Yanga, Mungu awape nini tena?

NIANZE kwa kuupongeza uongozi wa Yanga, chini ya Mwenyekiti Imani Omar Madega kwa kuamua kuachana na ubabaishaji, na hatimaye kuonekana kushika njia sahihi ya uendeshaji wa kisasa wa klabu.
Ninazungumzia uamuzi sahihi, usio na chembe ya mashaka wa kuiweka kambi ya timu hiyo katika makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, kariakoo jijini Dar es Salaam .
Kabla ya kutangazwa kwa uamuzi huu mwishoni mwa wiki, nilikuwa napata taabu kuwaelewa viongozi wa Yanga baada ya kusikia walikuwa wanasuka mikakati ya kuipeleka kambi ya timu hiyo Jijini Mwanza.
Sikuwaelewa hata chembe. Kwamba, inakuwaje ukarabati mkubwa wa jengo la makao makuu limekamilika, lakini bado klabu iingie gharama za hoteli kwa ajili ya kambi ya timu?
Kamwe isingeingia akilini, na bila shaka hatua hiyo ingewasikitisha wadau wengi, akiwamo bilionea aliyepania kuikomboa klabu hiyo, Yussuf Mehboob Manji aliyejitolea kufanya ukarabati unaotajwa kugharimu zaidi ya sh bilioni 1.2!
Lakini kwa kuwa Madega na wenzake wameona mbali, ndiyo maana nachukua hatua hii kuwapongeza kwa busara yao ya kuamua kubana matumizi ya klabu.
Kimsingi, Yanga ni kama imezaliwa upya 'kiakili', kiasi cha kutaka kurejesha hadhi ya klabu yao .
Ukarabati mkubwa wa vyumba 39, vyenye kila kitu ikiwa pamoja na viyoyozi, ofisi za viongozi, makocha na maofisa wengine, chumba cha mikutano, mgahawa, baa, sehemu ya mazoezi na bwawa la kuogelea, ni hatua kubwa ya kupongezwa.
Na kubwa zaidi linalotarajiwa kukamilika wakati wowote ni Uwanja wa Kaunda ambao unaweza kutimika kwa mechi za Ligi Kuu!
Nasisitiza, kukamilika kwa haya ni sawa na kuzaliwa upya kwa Yanga iliyokuwa imeyaasi makao yake makuu, hasa kwa upande wa kambi kwa takribani miaka 20.
Hata hivyo, busara yao isigeuke kiini macho mbele ya wanazi wa Yanga, timu kongwe za soka kuliko zote nchini ambayo bado iko hai na iko matawi ya juu.
Kwamba, kwa kuwa imeamua kubana matumizi makubwa ya fedha yaliyokuwa yanakwenda katika hoteli za watu binafsi, sasa klabu iwe na mikakati ya dhati ya kutunisha hazina yake.
Haitapasua kichwa pahala pa kulaza wachezaji, sehemu ya mazoezi na hata kulazimika kukodi uwanja kwa ajili ya mazoezi.
Badala yake, ni Yanga ndiyo itakayonufaika kama ikiamua kutumia vitegauchumi vyake kuzalisha pesa na hivyo kuifanya klabu ya kisasa zaidi.
Jamani, kama haya yalishindikana kwa miaka nenda miaka rudi, lakini sasa yanawezekana, Mungu awape nini Wanayanga?
Kwa kuwa Mungu amemshusha 'Malaika Manji' ndani ya Jangwani, kamwe Wanayanga wasigeuka pepo wa kuchafua hali ya hewa ndani ya klabu hiyo.
Wanapaswa kushikamana zaidi na kubuni mikakati ya kuziba mianya yote ya upotecu wa fedha, na badala yake waisake mianya ya kuingiza fedha, ili kuanza kuzifuata kwa kasi klabu nyingine zilizopiga hatua kisoka duniani.
Kwa kufanya hivyo, si kwamba Yanga itakuwa imezizindua klabu nyingine kama Simba ambazo kwa sasa zinatamba kwa habari za 'migogoro' ya viongozi wake, bali hata nyingine za ndani na nje ya nchi.
Staili hii ya uendeshaji soka inayoelekea kuonekana Jangwani, ndiyo inayopaswa kukumbatiwa, kwani hata klabu tajiri, tuchukuliea mfano za hapa Afrika kama Al Ahly ya Misri na ASEC Mimosas ya Ivory Coast zilianzia chini.
Lakini kwa kuwa zilidhamiria, ni nani anayeweza kuzichezea leo hii kifedha? Bila shaka hakuna, ndiyo maana Ahly ina jeuri hata ya kumzuia nyota wake Amr Zaki asirejee England msimu ujao, kwani wana jeuri ya kumlipa.
Yanga nao wanapaswa kusimama katika mstari huo, kwani uimara wa nguvu za kiuchumi, ndio utakaotengeneza soka maridadi ya kuitikisa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Hilo likiwezekana, hata wafadhili nao watapapatika kumwaga mapesa, wakiamini watajitangaza zaidi kupitia Yanga.
Nihitimishe kwa kusema, huu ni mwanzo mzuri kwa Wanayanga, washikamane na kusonga mbele, badala ya kurudisha kule kulikoacha maswali mengi, kiasi cha kumlazimu kocha maarufu hayati Tambwe Leya kutunga kitabu: "Yanga, Meli Kubwa Isiyo na Nahodha."
Safari imeanza, kamwe Yanga chini ya Madega na wengine watakaofuatia wasiturudishe nyuma.