Zambi: Kafulila mzushi bungeni


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version
David Kafulila

MBUNGE wa Mbozi Mashariki, Godfrey Weston Zambi (CCM) ana amani moyoni. Kitu kinachomfanya atembee akiwa na amani ni namna alivyofanikiwa kuwaaminisha wapigakura wake kwamba yeye ni mtu safi licha ya shutuma kuwa ni mla rushwa alizotupiwa bungeni.

Akijipima uaminifu wake, akitazama utendaji kazi wake, akiangalia ushirikiano na wenzake, anajipa nguvu kuwa rekodi haijaathiriwa na madai ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila aliyemtaja kuwa ni miongoni mwa wabunge wala rushwa.

Tuhuma hizo hazikuchafua hadhi yake tu mbele ya jamii, bali pia zilimweka pabaya katika jimbo lake. Kazi ikawa kujisafisha kwa wapigakura wake na kusafisha hali ya hewa jimboni.

“Mbozi walipokea vibaya madai yale, na kwa kweli kama nisingesimama imara kuwaambia ukweli jimboni, shutuma hizi zingepunguza hadhi yangu,” alisema Zambi alipozungumza na MwanaHALISI mwishoni mwa wiki iliyopita.

Anasema, “…ila nashukuru nimeeleweka na Kafulila anaonekana anabwata tu.”

Katika mkutano uliopita wa Bunge, Kafulila aliwataja wabunge watatu wa CCM kwamba wanakula rushwa. Mbali ya Zambi, wengine ni Omary Badwel (Bahi) ambaye amenaswa tena hivi karibuni na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na Zabein Mhita (Kondoa Kaskazini).

Kafulila alidai kwamba wabunge hao hawakuonyesha uaminifu na uadilifu wao wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) katika ziara ya mkoa wa Tanga.

Tangu hapo kibarua kikawa kwa Zambi kujisafisha kwa wananchi. Lakini pamoja na kuchafuliwa jina na hadhi yake mbele ya jamii, anasema hana mpango wowote wa kufumshitaki Kafulila kwa kile alichodai “mbunge wa Kigoma Kusini ni mtu wa vurugu”.

Anasema, “…huyu mtu anayeitwa David Kafulila ana matatizo; anawaza vurugu na ugomvi wakati wote. Ndiyo maana ameshindwa kukaa katika vyama vya CHADEMA na NCCR-Mageuzi. Sasa anataka kuvuruga kazi za bunge.”

Ushahidi wa Zambi ni matukio mawaili ya kufukuzwa uanachama. Tarehe 18 Novemba 2009, Kafulila alijitoa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kuibuka kutoelewana na viongozi wenzake na akajiunga NCCR.

Huko alipokewa, akagombea ubunge akashinda. Lakini alizusha balaa na tarehe 18 Desemba 2011 alifukuzwa katika chama hicho pamoja na wajumbe wengine sita.

Zambi anasisitiza rekodi hizi si nzuri, “…haiwezekani kwa mwanasiasa ukawa unatimuliwa tu kwenye vyama vya siasa.”

“Nimechoshwa na vurugu za Kafulila. Sitaki tena kuchafuliwa. Nadhani sasa tufikishane kwenye vyombo vya sheria kama suala hili lipo au halipo,” anasisitiza mbunge huyo.

“Kafulila hana uhakika na anachodai. Kwanza anasema ametukamata, lakini pili anasema ametusikia tukipanga mipango ya kuomba rushwa. Mbona hakutoa taarifa TAKUKURU au polisi waweke mtego? Huyu mtu wa ajabu sana!,” anasema Zambi.

Mbunge huyo alipoulizwa kama yuko radhi kujisafisha kwa kumfikisha Kafulila kwenye vyombo vya sheria, alisema hana mpango huo.

Anasema maadamu hajawahi kuitwa kwa mahojiano na TAKUKURU wala kushikiliwa kwa mahojiano juu ya undani wa suala hilo anaona Kafulila “amefulia” kwani hana hoja.

