Yanga: Mbinu au woga kwa Ahly?

KITENDAWILI cha Yanga cha ama kuendelea na safari ya kuusaka ubingwa wa Afrika au kurudi mchangani kusubiri ratiba ya mwaka 2010, kinatarajiwa kuteguliwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Utakuwa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya wiki mbili zilizopita Yanga kukubali kipigo cha mabao 3-0 mbele ya mabingwa watetezi wa soka barani Afrika, Al Ahly ya Cairo, Misri.
Kwa Wanayanga, kilikuwa kipigo kizito, ingawa si kigeni mbele ya Waarabu kwa sababu hata siku moja haijawahi kujitetea mbele yao.
Lakini kilikuwa kipigo kizito kutokana na Yanga ya sasa ilivyosheheni nyota wa kweli wa soka waliomgharimu bilionea Yussuf Manji kiasi cha shilingi za Kitanzania nusu bilioni!
Ukiachilia mbali kikosi kilichoshiba wachezaji mahiri, Yanga ina jopo zito la ufundi, likiwa na makocha watatu kutoka Ulaya wakiongozwa na Profesa Dusan Kondic.
Na zaidi ya yote, Yanga ya sasa si ile ya walia njaa. Hii ya sasa inajiweza kimipango na mikakati, ingawa kupitia fedha za Manji.
Wanachopaswa kufanya viongozi wa Yanga na wadau wengine wa kamati ya ufundi ni kupanga mikakati ya ushindi, mambo mengine yanamalizwa na Manji, basi!
Ndiyo maana kwa Wanayanga, kipigo cha Ahly kiliwaumiza, kwani ukiondoa dosari za uwanjani, hawakuwa na sababu za msingi za kupokea kipigo kikubwa cha aina hiyo.
Pengine kwa kuamini kuwa walitekeleza, ama kwa mchecheto au kwa kuzidiwa mbinu, viongozi wa Yanga wamekuwa wakitamba kwamba, piga ua, Ahly haitatoka salama Dar es Salaam.
Na katika kuthibitisha hilo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesikika likiishangaa Yanga kwa kuukataa uwanja mpya na wa kisasa wa Taifa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000 kwa wakati mmoja, na kung’ang’ania uwanja wa kale ambao ni wa kizamani na mdogo, ukiwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 25,000 tu?
Lakini Mwenyekiti wa Yanga, amewaacha midomo wazi wanazi wa soka nchini kwa kutetea uamuzi wa klabu yake, akidai uwanja wa kisasa ‘utawazingua’.
Eti nyota wamezoea kucheza `mchangani’ ambako wana uhakika wa kuibuka na ushindi mnono wa kuweza hata kuwavua ubingwa Ahly!
Mmh! Yawezekana, na hiyo ndiyo dua ya Watanzania kuona pesa nyingi zilizotumika kusajili kikosi cha michuano ya kimataifa hazipotei bure.
Kama ndoto hizi zikitimia, Yanga itakuwa imeua ndege wawili kwa jiwe moja, kwanza ni kuonja ushindi mbele ya klabu kutoka mataifa yenye asili ya Waarabu na pili ni kuwafungasha virago mabingwa watetezi, historia iliyowekwa na Simba mwaka 2003 ilipoing’oa Zamalek.
Lakini cha kujiuliza ni kwamba, kwa klabu kongwe na yenye kufahamu mbinu za soka kama hii, ilistahili kukimbia uwanja? Hili linaleta mashaka makubwa juu ya uthabiti wa maandalizi ya Yanga katika kurudiana na Ahly.
Kwa timu yenye kujiamini, uwanja isingekuwa habari kubwa, na pengine ingehitaji mikakati zaidi ya kiufundi kuliko imani nyingine.
Aidha, tulitarajia Yanga ingefurahia uwanja wa kisasa kwa sababu kadhaa, baadhi zikiwa ni kuwa na uhakika wa kupata umati mkubwa wa mashabiki wa kuipa timu sapoti, na hata kama mambo yatakwenda vibaya (hatuombei), timu itajipoza kwa kuvuna kitita kikubwa cha fedha, tofauti na senti za uwanja wa zamani.
Kwa tafsiri rahisi ni kwamba, Yanga ingelenga kote, kuibuka na ushindi, tena mnono na wakati huohuo kuwapa nafasi wafuasi wake wengi kuweza kuingia uwanjani kuishangilia timu, huku kwa upande mwingine wakisaidia kutunisha mapato ya klabu.
Na katika hili, Yanga inapaswa kuwa imara kweli kweli, kwani tayari `fitna’ yao imeshanaswa na Ahly wanaodai wapo tayari kucheza popote, huku wakitoa mifano ya kuzigalagaza timu kama ASEC Mimosas ya Abidjan, Ivory Coast licha ya kuchezeshwa kwenye viwanja vya ajabu.
Tujiulize, kama Yanga ikishindwa kutimiza ndoto kama `anayoiota’ Madega, itakuwa na lipi la kujivunia angalau kwa kupata nafasi ya kucheza na timu bora kabisa barani Afrika? Bila shaka hakuna.
Ndiyo maana tunashauri, pamoja na kuwa Yanga itacheza nyumbani, mbele ya mashabiki wake wengi na hivyo kujawa na matumaini ya ushindi, juhudi pia zinapaswa kufanywa katika kuiandaa timu.
Hili likizingatiwa, hakuna kitakachoizuia Yanga kuibuka na ushindi, hasa ikizingatiwa kwamba, pamoja na kushindwa kuwatambia Waarabu miaka nenda miaka rudi, angalau Dar es Salaam imekuwa ikipata matokeo ya kuridhisha, yaani sare.
Kama miaka yote sare zilipatikana nyumbani na `kuachia’ ugenini, kwanini timu bora kama ya 2009 isiweze kufanya makubwa zaidi?
Dawa ni maandalizi, si kukimbia uwanja.Mathalani, miaka nenda miaka rudi Simba imekuwa ikilia na uwanja wa Sokoine, Mbeya, kiasi cha kutopindua mbele ya Prisons, lakini kwa timu zinazojiandaa, Prisons kuna wakati inakubali kipigo kwenye uwanja huo huo unaolalamikiwa na Simba.
Msisitizo ni kwamba, maandalizi ya dhati yatangulie, ndipo fitna zimalize kazi.