Yuko wapi mgombea anayeifaa Zanzibar ?

- Makada 11 CCM wataka urais
ZIPO hekaheka kubwa Zanzibar katika kipindi hiki. Tumeona nani na nani wamechukua fomu kuomba vyama vyao viwapitishe kugombea urais, wadhifa wa juu kabisa katika nchi.
Inajulikana wazi ushindani mkali wa nafasi hii unatarajiwa kwa vyama viwili vikuu: Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Hakuna chama kingine kilichofanikiwa kupata wafuasi wengi wa kushindana navyo. Hakuna tangu mwaka 1992 wakati mfumo wa vyama vingi uliporudishwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Ikifika Oktoba mwaka huu, kiti cha urais kitakuwa wazi kwa kuwa anayekishikilia tangu Novemba 2000, Amani Abeid Karume, anamaliza muda wake uliowekwa na katiba.
Kama kawaida, hakuna kishindo kwa CUF katika kupata mgombea wake. Imejengeka kuwa kila unapofika uchaguzi mkuu, kinamtegemea kiongozi wake muasisi Maalim Seif Shariff Hamad kuwania akipambana na mgombea wa CCM.
Mara tatu amegombea lakini mwenyewe anasema, “mambo hayajakubali.” Safari hii ameingia tena na anasema ataukwaa urais kwa sababu “sasa yapo mazingira mazuri ya kufanyika kwa uchaguzi ulio huru, wa haki na kwa njia ya uwazi.”
Tayari Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, amepigiwa kura na mkutano mkuu maalum wa chama za kumuidhinisha kugombea.
Lakini kwa upande mwingine, kama ilivyo kawaida, kuna vishindo kwa CCM katika kumpata mgombea wake. Makada 11 wamejitokeza kuchukua fomu ili kutafuta uteuzi. Nini kama si vishindo.
Saba kati yao – Shamsi Vuai Nahodha, Ali Abeid Karume, Ali Juma Shamhuna, Bakari Hamad Mshindo, Mohamed Gharib Bilal, Mohamed Aboud Mohamed na Ali Mohamed Shein – walichukua siku moja 21 Juni uchukuaji fomu ulipofunguliwa.
Omar Sheha Mussa, mbunge wa Chumbuni tangu 2005, na ofisa mwandamizi serikalini, alifuata 23 Juni. Makada watatu wengine, Mohamed Raza, Haroun Ali Suleiman na Mohamed Yussuf Mshamba walichukua fomu 24 Juni.
Kila mmoja alikutana na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu. Wakajilabu na wakajibu maswali mawili-matatu ya waandishi.
Kwangu ilikuwa ni mikutano ya maonyesho tu si ile niliyoitarajia itoe nafasi kwa waandishi kuuliza maswali ya kuwapima wagombea. Hakuna aliyetimiza saa mbili za kujibu maswali. Baadhi hata saa moja haikufika.
Kumbukeni wakati taifa likielekea kupata rais wa kwanza ndani ya mfumo wa siasa wa vyama vingi mwaka 1995, Mwalimu Julius Nyerere alitumia zaidi ya saa mbili kueleza mbele ya waandishi wa habari, sifa za kiongozi anayeifaa Tanzania ya leo.
Baada ya kuchukua fomu, kila mmoja aliingia mbioni kutafuta wanachama wa kumdhamini. Ni hapa mikakati ya kutafuta kujulikana hata kwa miongoni mwa wana CCM watakaoshiriki vikao vya juu vya chama iliposhamiri.
Shamsi alikimbilia Dodoma . Wakafuatia Shein na Bilal ambao wanahudhuria vikao hivyo kwa nafasi zao. Shamsi akaibukia bungeni. Akatambulishwa na Spika Samwel Sitta kwa wabunge. Siku ya pili akaibukia studio za TBC1 mjini Dodoma katika kipindi cha Jambo Afrika Jambo Tanzania akiulizwa na mtangazaji mahiri Marin Hassan Marin.
Baadae akatua studio za Star Tv mjini Dar es Salaam katika kipindi cha Tuongee asubuhi akiulizwa na mtangazaji chipukizi Flora Mallya na kwenye studio kuu za mjini Mwanza akiwapo mkongwe Samadu Hassan. Ile ni mikakati ya kujitanua na kujitangaza.
Vishindo katika kupata wanachama wa kudhamini vilikuwa si haba. Misafara ya Shein ilipata tabu kukubalika huku kukiwa na ishara ya ngome kuu za Bilal. Kijijini Bambi, ndani ya jimbo la Uzini, ikatokea shaghalabaghala.
Wanachama waliokuwa wametia saini zao katika fomu za Shein ambaye wapambe wake walitangulia kufika, wakafuta majina na kurudisha ‘chenji’ waliyokuwa wamepokea. Kisa? Walidanganywa kwani wao walikuwa wamejiandaa kumdhamini Bilal.
Nini kama si vishindo maana wote hawa ni viongozi wa CCM. Itakuwa mambo yamewekwa sawa na wenye kazi zao ili kumwezesha Shein, Makamu wa Rais wa Tanzania , kudhaminiwa.