Alipoulizwa itakuwaje ikiwa Spika wa Bunge, Anne Makinda atavunja Kamati ya LAAC ambayo yeye ni mjumbe, Zambi alisema haoni uwezekano wa Spika kuvunja kamati hiyo.

“Sidhani kama spika ataivunja kamati hii. Namna inavyofanya kazi kwa uadilifu, naona Kafulila anapiga porojo tu. Kafulila ni nani hata spika amsikie kwa hili?” alihoji.

“Mtu mwenyewe hahudhurii vikao, sasa akijitoa ni sawa tu kwa sababu si mchangiaji na mhudhuriaji mzuri. Kwanza kamati imemchoka sana, tena sana na haifurahishwi na matendo yake,” anasema.

Jambo linalomfurahisha sasa ni kwamba ameeleweka Mbozi, anasema hawana nongwa naye. “Kwa bahati nzuri mimi ni msemakweli. Wananchi wa Mbozi wana imani na mimi na ndiyo maana nilirejea tena bungeni katika uchaguzi wa mwaka juzi (2010).”

Zambia aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2005 baada ya kumng’oa Edison Halinga, anajivunia pia tathimini iliyofanywa na watafiti waliokuwa wanafuatilia michango ya wabunge na kumpa nafasi ya saba ya ubora kati ya wabunge zaidi 340. Katika Bunge la Tisa, Zambi alikuwa mjumbe katika kamati ya miundombinu.

Alipoulizwa kama atapenda kuendelea katika kamati hii hadi kipindi cha bunge kitakapomalizika mwaka 2015, alijibu kwamba huo ni uhuru na mamlaka ya spika kwani hii ya LAAC hata ya miundombinu alipangwa tu na spika.

Je, yeye ni miongoni mwa wapinzani ndani ya CCM? “Hapana,” alijibu. Amesema yeye anasukumwa na kusema ukweli na kuwatumikia wananchi katika kazi ya mbunge ya kuishauri na kusimamia serikali.

Mbunge huyo anajivunia kutekeleza mambo kadhaa ya maendeleo katika jimbo lake, kama kuweka umeme ambapo kwa asilimia 50 ya vijiji 117 vya Mbozi Mashariki vitapata umeme kabla ya mwaka 2015.

Hata hivyo, kilio chake ni hali iliyojengeka ya kupuuzwa kwa watu wa Mbozi na Mbeya katika suala la kuzalisha zao lao la Kahawa. Anaona wakulima wa kahawa Mbozi wanaonewa kimsingi kutokana na kulazimishwa na Bodi ya Kahawa kuuza kahawa mbini (Red Cherry).

Mfanyakazi huyo wa zamani wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kuanzia mwaka 1994 hadi 1997 anasema biashara ya kuuza kahawa mbichi inanyonya wakulima wadogo.

“Bei ya kahawa bora msimu uliopita ilikuwa Sh. 12,000 kwa kilo. Sasa kitendo cha bodi kudai kwamba ilikaa katika kikao huko Moshi, Kilimanjaro na kuidhinisha ununuzi wa kahawa mbichi si kweli,” alisema Zambi.

“Kikao cha bodi na wadau wa kahama kwa mara ya mwisho kilifanyika Morogoro, Mei mwaka jana na suala la kununua kahawa mbichi halikupitishwa. Halimo kwenye maazimio,” anaeleza.

Anafafanua zaidi kwa kusema, “…maazimio yalikuwa kwamba bodi inapaswa kuratibu tathimini ya kina ya mfumo wa sasa wa biashara ya kahawa kwa nia ya kuwa na mfumo wa uwazi utakaokuwa shindani katika mnyororo wa thamani.”

Zambi anasema kwamba kwa mfumo wa kununua kahawa mbichi ni njia ya kumdidimiza mkulima mdogo kwa sababu ongezeko la thamani halitakuwako kwenye ushindani sokoni.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: