ZEC katika mtihani mgumu


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 18 March 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inakuja tena kwenye muonekano. Inakabiliwa na kipimo cha uadilifu.

Wapo wanaosema hii ni tume tofauti na iliyosimamia uchaguzi tangu 1995. Sikubaliani nao. Angalau hii iliyoteuliwa mwaka jana ina tofauti na ile ya 1995.

Tume hii ya Mwenyekiti Khamis Mwinchande, kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), haina tofauti yoyote na iliyoongozwa na Masauni Yussuf Masauni; ile iliyosimamia uchaguzi wa 2005.

Tofauti kati yake ni ule msemo wa mvinyo mpya ndani ya chupa ya kale. Wanaojua vizuri uchaguzi unavyoendeshwa nchi nyingi za Afrika, wanajua uchaguzi si Tume kwa maana ya wale makamishna.

Nguvu ya Tume ni sekretarieti inayoundwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi akisaidiwa na maofisa wa serikali wenye majukumu ya kitaalamu. Hawa ndio mabingwa wa sayansi mbalimbali.

Hawa hujenga mtandao na wanausalama ili kuhakikisha matokeo ya uchaguzi yanalingana na matakwa ya kinachoitwa “maslahi ya taifa.” Ukweli haya si maslahi ya kweli ya taifa, bali ya watawala wanaotaka kubaki madarakani.

Tume ya sasa, kama ilivyo ya 2005, inaundwa na makamishna wa vyama viwili vya siasa: CCM na Chama cha Wananchi (CUF) kufuatia muafaka wa kisiasa wa 2001 uliolazimisha mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Kila chama kina makada wake wawili. Rais huteua wajumbe wawili kwa mashauriano na Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi.

Rais ambaye ni kiongozi wa chama kilichounda serikali baada ya uchaguzi, huteua mtu mwingine kwa kadri anavyoona inafaa anayekuwa mwenyekiti wa tume na watu wengine wawili wanaotajwa kikatiba kama wenye hekima.

Mwinchande, kwenye tume iliyosimamia uchaguzi wa 2005, aliteuliwa kama mmoja wa makamishna wawili kutoka CCM na akawa makamu mwenyekiti. Ndio kusema ni kada wa CCM.

Wakati wa uteuzi, Masauni alikuwa ofisa uhamiaji mstaafu, kazi iliyomlazimu kupitia itikadi ya CCM hasa kwa kuwa aliajiriwa kama askari.

Aliongoza tume iliyopuuza malalamiko mengi ya vyama vya upinzani wakati wa uandikishaji watu kwa ajili ya daftari la kudumu lililoanzishwa mwaka 2005.

Alikuwa mgumu kukutana na waandishi wa habari. Alipothubutu, alikwepa au kubeza maswali ya msingi yaliyotokana na malalamiko ya wananchi, achilia mbali yale yaliyotolewa na vyama.

Baada ya kukubali kuburuzwa na mtandao wa kiusalama uliopata nguvu ya wataalamu katika tume, Masauni alijikuta kama mwenyekiti asiye na mamlaka yoyote ya kuamua jambo. Inaelezwa kuwa hata alipotaka kujiuzulu, alitishwa.

Matokeo yake baada ya uchaguzi, akijua alishiriki kuridhia mikakati ya kuhujumu uchaguzi, alikubali angalau kukiri katika ripoti ya uchaguzi, kuwa viongozi wa serikali waliingilia sheria na taratibu za uchaguzi.

Alikiri pia kuwepo zaidi ya watu 3,000 waliojiandikisha zaidi ya mara moja. Hata hivyo, alishindwa kuwasilisha polisi vielelezo ambavyo vingewezesha kuwashtaki mahakamani.

Hakushindwa kwa bahati mbaya. Ni mpango uliobuniwa ili kusaidia mikakati ya ushindi ya CCM. Katika kufanikisha hilo, hata mara moja serikali ya CCM haitakubali kutoa kafara mamluki waliosaidia kufanikisha “ushindi wa kishindo.”

Wakati wote wa mchakato wa uchaguzi, Masauni na timu yake – baki wale makamishna wa CUF – walikuwa wakitoa kauli za kusimamia sheria na taratibu za uchaguzi.

Hata Mkurugenzi wake, Khamis Ali Ame, ambaye baada ya uchaguzi aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa kamishna wa Tume ya Pamoja ya Fedha ya Muungano (JFC), alikuwa akikwepa maswali yaliyohusu kasoro za utendaji wa tume.

