Ya TFF na makocha wa ughaibuni

TIMU ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20, inahujumiwa. Mhujumu mkuu ni Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).
Katika wiki mbili zilizopita, timu ya vijana imehujumiwa mara mbili.
Kwanza, kocha wake Rodrigo Stockler alikimbilia Kenya “kuona michuano ya Chalenji” badala ya kubaki Dar es Salaam kutafuta vipaji kutoka michuano ya timu 12 za vijana.
Michuano ya Chalenji ilichezwa nchini Kenya kwa muda wa wiki mbili. Ilianza 28 Novemba na kumalizika 13 Desemba, wakati ile ya vijana chini ya miaka 20 ilianza 29 Novemba na kumalizika 13 Desemba 2009.
Ni hivi: Hapa kuna mashindano ambamo kocha anatakiwa achague wachezaji kwa ajili ya timu ya taifa. Kocha mwenyewe hayupo!
Safari yake, licha ya kutokuwa na umuhimu kwa timu yake, haikuwa ya dharura wala yenye sababu za msingi. Utalii tu.
Pili, TFF ilipanga mashindano ya timu za vijana yafanyikie kwa wiki mbili tu, ilhali vijana wapo kwenye usajili wa msimu mzima.
Aidha, kwa kuwa TFF ilikuwa haifuatilii kuona iwapo timu hizo za vijana za klabu zipo kweli, tumeshuhudia klabu zikileta timu ambazo zimecheza tu kwa ajili ya kutimiza wajibu na bila maandalizi yoyote.
Kocha Stockler, raia wa Brazil alikwenda Kenya, akiambatana na “nduguye” Marcio Maximo anayeinoa timu ya taifa ya Tanzania Bara “kushuhudia” michuano ya Chalenji. Huu ni utalii wa aina yake.
Hivi kulikuwa na umuhimu wa Kocha Stockler kwenda Kenya akiyaacha mashindano yake yanafanyika? Kuna kazi gani aliyokwenda kuifanya? Jukumu lake la kuangalia vipaji vya vijana alimwachia nani?
TFF ndio bosi wa Stockler; sasa kama si wao ni nani mwingine alimruhusu kwenda kutalii Kenya? Je, tutakosea iwapo tutasema TFF wamegeuza Karume kuwa kijiwe na ofisi zile hazina majumuku tena?
Turejee kwenye timu za vijana za klabu. Vijana walioshiriki kwenye michuano hii wanatoka katika klabu 12 zinazoshiriki Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara. Vijana hawa wamesajiliwa na klabu zao kwa mujibu wa kanuni.
Moja ya masharti ya klabu 12 za Ligi Kuu ni kuwa na timu za vijana wasiozidi umri wa miaka 20. Vijana hawa wanahudumiwa na klabu zao kwa mwaka mzima.
Cha kushangaza, kama sio kusikitisha ni kwamba kwa mwaka mzima wanapangiwa kushiriki mashindano kwa wiki mbili tu. Basi.
TFF wanahubiri kuwa mtindo wa kuwa na klabu za vijana ndiyo njia sahihi ya kukuza soka la vijana. Lakini mchezaji gani akae mwaka mzima bila kushindana, halafu akuze kipaji, stadi na kiwango chake kwa mashindano ya wiki mbili?
Michuano ya klabu za vijana inabeba jina la “Uhai” kutokana na kudhaminiwa na kampuni inayotengeneza maji safi ya kunywa ya Uhai, Bakhresa Food Production.
Mwaka huu vijana wa Azam FC wamechukua ubingwa kwa mwaka wa pili mfululizo, kwa kuitandika Simba 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Ubingwa mbali. Lakini ukiangalia utedaji wa TFF unaona kuwa unatia shaka, ingawa ni haohao tunaotegemea watufikishe walikofika Nigeria, Ivory Coast, Cameroun, Misri, Ghana, Tunisia, Angola na nchi nyingine zilizopiga hatua ya soka katika bara la Afrika.
Kama kweli tunataka kukuza soka letu lazima tuwe na mashindano ya vijana yatakayochezwa kwa msimu mzima. Si tu mashindano kwa ajili ya vijana wenye umri wa miaka 20, bali hata wa miaka 17 na 15.
Lakini kwa mashindano ya wiki mbili, katika mwaka mzima, kile wanachofanya viongozi wanaopanga mashindano ya aina hii, kama si ubabaishaji ni kitu gani?
Klabu nyingi kama siyo zote nchini ni masikini. Kuzilazimisha kusajili timu za wachezaji vijana kunaonekana kuwa jambo sahihi na la busara.
Lakini kwa timu ambazo zimekaa tu au zinafanya mazoezi madogo ya hapa na pale; tena kwa kugharimiwa na klabu kwa mwaka mzima; halafu zikapewa wiki mbili tu za mashindano, hakika ni kuwekeza katika sifuri.
Baadhi ya klabu zilisajili wachezaji wa timu za vijana kutimiza kanuni na baada ya hapo kuwaachia wachezaji kuingia mitaani. Wameitwa juzi tu kushiriki michuano.
TFF haijajihusisha kikamilifu kuhakikisha kuwa timu za vijana zinakuwepo kweli, zinafanya mazoezi na ni hai kwa kila hali. Hivi soka letu linaweza kukua kwa mtindo huu?
Bahati mbaya mashabiki wengi wa soka Tanzania ni “vipofu.”
Ukiwauliza nani anayedidimiza maendeleo ya soka la nchi hii, wengi wao watakujibu kwa sauti kubwa “Maximo.” Huu ni upofu.
Ukiwauliza sababu, watakwambia Maximo amewachukia Juma Kaseja, Athuman Iddy Chuji na Haruna Moshi Boban. Huu ndio upofu.
Tena wanapiga kelele wakiitaka TFF kumfukuza Maximo, eti hafai, atimuliwe, wakidai “hambiliki.” Hii ni kwa kuwa mashabiki wana wachezaji wao wanaotaka kuwaona timu ya taifa.
TFF wanasema tumesikia kelele za mashabiki, lakini kwa hili la Maximo liko juu yetu kwa sababu ameletwa na rais. Analipwa na serikali. Hivi ndivyo TFF inavyojitetea kwa kuwapiga mashabiki changa la macho.
Kama wanashindwa kumwambia chochote Maximo kwa sababu ameletwa na rais, je, huyu kocha wa vijana naye ameletwa na Kikwete?
Je, analipwa na serikali? Ni Kikwete aliyemwambia aende Kenya kutalii? Au Maximo ndiye ametaka kwenda naye Kenya, na wao TFF kwa kumuogopa wakamwambia “sawa mzee?”
Iwapo serikali na TFF hawatakuwa na mipango endelevu kwa vijana, tutaendelea kuwalaumu makocha mpaka mwisho wa dunia; na hakuna hatua yeyote tutakayopiga katika soka.