi ana husika kwa namna moja ama nyingie ktk kudidimiza uchumi wa taifa ili wanufaike wao.Mifano ipo hai Mitambo ya Songas ilikuwa mali ya Tanesco wakaiuza kwa songas kisa eti Tanesco hawakuwa na haja ya kuitumia kwa wkt ule sasa mitambo hio hiyo ndo sisi tunalipishwa hela nyingi kwenye garama za umeme kufidia ujinga wa viongozi waliouza.Pili IPTL na mikataba yake ilifanikishwa kwa kiasi kikubwa na mtemi wetu wkt huo akiwa waziri,Kiwira nayo badala ya kuibinafsisha kwa wawekezaji wa Afrika Kusini wakaamua kuichukua wao yaani mzee wa kusini na huyu baba wa kipare ambae ana kesi wkt wakijua uwezo wa kuzalisha umeme hawana na tenda wakaifuta mara moja, hili la Dowans lipo wazi kampuni mfu wanataka kutuibia wakidhani watanzania wote ni wajinga na hatuna elimu yoyote.Ipo siku itawatokea puani na kuwapasua matumbo yao.Za mwizi ni arobaini Mda wa kukaa gizani na kuacha nchi iliwe na wachache umetosha sasa.Tumekichagua chama chetu kitawale tena kumbe tunajitia kitanzi cha mwisho hivi mbona hatuamki tu? wizi wizi mpaka lini?
Kweli nchi inaliwa na wajanja fulani. Kwa maelezo hayo ni bora copy ya hukumu ikalindwa ili isichakachuliwe ikija kuwa balaa. Naomba kama MH lina nakala ya hukumu hiyo liitunze pindi ikichakachuliwa tu iwekwe jamvini kwa mustakabali wa taifa.
Hapa mwanahalisi hamjasema wala kuwataja hawa mafisadi ila, hapa kuna Rostam Azizi, Lowassa na Nimrodi Mkono. Hawa ndio wezi waTanzania. Ila wajue kuwa: This time imekula kwao.
Kumbe Tunawajua, Tuwapige mawe barabarani kama KIKWETE hataki kuchukua hatua