Basi ndivyo alivyoanza Mwinchande na timu yake. Sheria, sheria, sheria. Hawa wamekwenda mbali zaidi kwa kusema, “Hatutafuata shinikizo za mtu yeyote au chama chochote cha siasa katika kutekeleza wajibu wetu.”

“Kila kitu tunachokifanya kitakuwa kinafuata sheria na taratibu zilizowekwa kulingana na Sheria ya Uchaguzi na Katiba ya Zanzibar,” ndivyo wanavyosema katika mikutano ya wadau wa uchaguzi, ikiwemo iliyohudhuriwa na waandishi wa habari.

Ndani ya sekretarieti ya Tume wangalipo maofisa watendaji kama Kassim Kadu Masego na Maalim Mbarak Ali. Ni wazoefu wa fani zao tangu tume ya mwaka 1995. Khamis Ali Ame ni mfano wao.

Sina ubavu wa kusema ni wazoefu wa uvurugaji taratibu za uchaguzi ambao, kwa asili, huanzia kwenye hatua za maandalizi ya uandikishaji wapiga kura hadi kwenye ujumuishaji matokeo yaliyokusanywa vituoni.

Sina ushahidi. Ninachosema ni kuwa uzoefu walionao maofisa kama hawa katika taasisi yoyote na hasa za umma, unajenga urahisi wa kuweza kutumika kwa minajiri ya kusaidia kufanikisha matakwa ya watawala.

Kwa ushauri wa watu kama hawa, Masauni na timu yake walishindwa kuondoa mivutano kwenye vituo. Tume ilishindwa kurekebisha daftari kwa namna ilivyoamini inafaa, kwani iliridhia utashi wa serikali na kuharibu uhakiki wa daftari.

Tume hiyo ikakataa kutoa mapema daftari hilo kwa vyama vya siasa ili kuangalia dosari. Ililitoa dakika za mwisho na kuharibu maana nzima ya kuwepo kwake; kuhakikisha wale tu wenye haki ndio wanaingia.

Lakini yote hayo, yalitokea kwa mpangilio ulioandaliwa kwa umakini mkubwa na watawala. Ni mpangilio uliolenga kusaidia kufanikisha maslahi ya watawala.

Sasa tunayo tume ambayo imeanza kuonesha ubutu uleule. Tayari imeshindwa ubavu na serikali katika suala la vitambulisho vya Mzanzibari kutumika kama kibali cha mtu kutambuliwa mpiga kura. Tume hii inaandaa uchaguzi mdogo wa uwakilishi jimbo la Magogoni.

Awali,tume ilisema inaandikisha wapiga kura kwa kutumia vielelezo vingine mbali na hicho. Kwamba wapo waliokuwa hawajatimia umri wa miaka 18 wakati wa utoaji wa kitambulisho mwaka 2005, na kwamba wanaweza kuandikishwa sasa wakitoa cheti cha kuzaliwa.

Kwa kujua wapo wananchi hawakupata kitambulisho cha Mzanzibari kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ile ya kutopewa tu haki yao kwa hisia za kisiasa, Tume iliamua kusaidia hawa wapate haki ya kupiga kura bila ya usumbufu.

Tume ilisema itakubali hata hati ya malipo ya umeme, leseni ya biashara na kodi kama uthibitisho wa ukaazi wa mtu ili aingizwe katika daftari la wapiga kura.

Wapi? Siyo tu imebadili msimamo bali pia imeshindwa hata kusaidia waliokosa kitambulisho cha Mzanzibari. Zaidi ya watu 200 wakiwemo wale walioruhusiwa kupiga kura ya Muungano 2005, wamenyimwa hata fomu ya kudai haki yao ya kuandikishwa.

Ukiuliza haya, Tume watasema, “hatujapokea malalamiko yoyote.” Yapelekwe kwa njia ipi wakati maofisa wao hawakutoa fomu? Siku ya mwisho ni kukuta mamia ya watu wamenyimwa haki ya kuchagua.

Kwa mwanzo huu wa Magogoni, sijaona mabadiliko yoyote ya kunishawishi kuwa tume inaweza kutenda kwa uadilifu. Na huu ndio mtihani mpya wa tume isiyokuwa huru asilani.

Ni pale tu idadi ya wapiga kura Magogoni  itakapowekwa wazi, ndipo mwelekeo wa upigaji kura utakapoeleweka. Hatutarajii maajabu.

0
No votes yet