Wakati makada wengine wanafanya mambo yao kimyakimya na kwa uhakika, kambi ya Bilal haijali chochote. Inaonyesha hasa ilivyo nguvu kubwa visiwani. Hamkani kila mahali mjini na vijijini.
Waliandaa makundi ya wanachama kutoka mashamba hadi Mwembekisonge, ilipo maskani kuu ya CCM. Kucheza ngoma, kula na kunywa. Kutwa nzima tangu kumekucha.
Kundi likamfuata Bilal nyumbani kwake baada ya kurudisha fomu. Huko aliita waandishi. Karibu wagome kwa kuwa chumba kilijaa makada. Baada ya Bilal kujibu maswali mawili-matatu, akaruhusu aliowaita “wazee wa chama” wahutubie.
Hawa ni wazee walioshuhudia na kushiriki harakati za kuondoa serikali ya uhuru kupitia kilichoitwa Mapinduzi ya 12 Januari 1964. Wamo pia watu walioshiriki kutesa wananchi kwenye ile nyumba maarufu ya “Kwa Bamkwe.”
Wakasema kwa sauti kali na za kutisha ikiwemo kuitahadharisha NEC ya CCM kwamba isipomteua mtu wao, hapatatosha. Walisema wataondoka Dodoma kurudi Zanzibar na ASP yao . ASP ni chama kilichoongoza mapinduzi na ambacho kilipoungana na TANU 5 Februari 1977, kilizaliwa CCM. Kama kweli, sijui watakisajili wapi.
Labda wanatisha baada ya kuona bahari imechafuka; upepo mkali na mawimbi ni makubwa mno kiasi cha kutishia “chaguo” lao. Watajua wenyewe CCM maana hayo ni mambo yao na hao wasemaji ni wanachama wao.
Kwenye baraza za watu katika miji na vijiji Zanzibar kumejaa minong’ono eti chaguo la CCM au tuseme “wakubwa” ni Shein maana inadaiwa amepata ridhaa ya Rais Jakaya Kikwete na ndiye chaguo mbadala la Rais Karume, baada ya kukosa mwandani wa kumsukuma agombee. Si vishindo hivi?
Kufikia Jumatatu jioni, mbali na Bilal, waliorudisha fomu walikuwa Mshindo, Shein, Karume, Aboud na Shamsi. Ilitarajiwa hata Shamhuna alipanga kurudisha juzi.
Kwa vyovyote vile, vishindo ni vikubwa kutokana na kundi kubwa la makada wa CCM kutaka urais. Watu wanajiuliza mbona wengi hivi? Kwani wanagombania nini? Ikulu ipi? Ile ambayo anayeikalia lazima awe kiongozi muadilifu, mpenda nchi na watu wake? Mpenda marafiki wa Wazanzibari; mtiifu kwa katiba na sheria; mlinzi mzuri wa raslimali za Wazanzibari na bila shaka mtetezi wa muungano?
Najiuliza hivi kati yao yupo hasa mwenye utashi wa kufanya mapinduzi katika kila nyanja ya maendeleo kwa kuwa Zanzibar haina uchumi; utamaduni wake unapotea kwa kasi; haina ukarimu tena; serikali yake inategemea wahisani kwa kila kitu.
Nchi ipi? Hii ambayo inaumwa ugonjwa wa ukabila kwa misingi ya Unguja na Pemba iliyopandikizwa na viongozi wachafu tangu enzi? Viongozi waliopandikiza kasumba ya kutunukua kazi kwa kujuana hata kama mtu hana ujuzi wala sifa? Siku hizi ni watu kutafutana huyu kazaliwa au ana asili ya wapi?
Zanzibar ipi? Hii inayopambana kwa nguvu na Serikali ya Muungano katika kujikwamua kutoka umasikini uliokithiri? Nchi ambayo inalea ufisadi na uzembe serikalini? Nchi inayotumaini kuchimba mafuta lakini inalazimika kwanza kutunisha misuli dhidi ya ukomandoo wa CCM Bara?
Naona urais wa Zanzibar ni kazi nzito na ngumu. Kazi inayohitaji mtu makini kwa vigezo vyote vya uongozi bora au uongozi uliotukuka. Sasa je, kati ya hao 11 kutoka CCM peke yake, wangapi wanajiamini kuitoa nchi kimasomaso?
Zanzibar inataka kiongozi mwenye hekima na busara katika kuongoza watu. Kiongozi anayewaheshimu watu. Yupo kati yao ? Au tumeona makada wanaojipenda zaidi wenyewe na familia zao na rafiki zao?
Tatizo baadhi yao wamefisidi uchumi na kutumia walichochuma kujenga utajiri wao katika familia zao; wapo waliotoa ahadi za uongo kwa wananchi walipokuwa mawaziri au chini ya hapo. Hawa hawatibu watoto wao Zanzibar bali karibu ni Afrika Kusini.
Wapo waliodhulumu wananchi binafsi nyumba, mashamba na ardhi. Wapo walioeneza siasa tenganishi; wakafukuza watu kazini.
Ninaona ipo kazi kwa CCM kuleta mgombea muadilifu. Tutaona.